
Sheria na mikataba mbalimbali inayozungumzia huduma na haki za mtoto, inamtambulisha mtoto kama mtu yeyote mwenye umri wa miaka chini ya 18.
Je, kuna sababu inayomfanya mtu wa umri huu kuwa mtoto? Kwenye hili, ipo mitazamo mbalimbali. Kwa mfano, tukizingatia kigezo cha hali ya ukuaji wa kimwili, tunaweza kusema sifa kuu ya utoto ni kuendelea kupevuka viungo vya mwili. Tatizo la mtazamo kama huu ni ukweli kuwa mtoto wa miaka 13 anaweza kuwa keshabalehe na amepevuka kimwili. Unamwitaje mtoto?
Hapa ndipo penye umuhimu wa kuelewa athari za historia, tamaduni na mienendo ya jamii. Uelewa wa nini kinamfanya mtu ahesabike kuwa mtoto na wakati gani watoto hukoma kuitwa watoto na kuingia kwenye utu uzima, unatofautiana katika jamii zetu.
Katika jamii nyingi za Kiafrika kwa mfano, matukio fulani yanaweza kuchukuliwa kuwa mpaka wa utoto na utu uzima. Kuna mila kama jando na unyago zinazotazamwa kama kivuko cha utoto kwenda utu uzima. Pia zipo imani/mila za kidini zenye matukio ya namna hiyo kama kipaimara, sakramenti ya kwanza na kadhalika.
Haya yote ni matukio yenye ‘uwezo’ wa kumvusha mtoto kwenda utu uzima bila kueleza ni mambo gani hasa yanamfanya mtu aonekane ni mtoto au mtu mzima.
Kwa upande mwingine, wapo wanaomwangalia mtoto kwa jicho la mahitaji yake ya kimsingi. Mashirika na taasisi zinazojishughulisha na ustawi wa watoto kisera na kisheria hutumia mahitaji kama kigezo cha kuamua nani ni mtoto na nani siye.
Kwa mfano, watetezi wa haki za watoto huweza kumchukulia mtoto kama mtu yeyote mwenye umri fulani asiye na uwezo binafsi wa kujitetea na hivyo kuhitaji kulindwa na unyanyasaji au ukiukwaji wa haki zake fulani fulani.
Ukisoma biblia, kuna mahali Mtume Paulo anawaonya waumini wa Korintho kuacha mambo ya kitoto. “Ndugu zangu, msiwe watoto katika akili zenu; lakini katika uovu mgeuzwe watoto wachanga, bali katika akili zenu mkawe watu wazima. Ndio usiwe mtoto katika akili zako lakini katika uovu mgeuzwe watoto wachanga Bali katika akili zenu mkawe watu wazima.” Mwisho wa kunukuu.
Utoto, kwa mukhtadha huu, ni ile hali ya kutokuelewa mambo, ufinyu wa fikra na mawazo unaokufanya usiaminike kwa mambo makubwa. Utoto ni hali mbaya tunayotakiwa kupambana nayo.
Lakini ukimsikiliza Yesu Kristo kwenye mafundisho yake kuna mahali anauelezea utoto kama sifa ya kuurithi ufalme wa Mungu. “Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, yeyote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni.” Mwisho wa kunukuu.
Hapa tunaona anazungumzia kuongoka. Kwa kawaida watoto wana uwezo mzuri wa kujutia makosa yao, kuomba msamaha na kuanza upya.
Hawana kiburi cha kung’ang’ania kuwa sahihi. Kingine kinachojitokeza hapo ni kujinyenyekeza, uwezo wa kujishusha na kuheshimu mamlaka ya mzazi.
Ukitazama vizuri hata furaha ya watoto inategemea sana uwezo wao wa kuwaamini wazazi wao.
Mtoto mzuri ana matumaini, anajua kesho itakuwa bora, kwa sababu ana imani na mzazi wake. Unaweza kuona tafsiri ya utoto hapa si tabia mbaya. Utoto unabeba tabia zenye utu wema.
Kama kuna kitu cha thamani tunakipoteza kadri tunavyokuwa na kukutana na watu tunaowaheshimu ni kulazimika kuufukia ule ‘utoto’ ndani yetu unaoturuhusu kuwa na matumaini, kuamini kesho itakuwa bora, kujieleza bila hofu ya kuvaa sura ya ‘nitaonekanaje’, kujisikia huru kufunua hisia zetu, matamanio yetu, bila aibu, fedheha wala hatia ya kukataliwa na kukosolewa na watu tunaowahitaji.
Ukiwachunguza marafiki wa karibu, wapenzi na wanandoa wanaoaminiana na kufurahiana, kuna namna unaona mazingira hayo ya uhuru wa mtu kujifunua kwa uwazi bila hofu ya kulazimika kuonekana na sura fulani.
Hawa, kwa mujibu wa ushunuzi chanya, ndio watu wanaokuwa na furaha zaidi, wasiosumbuliwa na magonjwa mengi yasiyoambukizwa na ndio wanaoishi maisha marefu na utoshelevu.
Sote tunahitaji mtu tunayeweza kumwamini, atakayefufua ule utoto uliofichika ndani yetu, atakayetupunguzia shinikizo la maisha linalotuzuia kuifurahia leo, atakayechoza kicheko chetu, atayetufanya tujisikie huru kuusemea moyo bila aibu wala hofu ya kufedheheka na kutupunguzia kazi ya kuvaa sura ya ‘unapaswa’, ‘unatakiwa’, ‘unatarajiwa’, ‘unalazimika’,‘unatazamiwa’, ‘unategemewa.’
Furaha sio chaguo bali mazingira yanayotuhakikishia kiasi fulani cha uhuru huu wa kihisia kama ilivyo kwa mtoto.