‘Zanzibar iongeze vivutio vya utalii’

Unguja. Wakati wageni 84,069 wakiingia Zanzibar Januari mwaka huu,  wataalamu wa uchumi na takwimu, wameshauri kuongeza vivutio ili kuepusha watalii kuishia hotelini.

Pia, wamesema umefika wakati wa kuongeza nguvu ya kutangaza vivutio hivyo katika mabara ya China na Afrika ili kupata wageni wengi.

Meneja wa Uchumi na Takwimu kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tawi la Zanzibar, Shamy Chamicha

Mtaalamu wa Uchumi na Takwimu kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tawi la Zanzibar, Shamy Chamicha amesema hayo leo Jumapili Februari 16, 2025 katika taarifa za wageni waliongia Zanzibar na kuongeza kuwa, kuongezeka kwa wageni kuendane na ubunifu wa vivutio vingi ili fedha wanazokuja nazo wazitumie nchini.

“Wageni wanapokuja nchini kunatakiwa kuwapo na vivutio vingi ili watoke wakavitembelee na kuongeza mzunguko wa uchumi lakini wakija wakakaa tu kwenye hoteli, zile fedha wanazokuja nazo watarudi nazo,” amesema.

Mchumi Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza) Estela Ngoma Hassan amesema bado wadau wa utalii wanakazi ya kutangaza sekta hiyo katika mabara ya Afrika, China na mengine ili wageni wazidi kuongezeka Zanzibar.

Ofisa kutoka Kamisheni ya Utalii, Hassan Amer Vuai amesema kamisheni imejipanga kutangaza sekta ya utalii katika mabara hayo na India ili kuhakikisha wageni wanakuja kutembelea Zanzibar.

Mtakwimu kutoka Kitengo cha Utalii, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Fatma Hilali Mohammed amesema inaonyesha kuna upungufu wa asilimia 8.2 ikilinganishwa na wageni 91,611 walioingia Desemba 2024.

Kati ya wageni hao, 62,125 sawa na asilimia 73.9 walitoka Bara la Ulaya huku  Afrika ikiwa ya pili kwa kuingiza wageni 10,390 sawa na asilimia 12.4 ya wageni wote wa Januari 2025.

“Bara la Amerika lilikuwa la tatu kwa kuingiza wageni 5,546 sawa na asilimia 6.6 kwa Januari 2025 na Bara la Oceania lilikuwa la mwisho kwa kuingiza wageni 840 sawa na asilimia 1.0 ya wageni wote kwa Januari 2025,” amesema Fatma.

Amesema Italia ilileta wageni 11,725 sawa na asilimia 13.9 ya wageni wote ikifuatiwa na Polish iliyoleta wageni 8,150 sawa na asilimia 9.7 huku Ufaransa ikileta wageni 7,983 sawa na asilimia 9.5.

Ujerumani ilifuatia kuingiza wageni 5,401 sawa na asilimia 6.4 ikifuatia Amerika kwa kuingiza wageni 3,749 sawa na asilimia 4.5.

Kati ya wageni hao wote walioingia Zanzibar, ni  75,767 sawa na asilimia 90.1 wakipitia viwanja vya ndege na wageni 8,302 sawa na asilimia 9.9 waliingia kupitia bandarini.

Kwa mujibu wa mtwakwimu huyo, wageni 40,229 sawa na asilimia 47.9 walikuwa wakiume na 43,840 sawa asilimia 52.1 wanawake.

Fatma amesema kuwa, asilimia 99.5 ya wageni walikuja Zanzibar kwa ajili ya mapumziko, asilimia 0.4 walitembelea ndugu na marafiki, huku asilimia 0.1 ya wageni hao walikuja Zanzibar kwa ajili ya sababu nyingine kama biashara na mikutano.

Ofisa Uhusiano, Idara ya Uhamiaji, Mrakibu wa Uhamiaji, Shariff Bakar Shariff amesema wageni wengi wanaoingia Zanzibar hivi sasa wamekuwa wakifuata masharti tofauti na miaka mengine iliyopita.

Meneja wa Tehama kutoka Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC), Bakar Mussa Yussuf amesema wageni hao wamekuwa na utayari kuchangia bima ya msafiri kwa kuwa, imekuwa ikiwafaa wanapopata matatizo wakiwa nchini.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ilianzisha bima ya msafiri; kila mtalii anatakiwa kulipa Dola 44 za Marekani ambayo humsaidia anapougua akiwa nchini. Bima hiyo imeanza kutumika Oktoba mosi 2024.