
YANGA imemalizana na Songea United katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho (FA) uliochezwa jana Jumamosi na kituo kinachofuata ni mkoani Tabora huku Kocha Mzimbabwe Genesis Mang’ombe anayeinoa Tabora United akionekana kuwa na hofu kutokana na kauli aliyoitoa.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara wanakwenda kukabiliana na Tabora United, timu ambayo ilichangia kusitisha safari ya Kocha Miguel Gamondi kuinoa Yanga kufuatia kichapo cha mabao 3-1, Uwanja wa Azam Complex, Novemba 7, 2024.
Kuelekea mchezo huo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Aprili Mosi, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, timu hizo zinakutana zote zikiwa na makocha wapya.
Tabora United kwa sasa inanolewa na Mang’ombe aliyechukua nafasi ya Mkongomani Anicet Kiazayidi wakati Yanga ikiwa chini ya Miloud Hamdi mwenye uraia wa Ufaransa na Algeria. Hamdi ni kocha wa tatu kuifundisha Yanga msimu huu baada ya Gamondi na Sead Ramovic.
Mang’ombe amesema ili kufanya vizuri katika mchezo dhidi ya Yanga, kuna mambo ni lazima wayafanyie kazi ikiwemo safu ya ulinzi na kiungo katika suala zima la kukaba.
“Kuna mambo ambayo lazima tuyarekebishe kama kweli tunataka matokeo mazuri dhidi ya Yanga, kwanza ishu ya kulinda mabao yetu kwani ukiangalia tuna uwezo wa kutangulia kufunga halafu wapinzani wanarudisha hali ambayo tunapaswa kuibadilisha,” alisema kocha huyo ambaye katika mchezo wake wa kwanza kuiongoza Tabora United ilifungwa na Kagera Sugar kwa penalti katika hatua ya 16 bora ya Kombe la FA, mechi iliyopigwa Ijumaa wiki hii.
Kauli ya kocha huyo ni wazi inaonesha kuwa na hofu na namna Yanga inavyofanya mashambulizi yake kwani msimu huu ndiyo timu yenye mabao mengi Ligi Kuu Bara ikifunga 58 kwenye mechi 22.
Rekodi zinaonesha katika mechi tano zilizopita ambazo Yanga imecheza kwenye ligi chini ya Kocha Hamdi, imefunga mabao 16, ikiwa na wastani wa kufunga mabao matatu kila mechi jambo ambalo kukutana na timu yenye ulinzi dhaifu kama Tabora iliyoruhusu mabao 28 katika mechi 23 kwao ni hatari.
Hata hivyo, Kocha Mang’ombe amesema licha ya kuondolewa katika Kombe la FA, lakini amefurahi kukiona kikosi chake kikicheza mechi ya kimashindano na kuona wapi pa kuanzia kabla ya kukabiliana na Yanga.
“Kilichonifurahisha katika mechi hii nimeweza kukisoma kikosi changu vyema, ili niweze kujua naanza kufanyia kazi kitu gani kwa haraka kabla ya mchezo wetu ujao wa ligi,” alisema Mang’ombe.
Tabora United inayoshika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikikusanya pointi 37, imeondoshwa hatua ya 16 bora ya Kombe la FA kufuatia kupoteza kwa penalti 5-4 nyumbani dhidi ya Kagera Sugar baada ya muda wa kawaida matokeo kuwa 1-1.
Timu hiyo inakwenda kukabiliana na Yanga inayoongoza msimamo wa ligi kwa pointi 58 huku mechi ya duru la kwanza Tabora United ikishinda 3-1 ugenini.