
Dar es Salaam. Yanga Princess imeiweka Simba Queens katika uwezekano mgumu wa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu baada ya kuichapa bao 1-0 katika mechi baina yao leo kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yameifanya Simba Queens kubakia na pointi zake 34 baada ya kucheza mechi 13, ikiitangulia JKT Queens iliyo katika nafasi ya pili na ikiwa na mechi moj mkono kwa tofauti ya pointi mbili tu.
Bao la ushindi la Yanga Princess leo limefungwa na Jeannine Mukandayisenga katika dakika ya 49.
Mara ya mwisho Yanga kuifunga Simba bao 1-0 ilikuwa msimu wa 2021/22 bao la Clara Luvanga aliyetimkia Al Nassr ya Saudia.
Mzunguko wa kwanza zilipokutana timu hizo, Yanga ikiwa nyumbani ilikubali kichapo cha bao 1-0.
Huu unakuwa mchezo wa kwanza kwa Simba kupoteza msimu huu kwani kwenye mechi 13 imeshinda 11, sare moja na kupoteza mmoja.
Kwa Yanga unakuwa mchezo wa nane kushinda kwenye mechi 13 ikitoa sare tatu na kupoteza mbili.
Mabadiliko waliyofanya Yanga kipindi cha pili kumtoa Diana Mnally na kumuingiza Adebis Ameerat 48 yalionekana kuilipa Yanga kwenye eneo la kushambulia na dakika nne mbele akatoa pasi ya bao.
Matokeo hayo yanaifanya Simba iendelee kusalia na pointi 34, JKT nafasi ya pili na pointi 32 na Yanga yenye pointi 27.
Huu unakuwa mchezo wa 13 kwa timu hizo tangu zilipokutana mwaka 2019.
Kwenye michezo hiyo 13, Simba imeshinda tisa, sare mbili na kupoteza mmoja huku Yanga ikishinda mara mbili, sare mbili na kupoteza tisa.
Bato ya wachezaji
Pamoja na kushuhudia soka safi kutoka kwa wadada hao, lakini kulikuwa na vita ya wachezaji.
Vita ya Diana Mnally na Fatuma Issa ‘ Fetty Densa’ hawa wote ni mabeki wa kulia walikuwa na bato ya aina yao kila mmoja akipambana kuzuia mashambulizi kwa timu pinzani.
Bato hiyo ilichangiwa na kujuana kwani kabla ya Mnally kutimkia kwa wananchi aliwahi kuichezea Simba hivyo alimfahamu vyema mpinzani wake.
Bato nyingine ilikuwa kati ya Mghana Diana Antwi wa Yanga na winga Asha Djafar wa Simba.
Antwi ambaye anacheza mlinzi wa kushoto alifanikiwa kumdhibiti Djafar hasa anaposhambulia lango la wananchi.