Yanga yaiweka rehani Azam FC Caf

KILA siku zinavyozidi kwenda, Azam FC inashuka kiwango huku kipigo cha mabao 2-1 ilichokipata kutoka kwa Yanga, kikiweka rehani nafasi yao ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao huku ikiwa rasmi sasa haitaweza kumaliza ligi kwa kufikisha pointi zaidi ya 63.

Azam iliyo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, imekubali kichapo hicho ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar.

Mabao ya Pacome Zouzoua dakika ya 11 na Prince Dube dakika ya 34, yamehitimisha ushindi huo ambao umeifanya Yanga kufikisha pointi 67, ikijikita zaidi kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kucheza mechi 25 zikibaki tano, ikiiacha Simba nafasi ya pili na pointi 57 ikibakiwa na mechi nane, tofauti ni pointi 10. Azam bao lao limefungwa na Lusajo Mwaikenda dakika ya 81.

Azam ni ya tatu na pointi zake 51, moja zaidi ya Singida Black Stars yenye 50, zote zimecheza mechi 26 na kubakiwa nazo nne. Ile nne bora, rasmi itabaki kwa timu hizo, lakini zinaweza kubadilishana nafasi kwa mechi zilizobaki japo hakuna nyingine zaidi yao inayoweza kufika hapo kwa msimu huu kutokana na hesabu za pointi zilivyo kwani Tabora United inayoshika nafasi ya tano, ikishinda mechi zake nne itaishia pointi 49.

Kitendo cha Azam kupoteza mchezo huo, kinahatarisha nafasi yao ya tatu kwani Singida Black Stars ikichanga vizuri hesabu zake inaweza kuipiku katika mechi nne zilizobaki.

Katika mechi hizo nne, Azam itacheza dhidi ya Kagera Sugar (ugenini), Dodoma Jiji (nyumbani), Tabora United (nyumbani) na

Fountain Gate (ugenini). Singida BS mechi zake nne itacheza dhidi ya Tabora United (nyumbani), Simba (ugenini), Dodoma Jiji (ugenini) na Tanzania Prisons (nyumbani).

Endapo Azam itashushwa na Singida Black Stars kisha ikamaliza ligi nafasi ya nne, inaweza kuwa mbaya zaidi kwao na kujikuta ikikosa nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.

Uhatari wa Azam kuikosa nafasi ya kimataifa unatokana na ukweli kwamba timu hiyo tumaini lao pekee limebaki kwenye ligi kumaliza nafasi ya tatu ili kucheza Kombe la Shirikisho Afrika kwani Tanzania ina tiketi ya kupeleka timu nne kimataifa, itakayomaliza ya kwanza na ya pili zitashiriki Ligi ya Mabingwa, huku ya tatu na bingwa wa Kombe la FA, zitashiriki Kombe la FA. Kama bingwa wa FA atakuwa tayari na tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa, basi nafasi hiyo itachukuliwa na aliyeingia fainali na kama aliyeingia fainali naye atakuwa na tiketi kama hiyo, ndipo timu itakayomaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi itapewa tiketi hiyo.

Kwa sasa timu zilizopo Kombe la FA ni nane zikiwa hatua ya robo fainali ambazo ni Yanga, Simba, Singida Black Stars, JKT Tanzania, Pamba Jiji, Kagera Sugar, Mbeya City na Stand United.

Kilichopo kwa Azma hivi sasa ni kuhakikisha haitoki nje ya tatu bora kwani inafahamu kuwa ina mtego huo kwani timu zilizopo robo fainali ya Kombe la FA zisizokuwa na uwezo wa kumaliza nne bora kwenye ligi, nazo zinapiga hesabu nafasi ya kucheza kimataifa.

MCHEZO ULIVYOKUWA

Kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ moto ni uleule kwenye kutengeneza nafasi akibakiza pasi tatu kufikia rekodi ya Clatous Chama baada ya kumtengenezea nafasi Lusajo Mwaikenda dakika ya 81 aliyekwamisha bao la kufutia machozi.

