Yemen yatoa taarifa kuhusu mashambulizi iliyofanya dhidi ya ngome za utawala wa Kizayuni

Jeshi la Yemen limetoa taarifa kuhusu mashambulizi liliyofanya dhidi ya baadhi ya maeneo nyeti na muhimu sana ya kijeshi ya adui Mzayuni katika maeneo ya Jaffa na Ashkelon huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu iliyopachikwa jina bandia la Israel.

Akisoma taarifa hiyo mapema leo, Msemaji wa jeshi la Yemen Brigedia Jenerali Yahya Saree, amesisitiza kama ninavyomnukuu: “katika kutetea mataifa mawili yanayodhulumiwa ya Lebanon na Palestina na vile vile  katika kuunga mkono wanamuqawama wa Palestina na Lebanon, na katika utekelezaji wa awamu ya tano ya kushadidisha mashambulizi, kikosi cha ndege zisizo na rubani cha jeshi la Yemen kimefanya oparesheni za kijeshi dhidi ya vituo nyeti kadhaa vya kijeshi vya adui Israel vilivyoko kwenye maeneo ya Jaffa na Ashkelon kusini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Saree amefafanua na kusema kuwa: katika kujibu jinai za adui Mzayuni huko Gaza na Lebanon, vikosi vya ulinzi vya Yemen vitaendelea mfululizo wa oparesheni zake za kijeshi, na mfululizo huo wa oparesheni hautasitishwa mpaka yatakaposimamishwa mashambulizi dhidi ya Ukanda wa Gaza na kuondolewa mzingiro uliowekewa pamoja kukomeshwa mashambulizi dhidi ya Lebanon.

Kufuatia hujuma za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na Lebanon, kambi za usaidizi za Mhimili wa Muqawama, ikiwemo ya Yemen na Hizbullah ya Lebanon daima zimekuwa zikilenga vituo vya kijeshi vya  utawala wa Kizayuni kwa mashambulizi makali  ya makombora na ndege zisizo na rubani.