Zaka ya Fitr na hekima yake katika Uislamu

Maana ya Zaka ya Fitr

Neno Zaka katika muktadha wa lugha ya Kiarabu linamaanisha kukua kwa kitu, usafi wa kitu, na baraka. Na Fitr ni neno linalotokana na “iftr” (ufunguaji wa aliyefunga).

 Hivyo, Zaka ya Fitr inamaanisha kutoa sadaka kwa ajili ya mwili wa mfungaji na nafsi yake. Katika Uislamu, ni zaka inayotolewa kuwapa maskini na wahitaji wakati wa kuhitimisha mfungo wa Ramadhani, kama njia ya kumsafisha mfungaji kutokana na maneno machafu na porojo.

Wajibu wa Zaka ya Fitr

Kwa mujibu wa Qur’ani, Allah Mtukufu anasema: “Hakika amekwisha fanikiwa aliyejitakasa” (87:14). Na katika Sunna (Hadithi): “Mtume (rehema na amani ziwe juu yake) aliifanya Zaka ya Fitr kuwa faradhi kwa kila nafsi ya Muislamu…”

Masharti ya Zaka ya Fitr

1. Uislamu. Zaka ya Fitr ni wajibu kwa kila Muislamu, bila kujali kama ni mwanamume au mwanamke, mdogo au mkubwa.

 2. Uwezo. Zaka ya Fitr inapasa kutolewa na Muislamu anayemiliki kiasi cha chakula kinachozidi kile kinachohitajika katika matumizi yake, kwa ajili ya yeye mwenyewe, familia yake (wategemezi wake), na mahitaji yake ya msingi, wakati wa Sikukuu ya Id al-Fitr. Na ziada hiyo iwe inafikia pishi moja, (sawa na wastani wa kilo 2.5).

3. Muda wa wajibu. Zaka ya Fitr inapasa kutolewa baada ya jua kuzama, katika usiku wa Idd el-Fitr (kwa maana kuanzia jua kuzama siku ya mwisho ya Ramadhani).

Hekima ya Zaka ya Fitr

1. Kumtakasa mfungaji kutokana na maneno machafu na ya kipuuzi yaliyojitokeza wakati wa funga yake.

 2. Kulisha maskini, na inawasaidia kuacha kuombaomba katika siku ya Idd ef Fitr. Hii pia inahakikisha kuwa Idi ni siku ya furaha na sherehe kwa jamii nzima, maskini na matajiri.

 3. Kujenga umoja wa Waislamu wote, matajiri na maskini kwa kufarijiana, ili wote waweze kutekeleza ibada kwa furaha.

 4. Zaka kwa mwili, kwani Allah ametupatia uhai mwaka mzima, hivyo tunakuwa na jukumu la kutoa Zaka ya Fitr kama ishara ya kumshukuru kwa zawadi ya uhai na kuweza kuumaliza mfungo wa Ramadhani.

Wakati wa kutolewa Zaka ya Fitr

Wakati wake ni kuanzia jua linapozama siku ya mwisho wa Ramadhani hadi nyuma kidogo ya (kabla) ya sala ya Idd kuswaliwa. Kadhalika, inaweza kutolewa kabla ya Idd kwa siku moja au mbili hata tatu, lakini si wakati bora. Na haifai kutolewa baada ya sala ya Idd. Na iwapo itatolewa baada ya sala inakuwa sadaka ya kawaida.

Kiasi cha Zaka ya Fitr

Zaka ya Fitr ni pishi ya chakula kinacholiwa na watu katika nchi (mji) husika (hapa kwetu mchele). Ufafanuzi kutoka kwa Kamati ya Kudumu ya Utafiti wa Mambo ya Kislamu na Fat’wa inasema: Kiasi cha lazima kwa Zaka ya Fitr ni pishi moja kulingana na pishi ya zama za Mtume, na kiwango chake kwa kilogramu ni takriban kilo tatu. Japokuwa kwa kwetu (Tanzania) tunatoa wastani wa kilo 2.5.

Watu wanaopaswa kupokea Zaka ya Fitr

Suala hili lina mitazamo miwili kwa wanazuoni: Mosi, Zaka ya Fitr inapasa kutolewa kwa aina zote nane za watu wanaostahiki kupokea Zaka ya Mali waliotajwa katika Qur’an sura 9:60 hadi wenye madeni na waliosilimu karibuni.

Pili, Zaka ya Fitr inapasa kutolewa kwa maskini na mafukara tu. Kiupande wangu huu ndio mtazamo sahihi. Inaruhusiwa kumpa maskini au fukara mmoja tu au wengi.

Hukumu ya kutoa thamani (Pesa) badala ya chakula

Suala hili lina mitazamo miwili kwa wanazuoni: Mosi, mtazamo wa jopo la wanazuoni wa Sharia ya Kiislamu (Jumhr Al-Fuqah) yakiwemo madhehebu yetu ya Shafi: “Haitoshi kutoa thamani (pesa) badala ya chakula.” Hoja yao: Msingi wa ibada yoyote ni kufuata maelekezo yaliyothibitishwa na Mtume katika utoaji wa vitu na sio fedha. Pili, mtazamo wa Imamu Abu Hanifa na baadhi ya Masahaba: “Yafaa kutoa thamani (pesa) badala ya chakula.” Kiupande wangu huu ndio mtazamo sahihi unakidhi shida za maskini na mafukara, kwa kuwa fedha matumizi yake ni mapana zaidi kuliko chakula.

Wategemezi wanaowajibika kuwatolea Zaka

Wanazuoni wamekubaliana kuwa Zaka ya Fitr inamlazimu mtu mwenye uwezo wa ziada ya matumizi ya siku ya Idd, kujitolea yeye mwenyewe, wategemezi wake, kama vile watoto wake wadogo ambao hawana mali, mkewe, na wategemezi wake wengine wasiokuwa na uwezo.

Mahali Pa Kutolea Zaka ya Fitr

Sunna ni kuigawa Zaka ya Fitr kwa maskini wa eneo la mtu anayetoa zaka, lakini si vibaya kuihamisha kwa mujibu wa maoni ya wanazuoni wengi.

Hata hivyo, kuitoa katika mahali unapoishi ni bora na salama zaidi. Ikiwa utaituma zaka kwa familia yako ili waitoe kwa maskini wa eneo lako (ulilozaliwa), hakuna tatizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *