Yanga yaipiga Tabora United, Dube, Mzize wamkaribia Ahoua

KISASI ni haki! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga SC kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United, katika mchezo uliopigwa leo kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora na kulipa kisasi cha kufungwa nyumbani 3-1 mechi ya kwanza.

Yanga ilifungua ukurasa wa mabao dakika ya 21, baada ya beki wa kulia wa timu hiyo, Israel Mwenda kupiga frii-Kiki kali nje ya eneo la 18, kufuatia mshambuliaji, Prince Dube kufanyiwa madhambi na nyota wa Tabora Mkongomani, Andy Bikoko.

Wakati Tabora ikisaka kukomboa bao hilo, Clement Mzize alipachika la pili dakika ya 57, kabla ya Prince Dube kutupia la tatu dakika ya 68 na kuwafanya nyota hao kufikisha mabao 11 ya Ligi Kuu msimu huu, nyuma ya Jean Charles Ahoua wa Simba mwenye 12.

Kichapo hicho, ni cha kwanza kwa kocha mpya wa timu hiyo Mzimbabwe, Genesis ‘Kaka’ Mangombe, katika Ligi Kuu Bara tangu atambulishwe Machi 28, 2025, akirithi nafasi ya Mkongomani Anicet Kiazayidi aliyeondoka baada ya kuongoza kwenye michezo 14.

Mangombe alizifundisha Dynamos FC na Yadah Stars FC zote za kwao Zimbabwe, amerithi nafasi ya Anicet aliyetangazwa rasmi Novemba 2, 2024, ambapo katika michezo hiyo 14 alishinda saba na sare mitano huku miwili iliyobaki akiambulia kichapo.

Ushindi kwa Yanga umekifanya kikosi hicho kucheza michezo 13 mfululizo ya Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza tangu mara ya mwisho ilipochapwa mabao 3-1 dhidi ya Tabora United, Novemba 7, 2024, ikishinda 12, huku mmoja tu ukiisha kwa matokeo ya 0-0 dhidi ya JKT Tanzania.

Mbali na hilo, Yanga pia imelipa kisasi cha kupoteza mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam Novemba 7, 2024, dhidi ya Tabora United, baada ya kuchapwa kwa mabao 3-1, kipindi hicho ikiwa chini ya Kocha, Miguel Gamondi aliyeondoka kikosini.

Ushindi kwa Yanga umeifanya kufikisha pointi 61, baada ya michezo 23 na kuendelea kukaa kileleni, huku kwa upande wa Tabora United ikiendelea kusalia nafasi ya tano na pointi zake 37, kufuatia kucheza mechi 24 msimu huu.

Kikosi cha Tabora United: Jean-Noel Amonome, Kelvin Pemba/ Abdallah Seseme, Banele Junior/ Ibrahim Hamad Hilika, Shafih Maulid, Emmanuel Chilekwu, Nelson Munganga/ Shedrack Asiegbu, Emmanuel Mwanengo/ Yassin Mustafa, Andy Bikoko, Joseph Akandwanaho/ Ramadhani Chobwedo, Offen Chikola, Heritier Makambo.

Kikosi cha Yanga: Djigui Diarra, Israel Mwenda, Chadrack Boka, Dickson Job, Ibrahim Hamad ‘Bacca’/ Bakari Mwamnyeto, Duke Abuya, Maxi Mpia Nzengeli/ Jonathan Ikangalombo, Mudathir Yahya/ Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, Prince Dube/ Farid Mussa, Pacome Zouzoua, Clement Mzize/ Shekhan Ibrahim Khamis.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *