
Dar es Salaam. Klabu ya Yanga imemtambulisha rasmi Mustapha Kodro kuwa kocha msaidizi akichukua nafasi ya Moussa N’Daw raia wa Senegal.
Kodro anaenda kuongeza nguvu katika benchi jipya chini ya kocha mkuu, Sead Ramovic wakiwa na jukumu la kuiongoza timu hiyo katika michezo ijayo kwa kuanza na hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika Novemba 26 mwaka huu.
Kondro ambaye alikuwa msaidizi wa Ramovic pale TS Galaxy, amezaliwa Agosti 29, 1981, huko Mostar nchini Bosnia-Herzegovina huku akiwa na leseni ya UEFA Pro.
Kabla ya kuwa kocha, Kodro katika kipindi chake cha kucheza soka alikuwa kiungo mkabaji, akizitumikia Zvijezda na FK Velez Mostar zote za Bosnia-Herzegovina.
Kazi ya ukocha alianzia FK Velez Mostar akiwa kocha msaidizi ambapo majukumu hayo aliyachukua kuanzia Agosti 5, 2019 hadi Juni 1, 2022. Juni 2, 2022 akatua FK Sarajevo kabla ya kuachana nayo Oktoba 19, 2022, ndipo Desemba 28, 2022 akatua TS Galaxy aliyoachana nayo hivi karibuni alipopata dili la Yanga.
Ikumbukwe kwamba, Ramovic alipokabidhiwa mikoba ya kuifundisha Yanga amewabakisha makocha wengine wote waliokuwa wasaidizi kwa Gamondi akiwemo kocha wa viungo Taibi Lagrouni, kocha wa makipa Alaa Meskini na mchambuzi wa mikanda ya video Mpho Maruping.