Yemen yashambulia meli tatu zilizokiuka marufuku ya kuelekea bandari za utawala wa Kizayuni

Vikosi vya Ulinzi vya Yemen vimetangaza kuwa vimezishambulia meli tatu kwa kukiuka marufuku iliyowekwa na nchi hiyo ya kupita kwenye eneo la maji yake kuelekea bandari za utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.

Msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen Brigedia Jenerali Yahya Saree alitoa tangazo hilo jana katika taarifa kupitia televisheni.

Saree amesema: “meli ya SC Montreal ililengwa na ndege mbili zisizo na rubani kusini mwa Bahari ya Arabia” na akaongeza kuwa, meli nyingine iliyotambuliwa kama Maersk Kowloon, ililengwa katika Bahari ya Arabia kwa kombora la kruzi.

Kwa mujibu wa msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen, meli nyingine ya Motaro ililengwa katika Bahari Nyekundu na Bab al-Mandab kwa makombora kadhaa ya balestiki.

Brigedia Jenerali Yahya Saree

Wakati huohuo, Shirika la Uingereza la Operesheni za Biashara ya Baharini (UKMTO), limeripoti kuwa kuna meli ambayo imeshambuliwa umbali wa maili 25 kusini mwa mji wa bandari wa al-Mukha katika Bahari Nyekundu kusini magharibi mwa Yemen.

Tangu Oktoba mwaka jana, vikosi vya ulinzi vya Yemen vimekuwa vikiendesha mamia ya operesheni za mashambulizi dhidi ya meli zinazosafiri kuelekea au zinazotoka bandari za ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel, na kuzipiga makombora na ndege zisizo na rubani meli kadhaa kati ya hizo.

Operesheni hizo zilianza baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuanzisha vita vya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza, kushadidisha mzingiro wake dhidi ya eneo hilo na kuzidisha mashambulizi ya kikatili dhidi ya Lebanon.

Brigedia Jenerali Saree ameeleza bayana katika taarifa yake: “vikosi vya ulinzi vinaapa kuwa vitaendelea kuweka mzingiro wa majini dhidi ya adui na kufanya mashambulizi katika maeneo yote yanayohusiana na adui Israel katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu;” na akaongezea kwa kusema, vikosi hivyo vya majeshi ya Yemen “havitasimama hadi uvamizi utakapokomeshwa, mzingiro dhidi ya Ghaza utakapoondolewa, na mashambulio dhidi ya Lebanon yatakaposimamishwa”…/