
WAKATI ikibaki siku mbili kabla ya Yanga na Simba kukutana katika pambano ya Ligi Kuu Bara litakalopigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, rekodi zinawabeba zaidi watetezi hao tofauti na Wekundu wa Msimbazi.
Mchezo huu utakaokuwa wa 114, kwa timu hizi kukutana katika Ligi Bara tangu 1965, rekodi zinaonyesha Yanga imekuwa timu tishio kwa michezo iliyocheza hadi sasa kwenye kuzifumania nyavu kwa kila kipindi, tofauti na wapinzani wao Simba.
Yanga inayoongoza Ligi Kuu na pointi 58, baada ya kucheza michezo 22, ikishinda 19, sare mmoja na kupoteza miwili, rekodi zinaonyesha imekuwa na safu kali ya kufumania nyavu kwenye vipindi vyote viwili, ukilinganisha na washindani wao.
Katika michezo hiyo 22, Yanga imefunga mabao 58 ikiwa ndio kinara wa kufumania nyavu hadi sasa, ambapo 30 kati ya hayo imeyafunga kipindi cha kwanza, huku 28, ikiyapachika cha pili, ikionyesha kikosi hicho kina safu kali ya ushambuliaji.
Katika mabao hayo, mawili ni ya kujifunga kwa wapinzani ambapo moja ni la beki wa kulia wa Simba, Kelvin Kijili dakika ya 86, akiwa kwenye harakati za kuuokoa mpira, wakati kikosi hicho cha Msimbazi kilipochapwa bao 1-0, Oktoba 19, 2024.
Bao jingine ni kujifunga pia la beki wa kati wa Fountain Gate, Jackson Shija dakika ya 53, wakati timu hiyo ilipochapwa mabao 5-0, Desemba 29, 2024, hivyo kusababisha muda mfupi tu aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Mohamed Muya kutimuliwa.
Kwa upande wa Simba iliyopo nafasi ya pili na pointi zake 54, baada ya kucheza michezo 21, ikishinda 17, sare mitatu na kupoteza mmoja, imefunga mabao 46 pungufu ya 12 nyuma ya Yanga, ambapo 26 ni ya kipindi cha kwanza na 20, ya kipindi cha pili.
Mchezo huu huenda ukatoa taswira ya vita ya ubingwa msimu huu kutokana na gepu la pointi lililopo baina yao, japo Yanga inaingia na rekodi nzuri baada ya mchezo wa kwanza kushinda kwa bao 1-0, la kujifunga la Kelvin Kijili Oktoba 19, 2024.
Simba imepoteza mechi tatu mfululizo za ligi dhidi ya Yanga.
Vipigo vitatu mfululizo katika Ligi Kuu vilianza na kile cha mabao 5-1, Novemba 5, 2023, kisha 2-1 Aprili 20, 2024, na cha mwisho cha bao (1-0), Oktoba 19, 2024.
Mchezo huu ni wa kisasi zaidi kwa Simba kutokana na rekodi mbovu kwa wapinzani wao kwa sababu mara ya mwisho kushinda ilikuwa ushindi wa mabao 2-0, Aprili 16, 2023, yaliyofungwa na beki wa zamani wa timu hiyo, Henock Inonga na Kibu Denis.