Vikosi vya jeshi la Yemen vimesema kuwa vimefanikiwa kuipiga kambi ya kijeshi ya Israel kwa kombora la hypersonic.
Harakati ya Ansarullah ya Yemen jana Jumanne ilitoa taarifa na kueleza kuwa, kombora hilo limepiga kambi ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel mashariki mwa eneo linalokaliwa kwa mabavu la Yafo.
Msemaji wa jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree, amesema kuwa kombora hilo la balestiki la hypersonic limeipiga shabaha iliyokusudiwa kwa mafanikio na kuvuka mifumo ya ulinzi wa anga ya Marekani na Israel.

Amesema, vikosi vya jeshi la ulinzi vya Yemen vimetekeleza oparesheni hiyo katika kuonyesha mshikamano na kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina na Lebanon na katika kuunga mkono mapambano yao.
Msemaji wa jeshi la Yemen amesema vikosi vya ulinzi vya Yemen vitaendelea kufanya oparesheni za kijeshi dhidi ya utawala wa Israel hadi uvamizi utakapokomeshwa, mzingiro wa Gaza kuondolewa na mashambulizi dhidi ya Lebanon yatakapostishwa.