Yanga imeendeleza dozi katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la CRDB baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Coastal Union katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam leo.
Ushindi wa Yanga umetokana na mabao yaliyopachikwa na Maxi Nzengeli aliyefunga mawili na lingine moja likiwa la Clement Mzize huku bao la kufutia machozi la Coastal Union likipachikwa na Miraji Abdallah.
Kikosi cha Yanga hakikuwa na mabadiliko mengi kulinganisha na kile kilichozoeleka ambapo mchezaji mmoja tu alipumzishwa kumpisha ambaye amekuwa hapati nafasi ya kuanza kikosini.
Mchezaji huyo ni kipa Abuutwalib Mshery aliyechukua nafasi ya Djigui Diarra ambaye katika mchezo wa leo alianzia benchi.

Hakukuwa na mabadiliko makubwa kiuchezaji na Yanga ilitamba kwa kumiliki mpira kuanzia dakika ya kwanza hadi filimbi ya kumaliza mchezo ya refa Ramadhan Kayoko ilipopulizwa.
Bao la kwanza limefungwa na Maxi Nzengeli baada ya kuwatoka walinzi watatu wa Coastal Union na kupiga shuti lililojaa wavuni na dakika ya 14 akafunga bao la pili kwa shuti la mguu wa kulia akimalizia pasi ya Pacome Zouzoua.
Dakika ya 18, Miraji Abdallah aliifungia Coastal Union bao pekee kwa shuti kali lililomshinda kipa Mshery na kujaa wavuni lakini lilidumu kwa dakika tatu kwani dakika ya 21, Clement Mzize alipachika bao la tatu akimalizia pasi ya Prince Dube.
Ushindi huo umeifanya Yanga kukamilisha hatua ya 32 bora ya mashindano hayo ikiungana na timu nyingine 15.
Timu 16 zilizofuzu hatua ya 16 bora ni Yanga, Simba, Pamba Jiji, Kagera Sugar, KMC, Bigman, Singida Black Stars, Mbeya City, Mashujaa, Mtibwa Sugar, Stand United, Mbeya Kwanza, Girrafe Academy, JKT Tanzania, Tabora United na Songea United.
Hatua ya 16 bora ya mashindano hayo itaanza leo kwa uwepo wa mechi tatu ambazo zitachezwa katika viwanja na miji tofauti nchini.
Mkoani Manyara katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, wenyeji Singida Black Stars wataialika KMC, JKT Tanzania watakuwa Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kucheza na Mbeya Kwanza na katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Mbeya City itakabiliana na Mtibwa Sugar, michezo yote ikianza saa 10:00 jioni.