Dar es Salaam. Yanga imepanga kutumia mafanikio yake ya uwanjani kupaisha utalii wa Zanzibar ambapo sasa haitoishia kuvaa jezi za kuitangaza Zanzibar tu bali kutoa elimu kuhusu vivutio tofauti vya utalii vilivyomo visiwani humo.
Hilo limetangazwa leo Machi 28, 2025 na rais wa Yanga, Hersi Said katika mkutano wa kutangaza kuendelezwa kwa ushirikiano baina ya klabu hiyo na wizara ya utalii na mambo ya kale na mambo ya kale Zanzibar.
“Young Africans SC tunaitazama wizara ya utalii na mambo ya kale kama jicho la Zanzibar, mahusiano tunayoingia leo ni kwa ajili ya kuutangaza utalii wa Zanzibar kupitia klabu yetu. Na mahusiano haya sio kutangaza tu bali kutoa elimu na uelewa juu ya vivutio vyote vya utalii Zanzibar,” amesema Hersi.

Waziri wa utalii na mambo ya kale Zanzibar, Mudrick Ramadhan Soraga
Kwa mujibu wa Hersi, ushirikiano huo baina ya Yanga na wizara ya utalii na mambo ya kale Zanzibar ambao ulianza msimu huu, utaendelea hadi mwishoni mwa msimu ujao.
“Tuna furaha kubwa kupata fursa hii ya kuingia mahusiano ya ushirikiano na kamisheni ya utalii chini ya wizara ya utalii na mambo ya kale kwa ajili ya kutangaza vivutio vya utalii hapa Zanzibar. Mahusiano haya yatadumu mpaka mwisho wa msimu wa 2025/26. Logo ya “Visit Zanzibar” itaendelea kubaki kwenye jezi yetu katika michuano yote tutakayoshiriki.
“Huna haja ya kwenda Ibiza au Dubai kufanya utalii wakati Zanzibar ipo. Kwa nini upeleke hela yako nje ya nchi wakati Zanzibar yetu imebarikiwa vivutio vingi vya utalii? Klabu yetu inakwenda kuweka nguvu kuongeza idadi kubwa ya watalii wa ndani na nje watakaokuja kuitembelea Zanzibar,” amesisitiza Hersi.

Waziri wa utalii na mambo ya kale Zanzibar, Mudrick Ramadhan Soraga amesema kuwa ushirikiano wao na Yanga utakuwa wenye manufaa makubwa kwa sekta ya utalii visiwani Zanzibar.
“Niwapongeze sana Viongozi wa Young Africans SC chini ya rais wake Injinia Hersi Said kwa ushirikiano mkubwa mlioutoa kutoka mwanzo mpaka leo tunapokwenda kusaini mahusiano haya ya ushirikiano wa kutangaza Utalii wa Zanzibar.
Sekta ya utalii ina ushindani mkubwa sana, licha ya jina kubwa tulilokuwa nalo bado tunapata ushindani sana kutoka katika visiwa vya jirani hivyo ni lazima kama wizara tuweke nguvu kubwa kwenye kujitangaza,” amesema Soraga.
Ikumbukwe msimu huu, Yanga ilikuwa ikivaa logo ya kutangaza utalii Zanzibar ya ‘Visit Zanzibar’ pindi ilipokuwa ikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.