Yanga yamtupia virago Gamondi, msaidizi wake

Dar es Salaam. Klabu ya Yanga imemfuta kazi Kocha Mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi leo Ijumaa Novemba 15, 2024.

Taarifa ya kufutwa kazi kwa makocha hao imetolewa na Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Yanga ikisema:  “Uongozi wa Young Africans Sports Club unapenda kuutarifu umma kuwa umevunja mkataba na Kocha Mkuu wa kikosi cha kwanza, Angel Miguel Gamondi.

“Vilevile, Uongozi wa Young Africans Sports Club, umesitisha mkataba wa kocha msaidizi wa kikosi cha kwanza, Moussa Ndaw.”

Aidha, taarifa hiyo imesema uongozi wa Young Africans Sports Club unawashukuru makocha hao kwa mchango wao ndani ya Klabu yetu na unawatakia kila la kheri katika majukumu yao mapya.

“Tayari mchakato wa haraka wa kutafuta makocha wapya wa kikosi chetu cha kwanza umeanza na unatarajiwa kukamilika hivi punde,”imeongeza taarifa hiyo.

Hivi karibuni baada ya Yanga kulala kwa mabao 3-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi Tabora United, taarifa zilianza kuzagaa kuwa kocha huyo aliyechukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB msimu uliopita yupo kikaangoni.

Gamondi raia wa Argentina, ameondoka Yanga akiwa ameiacha timu hiyo ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kukusanya pointi 24 ikiwa nyuma ya vinara Simba kwa pointi moja tu.

Yanga sasa inajiandaa na mchezo wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, Novemba 26.