Yanga yatinga robo fainali FA, Ikangalombo akiwasha

Dar es Salaam. Ushindi wa nyumbani wa mabao 2-0 dhidi ya Songea United leo umeipeleka Yanga katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB mashindano ambayo timu hiyo ni bingwa wa kihistoria.

Walioihakikishia Yanga ushindi katika mchezo huo ni Duke Abuya aliyefunga bao la kuongoza katika dakika ya 22 na Jonathan Ikangalombo aliyepachika la pili katika dakika ya 54.

Baada ya kuanza kwa kutawala mchezo kwa muda mrefu huku ikitengeneza nafasi nyingi za mabao ambazo wachezaji wake hawakuzitumia vyema, Yanga ilitangulia kupata bao kupitia kwa Abuya ambaye alimalizia kwa shuti la wastani la mguu wa kulia, akiunganisha mpira uliookolewa na beki wa Songea United baada ya shuti la Maxi Nzengeli.

Bao hilo lilidumu hadi refa Isihaka Mwalile kutoka Dar es Salaam alipopuliza filimbi ya kuashiria muda mwa mapumziko.

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kuendelea kumiliki mchezo huku Songea United wakionekana kujilinda zaidi na kushambulia mara kadhaa kwa kushtukiza.

Juhudi za Yanga kusaka mabao mengine  zilizaa matunda katika dakika ya 54 ilipopata bao la pili kupitia kwa Ikangalombo ambaye alimaliza kwa shuti hafifu pasi ya Pacome Zouzou na mpira huo kujaa wavuni.

Hilo ni bao la pili kwa Ikangalombo kuifungia Yanga katika mechi mbili mfululizo za timu hiyo, la kwanza akifunga katika mechi ya kirafiki dhidi ya Singida Black Stars, Jumatatu wiki hii.

Ushindi huo umeifanya Yanga kuendeleza rekodi ya kuwa timu ambayo imeingia mara nyingi zaidi hatua ya robo fainali ya mashindano hayo tangu msimu wa 2015/2016 ambapo imetinga mara zote tisa yalipofanyika.

Baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa, kiungo wa Yanga, Pacome Zouzoua alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Katika mchezo mwingine uliochezwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, wenyeji Mashujaa FC wametupwa nje ya mashindano hayo baada ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Pamba Jiji.

Bao pekee la ushindi la Pamba Jiji katika mchezo huo lilipachikwa na Alain Mukeya katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza akimalizia pasi ya Deus Kaseke.

Ushindi wa Pamba Jiji unafanya kukamilika kwa idadi ya timu nane ambazo zimefuzu robo fainali ambapo saba nyingine ni Yanga, Simba, Stand United, Singida Black Stars, Kagera Sugar, Pamba Jiji na Mbeya City.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *