
NI kama fainali ya kuviziana, kwani kila upande unataka kufanya vizuri ili uongeze au uweke rekodi.
Kikosi cha Yanga usiku wa leo Alhamisi kitakuwa uwanjani kuwakabili JKU ya Zanzibar katika fainali ya Kombe la Muungano, huku nahodha wa hiyo, Dickson Job akifichua siri ya chozi alililomwaga mara baada ya mechi ya nusu fainali ywa michuano hiyo dhidi ya Zimamoto iliyowang’oa kwa penalti 3-1.
Yanga ilisubiri hadi hatua ya penalti baada ya dakika 90 za pambano hilo kuisha kwa sare ya 1-1 baada ya kipa wa timu hiyo, Abuutwalib Mshery kufanya kosa la kizembe lililowapa Zimamoto bao la kusawazisha kipindi cha pili na sasa leo inavaana na JKU ambao ni watetezi wa Ligi Kuu Zanzibar.
MECHI YA KUVIZIANA
Yanga, wanaoshikilia ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa tatu mfululizo kwa sasa itashuka uwanjani kuvaana na mabingwa wenzao wa Zanzibar, JKU iliyowatoa nishai Azam FC kwa kuifunga mabao 2-1 katika mchezo mwingine wa nusu fainali. Timu hizo ndizo mabingwa wa Ligi za Tanzania Bara na Zanzibar na leo itakuwa mechi ya kibabe kusaka mkali wao kwa Muungano.
Timu zote zitashuka kwenye Uwanja wa Gombani kuanzia saa 1:15 usiku kila moja ikiwa na lengo tofauti, Yanga ikitaka kuboresha rekodi ya kubeba mara nyingi taji la michuano hiyo, lakini JKU ikisaka ubingwa wa kwanza kwani haijawahi kutwaa taji hilo na hizi ni fainali za kwanza kwao.
Rekodi zinaonyesha tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo 1982, Yanga imetwaa mara sita miaka ya 1983, 1987, 1991, 1996, 1997 na 2000 ikilingana na Simba iliyotwa 1993, 1994, 1995, 2001, 2002 na mwaka jana iliporejeshwa ikiifunga Azam kwa bao 1-0 kwenye fainali iliyopigwa Uwanja wa Amaan.
Yanga inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu ikisaka taji la msimu wa nne mfululizo, inahiotaji kushinda ili kufikisha taji la saba na kuwa vinara mbele ya watani wao walishindwa kwenda kutetea taji hilo kutokana na kutingwa na ratiba ngumu ya michuano ya CAF ikitinga fainali y Kombe la Shirikisho.
Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi alisisitiza kwamba anahitaji kubeba kombe hilo ili kuwaweka sawa wachezaji kabla ya kumalizana na mechi za Ligi Kuu na nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya JKT itakayopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga siku ya Agosti 16.
Hata hivyo, mastaa wa Yanga wana kibarua mbele ya wenzao wa JKU ambao walianza michuano hiyo kwa kuing’oa Singida Black Stars kwa penalti 6-5 baada ya dakika 90 kufunga mabao 2-2 wakitoka nyuma mbele ya wauza alizeti hao wa Singida, inayoshika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu.
JOB HUYU HAPA
Mara baada ya penalti zilizoivusha Yanga kutinga fainali dhidi ya Zimamoto juzi, beki huyo wa kati, Job alimwaga chozi na kuibua hisia pengine nafurahia timu kutinga fainali, lakini yeye amefafanua alipozungumza na Mwanaspoti.
Job alisema aliyemliza na kipa Mshery ambaye licha ya kutoa ‘boko’ katika dakika 90 za mchezo huo, lakini ndiye aliyegeuka shujaa kwa kuokoa penalti mbili kati ya tatu zilizopotezwa na Zimamoto iliyowang;oa Coastal Union katika hatua ya robo fainali kwa kuifunga bao 1-0.
Job, alisema katika mechi hiyo ya nusu fainali, hawakuanza vizuri hasa eneo la ulinzi na hasa kwa kipa Mshery, ambaye alifanya kosa lililoonekana na kila mmoja kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba kunakofanyikia michuano hiyo iliyorejeshwa kwa msimu wa pili sasa baada ya kusimamia mwaka 2003.
Nahodha msaidizi huyo wa Yanga, alisema kila mmoja aliona makosa ya wazi ambayo kwa upande wa timu hiyo yalifanyika, lakini baadaye mambo yalibadilika na kuwa tofauti.
“Tulipofika hatua ya matuta kila mtu alikuwa na hofu, hata mimi nilipatwa na hali hiyo, lakini kubwa iliyofanywa na Mshery ambaye ni rafiki yangu aliyegeuka ndugu kwa sasa ilinifanya nilie kwa furaha. Nilishindwa kujizuia kwa furaha nikajikuta nalia tu, sio kwa kufuzu ila kwa kazi ya Mshery,” alisema Job ambaye pamoja na mabeki Kibwana Shomary, Nickson Kibabange na Mshery wameibuka wakicheza wakiwa pamoja tangu wakiwa Moro Kids ya Morogoro kisha timu za taifa za vijana na sasa Yanga.
“Kwani nilikuwa naelewa, isingekuwa kazi rahuisi kuhimili aibu kwa timu kubwa kama ya Yanga kutolewa nusu fainali y michuano hii ya Kombe la Muungano,” alifafanua Job na kuongeza;
“Nawaheshimu wapinzani tuliocheza nao, lakini wakati huo ushindi na utaka kwa ajili ya timu na rafiki yangu amalize mechi kwa rekodi nzuri.”