Zanzibar kuwakutanisha wataalamu wa AI Afrika

Unguja. Kwa mara ya kwanza, Zanzibar inatarajia kuwakutanisha wataalamu wa teknolojia na akili mnemba (AI) 1,500 kutoka nchi mbalimbali za Afrika kubadilishana uwezo na kuongeza ujuzi katika kukuza biashara.

Katika mkutano huo wa Tech and AI Internationa Expo 2025, utawaleta pamoja viongozi wa tasnia, wawekezaji, watunga sera na washiriki wa teknolojia kuchunguza maendeleo ya hivi karibuni, kushirikiana na kuendesha ukuaji wa uchumi.

Pamoja na washiriki hao, pia kutakuwapo na maonyesho makubwa zaidi ya 80 kuhusu tasnia hiyo Agosti 22 hadi 23, 2025.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Machi 4, 2025, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga amesema licha ya jitihada zinazofanywa na taasisi za Serikali, hakujawahi kuwapo na jukwaa linalowaleta pamoja wadau wa Tehama kutoka nchi mbalimbali kujadiliana, kuweka mikakati na namna inayoweza kulea biashara zinazokua (startups).

“Kwa hiyo, jukwaa hili kwa umuhimu wake utakuwa ni mwanzo wa kuleta mageuzi makubwa ya Tehama katika visiwa vya Zanzibar na inaendana na vipaumbele vya Serikali vya kuiweka Zanzibar katika ramani ya dunia hususan kwenye ukuaji,” amesema Soraga.

Amesema licha ya sera ya uchumi wa buluu kuwa na maeneo matano lakini eneo la Tehama bado halijashughulikiwa vya kutosha.

“Katika asili ya uchumi wa kisiwa ni huduma na huduma katika dunia ya sasa zinarahisishwa na masuala ya Tehama, kwa hiyo ni mambo yanaendana moja kwa moja huwezi kuwa na huduma usiwe na teknolojia kurahisisha utoaji wake,” amesema.

Amesema jambo hilo ni muhimu kwani kuna vijana wengi ambao wamemaliza masomo ya Tehama lakini wanakosa nafasi ya kuendeleza mawazo yao.

Amesema kwa Zanzibar mazingira yote kwa ujumla bado yanaonekana hayajawa rafiki kwa mawazo yanayokuwa licha ya vipaji vingi vilivyopo.

Kutokana na hilo, amewataka vijana kujitokeza kwani hilo litakuwa jukwaa muhimu kwa ajili ya kubadilishana mbinu na mikakati, kuona jinsi Zanzibar inainuka kwenye nyanja ya Tehama ili ishindane na wengine.

Hata hivyo, amesema bado inahitajika sheria na sera kulinda biashara zinazochipukia.

“Lazima kuwe na sheria sera na miongozo, kwa hiyo kuwa na kikao kama hiki ni mwanzo mzuri tunabadilishana mawazo lakini baada ya hapo Serikali itakuwa na kazi kubwa ya kurasimisha haya mambo ili mifumo yetu iweze kusimama na kutambulika kimataifa,” amesema.

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Rais Ufuatiliaji na Utendaji Serikalini (ZPDB), Profesa Mohammed Hafidh amesema Zanzibar inaonekana kuwa na vipaji vingi katika maeneo hayo, lakini bado havijatendewa haki ya kuvitambua na kuviendeleza kwa hiyo umefika wakati sasa kufanya hivyo.

“Tukijenga mazingira mazuri na kuwapatia vifaa kuna maajabu makubwa yanaweza kufanywa na vijana, umefika wakati sasa kumtambua hata mtoto wakati akicheza ni vitu gani anapendelea kutambua vipaji hivyo na kuviendeleza,” amesema.

Mkurugenzi wa Zanzibar Startups Association, Ikram Soraga Amesema, “tutake tusitake haya mabadiliko ya teknolojia yapo kwa hiyo lazima tukubaliane kwenda nayo hatuwezi kusubiri.”

Meneja Utalii PDB, Hafsa Mbamba amesema matukio kama hayo ndio yatafungua utalii wa kisiwa hicho kwani awali hakukuwa na majukwaa kama hayo, “Zanzibar inabidi tukaze buti AI ndio itatusaidia kuboresha mazingira yetu katika utalii.’

Mtendaji Mkuu wa Africa Business Inc, Stephene Chikozho amesema kisiwa hicho kinachojulikana kwa fukwe zake za kupendeza na tasnia ya utalii, ipo haja ya kuongeza bidii kubadili uchumi wake kidijitali.

Amesema Expo itatoa jukwaa Zanzibar kuonyesha utayari wake wa kuwa kitovu cha teknolojia na uvumbuzi ukanda wa Afrika.

Katika muongo mmoja uliopita, Afrika imeshuhudia kuongezeka maendeleo ya miundombinu ya kidijitali na kupitishwa kwa AI katika anuwai ya viwanda.

Mtendaji Mkuu wa Unique Touch, Edwin George amesema wapo tayari kuelea katika teknolojia ya kisasa hivyo kuwakaribisha wadau wote katika sekta hiyo, kushirikiana kwa pamoja katika kukuza vipaji na kuviendeleza.

Mkutano huo utakaofanyika Agosti 22 hadi 23, umeandaliwa na Taasisi ya Afrika Business Inc ya Afrika Kusini na Parem Solutions kutoka UK kupitia Taasisi ya Unique Touch ya Zanzibar.