Dar es Salaam. Yanga imerejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kishindo baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 6-1 dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam leo Februari 14, 2025.
Mabao mawili ya kipindi cha kwanza na manne kipindi cha pili, yameifanya Yanga kuandika rekodi ya kufunga mabao 12 katika mechi mbili za mwisho ndani ya Uwanja wa KMC na hakuna timu iliyowahi kufanya hivyo katika mechi mbili mfululizo ndani ya uwanja mmoja.

Mabao matatu (hat trick) ya Stephane Aziz Ki, na Maxi Nzengeli, Price Dube na Israel Mwenda waliofunga kila moja yametosha kuiwezesha Yanga kufikisha pointi 49 ambazo zimeirejesha juu ya kilele cha msimamo wa ligi ikiitangulia Simba yenye pointi 47 katika nafasi ya pili.
Kati ya mabao hayo matatu ya Aziz Ki, mawili yalikuwa ni ya mikwaju ya penalti jambo ambalo limemfanya amfikie Leonel Ateba wa Simba katika chati ya wachezaji wanaoongoza kwa kufunga idadi kubwa ya mabao kwa penalti ambapp kila mmoja amefumania nyavu mara nne.

Bao la Prince Dube limemfanya afikishe mabao nane na hivyo kuwafikia Elvis Rupia wa Singida Black Stars na Jean Ahoua na Leonel Ateba wa Simba ambao kila mmoja ana mabao nane wakiwa wanashika nafasi ya pilj katika chati ya kufumania nyavu.
KMC ambayo ilionekana kuzidiwa tangu dakika za mwanzoni mwa mchezo huo, ilifunga bao lake pekee kupitia kwa Redemptus Musa.

Kabla ya mchezo wa leo, Yanga ilipata ushindi kama huo katika Uwanja huohuo wa KMC Complex dhidi ya KenGold ya Mbeya.
Kichapo kutoka kwa Yanga kimeifanya KMC kubaki katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 21.
Mkoani Tabora katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, wenyeji Tabora United wamelazimishwa sare ya bao 1-1 na KenGold.
Bao la KenGold limefungwa na Seleman Bwenzi na lile la Tabora United limepachikwa na Heritier Makambo.
Kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera wenyeji Kagera Sugar wameibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate.
Peter Lwasa amekuwa shujaa wa Kagera Sugar baada ya kuifungia mabao mawili timu hiyo huku lingine likifungwa na Salehe Kambenga.