
Unguja. Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar imekiri kukabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji mtazamo wa sekta mtambuka ikiwemo mazingira, uchumi, teknolojia na utawala wa kimataifa.
Hayo yamebainishwa leo Februari 18, 2025 na Waziri wa wizara hiyo, Shaaban Ali Othman katika mkutano wa 18 wa Baraza la Wawakilishi wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Kwerekwe, Ameir Abdalla Ameir lililotaka kufahamu mkakati wa Serikali juu ya fursa za uchumi wa buluu zilizopo nchini.
Akijibu swali hilo, Shaaban amesema ili kuzitatua changamoto hizo, ushirikiano wa sekta mbalimbali, mikakati madhubuti na teknolojia bunifu zinahitajika.
“Ni ukweli usiopingika kwamba sekta ya uchumi wa buluu inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinahitaji mtazamo wa sekta mtambuka ili kuzitatua changamoto hizo, ushirikiano wa sekta mbalimbali, mikakati madhubuti na teknolojia zinahitajika,” amesema Shaaban.
Waziri Shaaban amesema sekta ya uchumi wa buluu inahitaji uwekezaji mkubwa katika bandari, viwanda vya samaki, nishati mbadala na utafiti wa baharini.
Hivyo, wizara hiyo itaendelea kuhamasisha uwekezaji binafsi kupitia sera za kifedha zinazovutia wawekezaji ikiwemo mikopo nafuu na motisha za kodi na kuendeleza ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) katika kuendeleza miundombinu bandari, viwanda vya kuchakata samaki na nishati ya baharini.
Pia, amesema wizara hiyo itaendelea kusimamia mfumo wa kisheria ulio imara kwa lengo la kulinda wawekezaji na kuondoa hatari ya kupoteza mitaji yao.