Yanga yatangulia fainali Samia Super Cup

YANGA Princess imetangulia fainali ya michuano ya Samia Women Super Cup 2025 baada ya kuitandika Fountain Gate Princess mabao 7-0.

Mchezo huo umepigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo jijini Arusha ambapo ulianza majira ya saa 8:00 mchana na kushuhudia dakika 45 za kipindi cha kwanza Yanga Princess ikitawala na kuongoza kwa mabao 3-0 yakifungwa na Protasia Mbunda dakika ya 21, Jeannine Mukandayisenga (dk 30) na Aregash Kalsa (dk 32).

Kipindi cha pili, Yanga Princess walirejea na moto ule ule kwa kushambulia lango la Fountain Gate Princess kama nyuki na kuwafanya wadada hao kutoka Babati mkoani Manyara kushindwa kushikilia bomba na kuruhusu mabao mengine manne.

Mabao hayo yamefungwa na Lydia Akoth dakika ya 54, Agness Pallangyo (dk 57), Neema Paul (dk 75) na Adebisi Ameerat (dk 81) na kuhitimisha ushindi wa mabao 7-0 ulioifanya Yanga Princess kutinga kibabe fainali ikimsubiri mshindi wa nusu fainali ya pili kati ya Simba Queens dhidi ya JKT Queens ambazo zitamenyana kuanzia majira ya saa 10:15 jioni.

Michuano ya Samia Women Super Cup 2025 inashirikisha timu nne za Ligi Kuu Soka Wanawake ambazo ni Simba Queens, JKT Queens, Yanga Princess na Fountain Gate Princess ambayo imeingia kama mwenyeji.

Mchezo wa fainali utapigwa Alhamisi baina ya Yanga Princess dhidi ya mshindi wa nusu fainali ya pili kati ya Simba Queens na JKT Queens.