Dar es Salaam. Aliyekuwa mke wa Haji Manara, Zaiylissa amefunguka kwa mara ya kwanza huku akiweka wazi kuwa kwa sasa hayupo kwenye ndoa na ameamua kupumzika kwanza.
Zaiylissa ameyasema hayo leo Aprili 12, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari huku akiweka wazi zaidi kuhusiana na Manara kutohusika kabisa kwenye mikataba yake.

“Sipo kwenye ndoa kwa sasa na napumzika kwanza. Kuhusu mkataba wa kwanza, press ya kwanza tulikuwa na aliyekuwa mume wangu nilitafutwa kabla mimi sijakutana na aliyekuwa mume wangu kwa hiyo nilitafutwa na tukakubaliana kufanya kazi.
“Bahati nzuri likatokea la kutokea mambo yakaunganika tukaendelea na kazi humo humo moja kwa moja na kuhusu yeye alikuwa hanisainii kwenye mikataba yangu, alikuwa ananisaidia na kunisimamia kama mke wake, mikataba nasaini mwenyewe, alikuwa ananisapoti si kwamba alikuwa kwenye mikataba,” amesema Zaiylissa.

Aidha ameweka wazi kuhusiana na baadhi ya tetesi zinazoeleza kuwa anampango wa kurudi kwa mpenzi wake wa zamani, Dulla Makabila ambapo ameeleza kuwa hana mpango wa kurudi kwa yoyote.
“Hizo video ni za muda mrefu sana halafu sina mpango huo wa kurudi kwa yeyote, sasa hivi nimeamu kufocus na kazi, familia, yaani sasa hivi vitu mtakavyoviona kwangu mimi ni kazi basi,” amesema mwanadada huyo.
“Lakini niwaambie tu ndoa sio mbaya, na msikurupuke pia, kila kitu kinakuja kwa wakati sahihi na mtu sahihi anakuja wakati sahihi, yaani hivyo tu msikurupuke.”

Utakumbuka kuwa siku mbili zilizopita Haji Manara na Zaiylissa waliingia katika sintofahamu iliyopelekea kurushiana maneno katika mitandao ya kijamii wakionesha kuwa penzi lao limefika mwisho.
Wawili hao walifunga ndoa Januari 24, 2024 huku ikiwa ni ndoa ya sita kwa Manara na ya pili kwa Zaiylissa.
Endelea kufuatilia Mwananchi.