Zanzibar mbioni kuanzisha Soko la Hisa, hati fungani ya Sukuk yatajwa

Zanzibar mbioni kuanzisha Soko la Hisa, hati fungani ya Sukuk yatajwa

Dar es Salaam. Wakati hatifungani ya Zanzibar Sukuk  ikiingizwa kwenye soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), inaelezwa Kisiwa hicho kiko mbioni kuanzisha Soko la Hisa Zanzibar.

Mkakati wa kuanzisha Soko la Hisa Zanzibar umeelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Fedha na Mipango, Saada Mkuya leo Mei 21, 2025 wakati wa hafla ya kuingiza hatifungani ya Zanzibar Sukuk kwenye soko la Hisa Dar es Salaam.

Mkuya amesema Zanzibar imeona itumie hatua hiyo ambayo ipo kisheria  kutokana na mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi, kijamii na kifedha.

“Soko la Hisa Zanzibar halitakuwa na lengo la kushindana na DSE kwani mawakala wa hisa ni wale, tutashirikiana na wenzetu wa DSE katika kutoa elimu ya jinsi gani watu watawekeza,” amesema.

Akielezea mchakato wa mkakati huo, Mkuya amesema tayari umeanza na sasa wako katika maandalizi ya miundombinu ya eneo na mifumo.

“Tunatarajia kwa mwaka wa fedha 2025/26 soko la Hisa la Zanzibar lianze kufanya kazi,” amesema na kuongeza.

“Tunaona ufanisi na mafanikio kwenye soko la hisa Dar es Salaam, na mafanikio ya Zanzibar Sukuk yanaonyesha ipo haja ya Zanzibar kuwa na soko la hisa,” amesema.

Kuhusu Zanzibar Sukuk

Akiielezea hatifungani ya Zanzibar Sukuk, Mkuya amesema ni uwekezaji unaotoa faida ya asilimia 10.5 kwa Shilingi ya Tanzania.

“Ni uwekezaji wa uhakika ambao muda ukifika muamala unapatikana katika akaunti yako,” amesema.

Ofisa mtendaji mkuu wa DSE, Peter Nalitolela amesema Zanzibar Sukuk ni dhamana iliyotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kupitia kampuni ya Zanzibar Treasury Sukuk1 Limited.

Amesema dhamana ya Sukuk ya Zanzibar ni tofauti na hatifungani ambazo zina riba.

“Hii kutokana na mafundisho dini ya Kiislamu haitakiwi riba, ila mkipata faida kwenye biashara mnagawana,” amesema.

“Leo hatifungani ya Zanzibar Sukuk imeorodheshwa kwenye soko la Hisa DSE ili kuwapatia fursa wawekezaji wengine kuwekeza,” amesema na kueleza mkakati uliopo kuwa ni  kuzalisha zaidi Sh1 trilioni.

“Katika mkupuo wa kwanza lengo lilikuwa kuzalisha Sh300 bilioni, kiasi kilichopatikana ni Sh381 bilioni na kuvuka lengo,” amesema akibainisha hatifungani hiyo ni ya miaka saba.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Yusra Sukuk ambaye pia ni mshauri elekezi wa Zanzibar Sukuk, sheikh Issa Mohammed  amesema itatoa fursa mbalimbali ikiwamo kuvutia wawekezaji kutoka nje, kuitangaza SMZ na Tanzania katika soko la Sukuk duniani na kutoa ajira kwa wananchi.

“Pia itaiwezesha Serikali kuhudumia miradi ya maendeleo,” amesema Sheikh Issa akitaja miongoni mwa miradi hiyo kuwa ni barabara, masoko na miradi mingine ya kijamii.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Zanzibar Treasury Sukuk1 Limited, Juma Amour Juma amesema kuingizwa kwa Zanzibar Sukuk kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam kutaimarisha uwazi na uaminifu wa soko.

“Kuna fursa nyingi ikiwamo ya ushirikishwaji wananchi katika maendeleo ya Taifa kwa njia ya uwekezaji,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *