
Azam FC ina deni la kupata ushindi dhidi ya Yanga ugenini leo kwenye Uwanja wa Azam Complex kuanzia saa 12.00 jioni ili ifaulu mitihani miwili ambayo imeonekana kuwa migumu kwa timu mbalimbali tangu msimu huu ulipoanza hadi sasa.
Mtihani wa kwanza ambao Azam itafaulu ikiwa itaondoka na pointi tatu dhidi ya Yanga leo ni kuwa timu ya kwanza kupata ushindi mbele ya vinara hao wa msimamo wa ligi, jambo ambalo limekuwa gumu kufanyika katika mechi 14 za mashindano tofauti rasmi ambazo imecheza hadi hivi sasa na imeshinda zote.
Yanga imeshinda mechi mbili za Ngao ya Jamii, imepata ushindi katika mechi nne za Ligi ya Mabingwa Afrika na pia imeondoka na pointi tatu katika mechi nane za Ligi Kuu Bara.
Mtihani wa pili ambao Azam itakuwa nao ikiwa itaibuka na ushindi mbele ya Yanga leo itakuwa timu ya kwanza kufunga bao/mabao dhidi ya mabingwa hao watetezi wa taji la Ligi Kuu kwani mechi zote nane ambazo Yanga imecheza hadi sasa, haijaruhusu nyavu zake kutikisika huku ikifumania nyavu mara 13.
Licha ya kutoanza vyema ligi msimu huu, Azam FC imeonekana kuimarika siku za hivi karibuni jambo ambalo linaashiria mchezo wa leo unawza kuwa mgumu na wenye ushindani kwa pande zote.
Tangu ilipopoteza dhidi ya Simba kwa mabao 2-0, Azam FC imecheza mechi tano mfululizo za ligi bila kupoteza ikiibuka na ushindi katika michezo minne na kutoka sare moja huku ikifunga mabao saba na kufungwa bao moja tu.
Hesabu za mbali
Ushindi katika mechi ya leo utaifanya Yanga iendelee kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi ambapo itafikisha pointi 27 huku ikibakiwa na mechi moja ya kiporo mkononi.
Azam FC ikipata ushindi, itafikisha pointi 22 ambazo zitaifa izidi kujikita kwenye nafasi ya nne katika msimamo wa ligi.
Kitendo cha Yanga kuondoka na pointi tatu leo, kitaifanya iongeze pengo la pointi baina yake na Azam FC kufikia tisa na kubaki kwao na mchezo mmoja wa kiporo mkononi, maana yake kutaweka uwezekano mkubwa wa kuzika ndoto za Azam kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu.
Pointi tatu za mchezo wa leo zitakuwa na faida kubwa kwa Azam FC kwani mbali na kuifanya ipate pointi za kuikaribia Yanga, itaendelea kuzipa presha Simba na Singida Balck Stars ambazo ziko juu yake kwa sasa.
Yanga na upepo mzuri
Yanga imekuwa na ubabe dhidi ya Azam katika miaka ya hivi karibuni ambapo katika mechi nyingi walizokutana imekuwa ikipata matokeo mazuri pamoja na ushindani mkubwa ambao timu hizo zimekuwa zikionyesha kwenye mechi za0.
Mfano wa hilo unaweza kuonekana katika mechi tano zilizopita hivi karibuni za mashindano tofauti baina yao, Yanga imeibuka na ushindi mara nne na Azam FC imepata ushindi mara moja tu.
Uwanja wa Azam Complex ambao utatumika kwa mechi hiyo, umekuwa na historia nzuri kwa Yanga katika mechi za Ligi Kuu ambapo tangu imeanza kuutumia, haijawahi kupoteza mechi yoyote hapo.
Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana kwenye Uwanja wa Azam Complex katika Ligi ilikuwa ni 06/04/2022 ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 yaliyowekwa kimiani na Djuma Shaban na Fiston Mayele huku lile la Azam likipachikwa na Rodger Kola.
Katika mechi tatu za Ligi ambazo Azam FC imecheza kwenye Uwanja wa Azam Complex msimu huu, imepata ushindi mara mbili na kutoka sare moja huku Yanga ikipata ushindi kwenye mechi zote tatu ilizocheza uwanjani hapo.
Hisia za makocha
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema kuwa licha ya muda mfupi walioupata wa kujiandaa na mchezo huo, shauku yao ni kupata ushindi.
“Tupo sawa. Tumejiandaa kwa uwezo wetu, hatukupata muda wa kutosha kujiandaa na mechi hii lakini siku zote tuko tayari. Lolote linaweza kutokea na kwenye soka ni jambo la kawaida. Nimebarikiwa kuwa na kundi kubwa la wachezaji ambao wanacheza vizuri na kuonyesha wanastahili kucheza Yanga.
“Azam ni timu nzuri, ina wachezaji wazuri na kocha mzuri. Na kiukweli itakuwa ni vita. Siwezi kuahidi chochote kwa vile tunaziheshimu timu nyingine zote. Kwetu tuna shauku kubwa ya kushinda mchezo,” alisema Gamondi.
Kocha wa Azam FC, Rachid Taoussi alisema kuwa mchezo wa leo ni fursa ya wachezaji wa timu yake kuonyesha thamani yao.
“Napenda mechi hizi kwa sababu Azam ina wachezaji wakubwa. Wachezaji sita katika timu za taifa. Tuna wachezaji wenye uzoefu na vipaji hivyo kwangu mimi ni jambo zuri kufanya kazi na wachezaji hawa.Tunatakiwa kucheza vizuri na kama tukiwa katika ubora wetu, naamini ushindi lazima.
“Naitazama zaidi timu yangu. Tuna uwezo wa kupata ushindi. Kama tutakuwa na uwezo mzuri wa kumalizia nafasi na kuwa na uwiano mzuri wa kushambulia na kuzuia naamini tutafanya vizuri,” alisema Taoussi.
Singida BS kujiuliza kwa Coastal Union
Baada ya kupoteza mechi iliyopita dhidi ya Yanga, Singida Black Stars leo itakuwa tena katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kuikabili Coastal Union kuanzia saa 2:30 usiku.
Wageni Coastal Union hapana shaka wako katika hali nzuri kisaikolojia wanapoingia katika mechi ya leo, ambayo imetokana na ushindi wa bao 1-0 walioupata mbele ya Kagera Sugar katika mchezo uliopita.
Kocha wa Coastal Union, Juma Mwambusi alisema wamejiandaa kikamilifu ili waweze kupata ushindi katika mechi ya leo.
“Najua tunakutana na timu yenye nguvu, lakini wachezaji wangu wamejiandaa kwa hali yoyote. Lengo letu ni kupata matokeo mazuri, na nadhani tunaweza kufanikisha hilo kwa nidhamu na umakini wa hali ya juu,” alisema Mwambusi.
Kocha Patrick Aussems wa Singida BS anataka wachezaji wake kucheza kwa nguvu leo na kuonyesha nidhamu ya juu katika safu ya ulinzi.
“Baada ya kupoteza dhidi ya Yanga, tunahitaji kushinda kesho (leo) ili kujirejesha kwenye hali nzuri. Coastal ni timu yenye nidhamu, lakini tunahitaji pointi tatu, na wachezaji wangu wamejiandaa kwa changamoto hiyo,” alisema Aussems.