Yanga yaitangazia vita Azam Kombe la Muungano

Dar es Salaam. Wakati ratiba ya mashindano ya Kombe la Muungano 2025 ikitoka leo, Yanga imesema inatamani kukutana na Azam FC katika hatua ya fainali ili ichukue ubingwa mbele yao.

Mashindano hayo yatafanyika visiwani Zanzibar katika Uwanja wa New Amaan Complex kuanzia Aprili 23 hadi Aprili 30 mwaka huu.

Timu nane zitashiriki mashindano hayo ambazo ni Yanga, Azam, Coastal Union, Singida Black Stars, Zimamoto, KVZ, JKU na KMKM.

Ofisa habari na mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe amesema kuwa lengo lao ni kutwaa ubingwa wa Kombe la Muungano lakini itafurahisha kama watafanya hivyo kwa kuifunga Azam FC kwenye fainali.

“Haya ni mashindano makubwa kwa vile yanashirikisha bingwa wa Tanzania Bara na bingwa wa Tanzania Visiwani sasa kwa huku kwetu sisi Yanga ndio mabingwa hivyo ni lazima ili kombe tuchukue ili tuwe mabingwa wa jumla.

“Kombe la Muungano lipo kwenye fikra zetu hivyo tunaenda Zanzibar kwa ajili ya kuchukua hilo kombe na tutaenda na kikosi kamili. Azam na timu nyingine yoyote ambayo inataka kukutana na sisi, ipambane tucheze fainali. Raha za mashindano haya ni Yanga kuchukua ubingwa na hasa kuchukua mbele ya timu kama Azam” amesema Kamwe.

Yanga na Azam hakuna uwezekano wa kukutana katika hatua ya robo fainali au nusu fainali ingawa mechi baina yao inaweza kuwa ya fainali iwapo timu zote mbili zitafanikiwa kufuzu.

Kamati ya maandalizi na usimamizi wa mashindano hayo, imeipanga Yanga kukutana na KVZ katika hatua ya robo fainali Aprili 25 na Azam FC itaumana na KMKM, Aprili 24.

Mechi ya robo fainali itakayofungua mashindano hayo msimu huu itakuwa ni kati ya JKU na Singida Black Stars ambayo itachezwa Aprili 23 na kesho yake Aprili 24, Zimamoto itaikabili Coastal Union.

Katika hatua ya nusu fainali ambayo itachezwa Aprili 27 na Aprili 28, mshindi wa mechi baina ya JKU na Singida Black Stars atakutana na mshindi wa mchezo baina ya KMKM na Azam na timu itakayosonga mbele baina ya Zimamoto na Coastal Union itakabiliana na mshindi baina ya KVZ na Yanga.

Mechi zote za mashindano hayo zitachezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar na kwa mujibu wa ratiba ya mashindano hayo, hatua ya fainali itachezwa Aprili 30, kuanzia saa 2:30 usiku.

Iwapo Yanga na Azam FC zitakutana katika hatua ya fainali, zitatoa jibu la nani zaidi baina yao msimu huu baada ya kila moja kuibuka na ushindi katika mechi mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara ambazo zimekutana msimu huu.

Mchezo wa mzunguko kwa kwanza wa ligi baina yao, Azam FC iliibuka na ushindi wa bao 1-0 na ziliporudiana, Yanga ikaibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *