
WAKATI Yanga iikijiandaa kushuka uwanjani jioni ya leo kuvaana na Copco ya Mwanza katika mechi ya kiporo cha hatua ya 64 Bora ya Kombe la Shirikisho nchini, beki nyota wa timu hiyo, Yao Kouassi anayesumbuliwa na majeraha, amelia na mambo matatu yanayomuumiza kwa sasa.
Beki huyo amesema mambo hayo yamechangia kumfanya awe na msimu mbaya kwake tangu ajiunge na timu hiyo akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast ya Ivoery Coast.
Muivory Coast huyo aliyeanza kuichezea Yanga msimu uliopita, tangu atue katika kikosi hicho amekuwa na kiwango bora wakati wote akitumika kikosi cha kwanza kabla ya kuumia na kuwa nje na sasa amefanyiwa upasuaji utakaomweka nje ya wiki kati ya 4 hadi 6.
Yao amecheza kikosi cha kwanza chini ya makocha wawili, akianzia kwa aliyepita Miguel Gamondi na sasa Sead Ramovic, aliumiza nyama za paja na kufanyiwa upasuaji na kumfanya akose mechi kadhaa zikiwamo za Ligi Kuu na zile za Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ikitolewa makundi.
Licha ya Yanga kuishia hatua ya makundi na kushindwa kutinga robo fainali kwa msimu wa pili mfululizo katika Ligi ya Mabingwa, beki huyo alicheza mechi tatu za mwanzo kabla ya kuumia zikiwamo ilizopoteza dhidi ya Al Hilal ya Sudan na MC Alger ya Algeria na ile ya sare ya 1-1 ya TP Mazembe ya DR Congo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Yao alisema kwa sasa anaendelea vizuri, japo yapo mambo yanayoendelea yanayomuumiza kwa sasa.
Alisema anaona huu ni msimu wa hasara kwake kwani mapema tu alianza na majeraha yanayomfanya kuwa nje kwa muda mrefu na kuainisha mambo matatu yanayomuumiza.
“Jambo la kwanza ni kwamba nimekuwa na vipindi tofauti vya kuwa majeruhi na sasa nimefanyiwa upasuaji ingawa naendelea vizuri, lakini sifurahii kukosa mechi nyingi za timu yangu,” alisema Yao na kuongeza jambo la pili ni kupoteza nafasi ya kutetea rekodi ya asisti aliyokuwa nayo msimu uliopita akiwa beki aliyefanya hivyo mara nyingi akiasisti mara saba sawa na ilivyokuwa kwa Lusajo Mwaikenda wa Azam.
“Kingine kinachoniumiza ni Yanga kutolewa Ligi ya Mabingwa nikiwa nje, kwani nilikuwa na ndoto za kuipigania timu icheze robo fainali ya pili mfululizo,” alisema.
“Majeraha yaliniweka nje na kwa bahati mbaya timu imekusanya pointi chache zilizoizuia kwenda robo fainali na kuyeyusha ndoto ya kila mmoja,” alisema.
Yao alisema bado anaamini kwa kikosi kilichopo chini ya kocha Sead Ramovic, kuna nafasi ya kukata tiketi kwa msimu ujao wa michuano ya CAF baada ya kuteleza msimu huu.
Rekodi za Yao zinaonyesha msimu huu amecheza jumla ya mechi saba za Ligi Kuu Bara, akiwa hana asisti wala bao lolote akitumika kwa dakika 538.
Yao alisema anaomba apone haraka na kutumia muda uliosalia wa mechi za Ligi Kuu ili kutetea nafasi hiyo, japo anaona ni ngumu kwa idadi ya mechi zilizopo na ushindani uliopo pia.