Yanga yaweka ngumu dabi, yaishika pabaya Bodi ya Ligi

Dar es Salaam. Yanga imetoa msimamo wake baada ya kuahirishwa kwa Dabi ya Kariakoo ikisema haitakubali haitocheza tena na Simba kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara namba 184.

Taarifa ya Yanga iliyotoka usiku wa leo Machi 9, 2025 kufuatia kikao cha Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo iliyokutana kwa dharura imesema haitarudiana na watani wao hao kufuatia mchezo huo kuahirishwa jana Machi 8, 2025 na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB).

Kwenye taarifa hiyo Yanga imetoa maazimio matatu ya Kamati yao ya utendaji ikisema inataka kupewa ushindi kwa mujibu wa kanuni pindi timu moja inaposhindwa kutokea uwanjani.

Yanga pia imelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuvunja Kamati ya Usimamizi wa Ligi iliyo chini ya Mwenyekiti wake, Steven Mnguto (Mwenyekiti wa TPLB) na katibu wake, Almas Kasongo (Ofisa Mtendaji Mkuu TPLB) kwa kile ilichoeleza kukosa imani nayo huku ikitaka watu wenye nia njema na yenye waadilifu kwa maslahi ya mpira.

Hatua hiyo ya Yanga kuikataa Kamati hiyo imesema inatokana na Mnguto jana Machi 8, na kueleza wazi kwamba hakuna mabadiliko ya mechi hiyo kuahirishwa huku akitaka mashabiki kuendelea kukata tiketi na kwenda uwanjani.

Aidha, Yanga pia imeweka wazi kwamba Simba haikutoa taarifa kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo huo kilichofanyika Machi 7, 2025 kwenye Hoteli ya Spice jijini Dar es Salaam kwamba, ingetaka kutumia haki yake ya msingi ya kufanya mazoezi na badala yake ikaibuka Ijumaa usiku ikitaka kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara imewaomba radhi mashabiki wa Soka Tanzania kwa kukosa mchezo huo huku ikisema timu yao ilijiandaa kikamilifu kucheza mechi hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *