
Yanga yarudi kileleni, rekodi mpya yaandikwa
WAANDISHI WETU
YANGA imeendeleza rekodi katika Ligi Kuu Bara baada ya kuifumua KMC kwa mabao 6-1 kwenye Uwanja wa KMC Complex, uliopo Mwenge, jijini Dar es Salaam, huku Stephane Aziz Ki akifunga hat trick inayokuwa ya pili msimu huu, ikiwamo ya kwanza ya Prince Dube.
Matokeo hayo yameirejesha Yanga kileleni kwa kufikisha 49 na mabao 47 ikiing’oa Simba kwa tofauti na pointi mbili na mabao manane, ikiwa imecheza mechi 19, moja zaidi na ilizonazo Mnyama, huku hicho kikiwa kipigo cha pili kikubwa kilichotolewa na timu hiyo baada ya ile ya KenGold.
Huo ulikuwa mchezo wa pili kwa Yanga ikiwa chini ya Kocha Miloud Hamdi aliyetua hivi karibuni kutoka Singida Black Stars, baada ya awali kutoka suluhu na JKT Tanzania na kasi ya timu hiyo ilionekana kuwa chini tofauti na ilivyocheza leo na ile Gusa Achia Twende Kwao ilionekana.
Dube aliitanguliza Yanga kwa bao la dakika ya 11 akimalizia pasi ya Maxi Nzengeli, likiwa bao la nane kwa nyota huyo raia wa Zimbabwe, kabla ya Aziz kufunga kwa penalti baada ya Dube kuangushwa dakika ya 18, mabao yaliyodumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili kilipoanza tu, Aziz alifunga bao la tatu dakika ya 49 kwa shuti kali kabla ya KMC kumtibulia kipa Diarra Djigui baada ya Remdatus Mussa kufumua shuti kali la pembeni lililomshinda ngumu kipa huyo na kutinga wavuni dakika ya 52.
Dakika tano baadae Yanga ilipata penalti nyingine baada ya Dube kuangushwa na Aziz Ki kufunga mkwaju huo likiwa bao la nne la mchezo la tano kwake msimu huu, lakini ikiwa penalti ya sita kupiga msimu huu akiwa kinara, licha ya kukwamisha nne kama alizonazo Leonel Ateba wa Simba.
Maxi Nzengeli alifunga bao la tano dakika ya 90 kabla ya beki Israel Mwenda akifunga hesabu dakika ya 90+5 akimaliza pasi ya Dube na kuiacha KMC iliyocheza hivyo leo tofauti na ilipoumana na Singiga BS na kushinda 2-0 ikiondoka uwanjani kinyonge. Maxi lilikuwa ni bao lake la nne msimu huu, wakati Mwenda ni la kwanza tangu ajiunge na timu huyo kutoka Singida BS.
IKANGALOMBO BADO
Winga wa Yanga Jonathan Ikangalombo bado amekosekana kuonekana uwanjani tangu asajiliwe akiwa jukwaani juu huku wenzake wakiendelea kuipigania timu hiyo.
GUSA ACHIA IMERUDI
Licha ya kwanza KMC ilicheza kinyonge, lakini kasi ya Yanga katika falsafa ya Gusa Achia ilionekana kurudi katika mchezo huo na hasa kipindi cha pili baada ya kocha Hamdi kufanya mabadiliko ya wachezaji yaliyoivuruga ngome ya wenyeji wa mchezo huo.
KAGERA YAZINDUKA
Katika mchezo mwingine uliochezwa jioni kati ya wenyeji Kagera Sugar iliyozinduka kwa kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate, huku straika Mganda, Peter Lwasa akifunga mara mbili kwa mikwaju ya penalti, licha ya matokeo hayo kuiacha Kagera nafasi ya 15 ikiwa na pointi 15.
Bao la tatu la Kagera katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Kaiatba, mjini Bukoba lilifungwa dakika za lala salama kupitia kwa Saleh Seif na kuipa timu hiyo ushindi wa tatu msimu huu.
PRISONS YALALA
Maafande wa Tanzania Prisons ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya ilikutana na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Namungo, bao likiwekwa kimiani na Ibrahim Joshua dakika ya tatu ya mchezo huo.
BWENZI ATUPIA TENA
Katika mechi nyingine ya mapema mchana KenGold ikicheza ugenini mjini Tabora, ilipata sare ya 1-1 na wenyeji Tabora United kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, huku kiungo Seleman Rashid ‘Bwenzi’ akifunga kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kuitangulia KenGold kwa bao la penalti.
Bwenzi alifunga penalti hiyo dakika ya 23 baada ya Chirwa kuchezewa madhambi kabla ya Heritier Makambo kusawzisha dakika ya 88 kwa kichwa akimalizia krosi iliyopigwa na Emmanuel Chilekwu.
Kabla ya kufunga leo, Bwenzi alifunga dhidi ya Yanga walipolala mabao 6-1, kisha kufunga wakati Kengold ikipata ushindi wa pili msimu huu walipoizamisha Fountain Gate kwa mabao 2-0 na sasa kufikisha mabao matatu, huku Makambo akifikisha matano hadi sasa.