Zanzibar yapata pigo, aliyeimba Subalkheri mpenzi afariki dunia

Unguja. Kifo cha msanii mkongwe wa taarab, Said Mpenzi, kimeacha pigo kubwa kwa Zanzibar, kwani alikuwa mmoja wa wasanii nyota waliotamba ndani na nje ya visiwa hivyo, akiiletea sifa kubwa nchi hiyo.

Msanii huyo alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumanne, Februari 11, 2025. Alikuwa sehemu ya kundi la wasanii waliopigania mapinduzi hata baada ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatano, Februari 12, 2025, Khamis Mbeto, katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo ya CCM, amesema Rais Hussein Mwinyi, makamu mwenyekiti wa CCM Zanzibar, amesikitishwa na kifo cha msanii huyo. Amemtaja kama bingwa aliyewika katika kipindi chake cha usanii.

“Dk Mwinyi amewatumia salamu za pole kwa ndugu, jamaa, marafiki, familia na wananchi wote wa Tanzania na Zanzibar kwa kumpoteza msanii huyo aliyekuwa kipenzi cha wengi kutokana na uwezo wake wa kuimba kwa viwango na ustadi mkubwa,” amesema Mbeto.

Urithi wa muziki

Mwapombe alitamba sana kupitia wimbo wake maarufu duniani, “Sabah Al Kheir Mpenzi, Waonaje Hali Yako”, uliopendwa na kuvuma barani Afrika na duniani kote. Wimbo huo, uliopigwa na Kikundi cha Taarab cha Mila na Utamaduni Zanzibar, ulimshirikisha msanii mahiri marehemu Sami Haji Dau.

Katibu wa Culture Music Club, Taimour Taha, amesema kifo cha msanii huyo ni pigo kubwa kwa sababu alikuwa mcheza, mwimbaji, na muigizaji mahiri.

“Tumepoteza mtu muhimu, mwimbaji na mwasisi wa klabu yetu. Mwapombe alikuwa mmoja wa wasanii wa mwanzo kabisa walipoanzisha kundi letu,” alisema Taimour.

Msanii huyo, anayefahamika pia kwa jina la Mwapombe Hiyari Mtoro, alikuwa kati ya waanzilishi wa kundi lililojulikana kama Shime Kuokoana, lililoanzishwa kabla ya mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1957. Baadaye kundi hilo liliunganishwa na Afro Shiraz Party (ASP) kwa lengo la kudumisha mila na utamaduni wa Zanzibar na Afrika kwa ujumla.

“Walikusanywa vijana hao kupiga taarab na michezo ya kuigiza katika mwaka 1957, kwahiyo walishiriki katika harakati za kudai Mapainduzi mpaka mwaka 1964, baada ya Mapinduzi mwaka 1965 likaundwa kundi la Mila na Utamaduni likakusanya wasanii wengine zaidi ili waanzishe taarab,” amesema katibu huyo.

Mwapombe alikuwa pia mjumbe wa kamati ya Culture Music Club, ambapo alishiriki kuimba nyimbo kama “Said Mpenzi, Mke wa Awali”, akisaidiana na Sami Haji Dau.

“Alikuwa mmoja wa wale walionyanyua klabu yetu; aliimba, alicheza, akaigiza na kushiriki michezo ya kitamaduni kama Mchezo wa Mwafrika, uliochezwa na Culture Music Club,” aliongeza katibu huyo.

Hata hivyo, ilifika wakati ambapo Mwapombe aliamua kupumzika na hakwenda tena kwenye klabu nyingine hadi mauti yalipomkuta.

Kifo chake kimeacha pengo kubwa kwa Zanzibar na ulimwengu wa taarab kwa ujumla. Mungu ampumzishe mahali pema.