Bao la Pacome ambalo ni la 10 kwake msimu huu limefungwa dakika ya 11 ya mchezo baada ya kukwamisha mpira uliopigwa na Dube ambaye amefunga bao lake la 12 dakika ya 34 akimfikia kiungo wa Simba, Charles Ahoua.

Mchezo ulianza kwa Yanga kuliandama zaidi lango la Azam FC ambao hawakufika golini kwa wapinzani wao kwa dakika 19 baada ya making wa watetezi kuandika bao la kuongoza.

Mfungaji wa bao la kwanza kwa upande wa Yanga, Pacome alitolewa dakika ya 19 baada ya kufanyiwa madhambi na Yahya Zayd na nafasi yake kuchukuliwa na Clement Mzize.

Mchezo ulikuwa upande wa Yanga zaidi ambao walionyesha kuliandama zaidi lango la wapinzani wao na kufanikiwa kuchonga kona saba ambazo hata hivyo hazikuwa na madhara langoni mwa Azam FC kwani hakuna iliyoamua bao.

Kwa upande wa Azam FC wao walipiga kona moja tu huku mabadiliko yaliyofanywa na kocha wao yakionyesha uhai kikosini kwa kujaribu kufika mara kwa mara langoni kwa Yanga.

Kipindi cha pili Azam FC walirudi kwa kasi lakini ubora wa Yanga kuanzia eneo la kiungo uliwadhibiti na kushindwa kujenga mashambulizi langoni mwa wapinzani wao wakijikuta mipira yao inaporwa kirahisi.

Dakika ya 62 Azam FC walifanya mabadiliko wakimtoa Abdul Suleiman Sopu na nafasi yake ilichukuliwa na Zidane Sereri na Pascal Msindo alitoka nafasi yake ilichukuliwa na Nathanael Chilambo wakati Yanga dakika ya 67 ilimtoa Clatous Chama na nafasi yake ilichukuliwa na Stephane Aziz Ki, alitoka Dube akaingia Jonathan Ikangalombo.

COASTAL 2-1 SINGIDA BS

Mechi nyingine jana ilishuhudiwa Coastal Union ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Coastal ilianza kufunga dakika ya 47 baada ya kiungo wa Singida BS, Arthur Bada kujifunga katika harakati za kuokoa faulo iliyopigwa na Lucas Kikoti.

Jonathan Sowah akaisawazishia Singida BS kwa mkwaju wa penalti dakika ya 76 na kufikisha mabao tisa kwenye ligi akicheza mechi 10 ambapo nyota huyo ametua kikosini hapo dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15 mwaka huu. Bakari Msimu akaihakikishia Coastal ushindi kwa bao la dakika ya 82.

Ushindi huo ni wa kwanza Coastal Union inaupata baada ya kupita mechi nane kwani mara ya mwisho ilishinda 2-1 dhidi ya JKT Tanzania, Februari 7 mwaka huu.

Coastal imepanda hadi nafasi ya 10 kutoka ya 13 ikifikisha pointi 28 ikibakiwa na mechi nne kumaliza msimu huu.

Kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni, Dar, wenyeji JKT Tanzania walitoka nyuma na kulazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya Namungo.

Namungo ilifunga mabao mawili kupitia Saleh Karabaka (dk 18) na Fabrice Ngoy (dk 49), kabla ya JKT Tanzania kusawazisha, wafungaji ni Maka Edward (dk 63) na Shiza Kichuya (dk 69).

Sare hiyo imeifanya JKT Tanzania kubaki nafasi ya saba na pointi 32, huku Namungo ikibaki palepale ya 11 ingawa imeishusha Pamba Jiji, zote zikiwa na pointi 28.

Mashujaa ikiwa uwanja wake wa nyumbani wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, imeibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United, ambapo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, wenyeji walikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Mundhir Abdullah (dk 8) na Jafari Kibaya (dk 45+5).

David Richard akahitimisha ushindi huo kwa bao la dakika ya 87 na kuifanya Mashujaa kufikisha pointi 30 ikipanda nafasi moja kutoka tisa hadi ya nane.

Ligi hiyo imesimama hadi Aprili 18 mwaka huu ikiendelea raundi ya 27 ambapo sasa inapisha mechi za robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *