Yanga, Singida BS mechi ya presha Ligi Kuu

Dar es Salaam. Hakuna kuzubaa ndiyo kauli mbiu ya duru la pili katika Ligi Kuu Bara wakati mchakamchaka wa ligi hiyo ukiingia raundi ya 20, huku Kocha wa Yanga Miloud Hamdi akienda kukutana na klabu iliyomleta Tanzania kwa mara ya kwanza, Singida Black Stars kabla ya kuibukia Yanga.

Katika raundi hiyo, leo zinaanza kupigwa mechi mbili zikikutanisha timu zote zenye presha ya kupata matokeo ya ushindi. Presha hiyo inatokana na kila mmoja nafasi aliyopo sambamba na aina ya matokeo waliyoyapata katika mchezo uliopita. Kumbuka mechi zote hizo za leo zitachezwa kuanzia saa 10:00 jioni.

Yanga vs Singida Black Stars

Unaweza kusema hii ni mechi ya kibingwa, Yanga yenye pointi 49 baada ya kucheza mechi 19, inapambana kuongeza gepu dhidi ya Simba inayoshika nafasi ya pili na pointi 47 katika michezo 18.

Singida Black Stars iliyotoka kuvunja rekodi ya JKT Tanzania iliyokuwa timu pekee ambayo haikupoteza nyumbani msimu huu kabla ya kufungwa 1-0, nayo inahitaji pointi tatu zitakazowaweka sehemu nzuri zaidi kwenye msimamo kwani inafahamu kwamba kupoteza kwao kunaweza kuhatarisha kukaa nafasi ya nne kwani Tabora United inakuja kwa kasi.

Hivi sasa Singida Black Stars ikiwa na pointi 37, imeizidi Tabora United pointi tano zikipishana nafasi ya nne na tano.

Yanga inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Singida Black Stars ilioupata duru la kwanza kupitia mfungaji Pacome Zouzoua dakika ya 67.

Rekodi zinaonyesha mechi tano za mwisho Yanga imekuwa na matokeo mazuri zaidi ya wapinzani wao kwani imeshinda nne na sare moja wakati Singida imeshinda mbili na kupoteza mbili, sare moja.

Kwa mechi za nyumbani, Yanga imecheza 10 na kukusanya pointi 24 zilizotokana na kushinda 8 na kupoteza 2, imefunga mabao 30 na kuruhusu 7, hali hiyo inadhihirisha kuwa safu yao ya ushambuliaji ni hatari lakini ulinzi upo imara.

Singida Black Stars iliyotoka kucheza ugenini mechi mbili ikipoteza moja mbele ya KMC kwa mabao 2-0 kabla ya kushinda 1-0 dhidi ya JKT Tanzania, rekodi ya ugenini inaonyesha imecheza mechi 9 na kukusanya pointi 19.

Ikumbukwe kwamba mchezo huu utamkutanisha Kocha Miloud Hamdi na kikosi cha Singida Black Stars alichokuwa akikinoa tangu Desemba 30, 2024 kabla ya kutambulishwa Yanga Februari 4, 2025 akichukua mikoba ya Sead Ramovic.

Fountain Gate vs Tabora United

Ni mchezo ambao utachezwa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa nyumbani kwa Fountain Gate, timu ambayo imekuwa haina matokeo mazuri katika mechi tano zilizopita.

Fountain Gate inayofundishwa na kocha Robert Matano, inarejea uwanja wa nyumbani baada ya kucheza mechi mbili mfululizo ugenini ambazo zote imepoteza tena bila ya kufunga bao dhidi ya KenGold (2-0) na Kagera Sugar (3-0), kabla ya hapo ilitoka 1-1 na Simba nyumbani.

Wakati Fountain Gate leo ikiwa nyumbani, rekodi zinaonyesha timu hiyo kwao imekusanya pointi 15 katika mechi 10 ikishinda nne, sare tatu na kupoteza tatu, ikifunga mabao 18 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 16.

Inakutana na Tabora United ambayo baada ya kushinda mechi mbili mfululizo, ikajikuta ikisimamishwa na KenGold kwa sare ya 1-1.

Walima asali hao kutoka Tabora wanaofundishwa na Anicet Kiazayidi, wanakwenda ugenini wakiwa na ufahamu kwamba rekodi zao wakiwa uwanja wa nje ya kwao wamekusanya pointi 13 baada ya kucheza mechi nane, wameshinda nne, sare moja na kupoteza tatu wakifunga mabao 12 na kufungwa 13.

Hapo katika kufungwa, inaonyesha timu zote hazipo imara eneo la kulinda jambo ambalo linaashiria tunaweza kushuhudia mchezo wenye mabao.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana Septemba 20, 2024 ambapo wageni Fountain Gate walishinda 3-1.