Yanga, Simba yaahirishwa, kupangiwa tarehe nyingine

Dar es Salaam. Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara imeahirisha mechi ya mzunguko wa pili wa ligi baina ya Yanga na Simba iliyokuwa ichezwe leo Jumamosi, Machi 8, 2025 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Uamuzi huo umefikiwa kufuatia uamuzi wa Simba kugomea kucheza mechi ikidai imenyimwa haki ya kikanuni ya kufanya mazoezi katika uwanja wa mechi siku moja kabla.

Taarifa ya TPLB imesema kuwa mechi hiyo imeahirishwa ili bodi ipate fursa ya kuchunguza zaidi undani wa tukio hilo.

“Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha leo Machi 8, 2025 ilipitia shauri la klabu ya Simba kuzuiliwa kuingia kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo namba 184 wa Ligi Kuu ya NBC (Young Africans SC vs Simba SC) uliopanga kufanyika kwenye uwanja huo leo kuanzia saa 1:15 usiku.

“Katika shauri hilo, klabu ya Simba iliandikia barua Bodi ya Ligi kueleza kuhusu tukio tajwa hapo juu, huku pia ikieleza nia yao ya kutoshiriki mchezo huo kwa sababu imezuiliwa kutumia haki yao ya kikanuni kama ilivyainishwa kwenye Kanuni ya 17:45 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

“Baada ya kupokea barua hiyo, Bodi ya Ligi iliwaagiza maofisa wake wa mchezo (ambao walishuhudia tukio hilo), kutuma taarifa ya tukio haraka ili hatua zinazostahili ziweze kuchukuliwa, ikiwemo kuitishwa kwa kikao cha dharura cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi Baada ya kupitia taarifa mbalimbali zikiwemo za maofisa wa mchezo na vyanzo vingine, Kamati ilibaini kuwa Klabu ya Simba, wakati ikielekea kutumia haki yake iliyoainishwa kwenye Kanuni ya 17:45 ya Ligi Kuu, haikuwasiliana na ofisa yeyote wa mchezo, timu mwenyeji wala mamlaka ya wanja kuhusu nia yao ya kufanya mazoezi katika wanja huo ili maandalizi ya kikanuni yafanyike,” imefafanua taarifa hiyo ya TPLB.

TPLB imeongeza kuwa ripoti ya usalama ndio imepelekea kuahirishwa kwa mechi hiyo.

“Katika taarifa hizo, Kamati ilibaini pia kuwa walinzi ambao baadhi walifahamika kwa sura kuwa ni wa klabu ya Yanga, walishiriki tukio la kuzuia basi la klabu ya Simba kuingia uwanjani kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:45 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

“Kwa sababu pia Bodi ilipokea taarifa ya Ofisa Usalama wa mchezo ambayo imeainisha matukio kadhaa yaliyoambatana na tukio hilo la klabu ya Simba kushindwa kufanya mazoezi, na kwamba baadhi ya matukio yanahitaji chunguzi ambao hauwezi kukamilika kwa wakati, Bodi ya Ligi kupitia Kamati yake ya Undeshaji na Usimamizi wa Ligi imeamua kuahirisha mchezo tajwa hapo juu kwa mujibu wa Kanuni ya 34:1 (1.3) ya Ligi Kuu kuhusu Kuahirisha Mchezo, ili kutoa nafasi ya kupata taarifa zaidi zitakazosaidia kufanya maamuzi ya haki. Bodi itatoa taarifa kamili,” imesema TPLB.

Ikiwa itabainika maofisa wa usalama wa Yanga walihusika kuizuia Simba kufanya mazoezi, kanuni ya 47 (1) inafafanua adhabu ambayo inaweza kupata.

“Klabu ina wajibu na jukumu la kuhakikisha kuwa wachezaji, viongozi, wanachama na wapenzi wake wanajiheshimu na hawajihusishi na vitend vyovyote vya utovu wa nidhamu kama vile matusi, vitisho, vurugu, vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina na vitendo vyovyote vingine visivyokuwavya kimichezo kwenye viwanja vya michezo.

“Klabu ambayo mashabiki/wachezaji/viongozi wake watafanya vitendo hivyo itatozwa faini ya Sh5 milioni na kwa makosa ya kujirudia, faini itatozwa kati ya Sh10 milioni na Sh20 milioni,” inafafanua kanuni hiyo.

Ikiwa Simba itabainika imegomea mchezo, kanuni ya 47(6) inafafanua kuwa adhabu kubwa ni timu kushushwa daraja.

“Klabu itakayoshindwa kupeleka timu uwanjani baada ya kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mchezo kitatozwa faini ya Sh5 milioni na kushushwa daraja. Kiongozi aliyeshiriki kutopeleka timu uwanjani atafikishwa kwenye Kamati ya Nidhamu au Kamati ya Maadili ya TFF,” imefafanua kanuni hiyo.

Muda mfupi baada ya taarifa hiyo, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amesema kuwa kuwa timu hiyo itaenda uwanjani hapo kama ratiba ya awali ilivyoonyesha.

“Kikosi cha Yanga kitawasili uwanja wa Mkapa saa 11:00 jioni kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa leo wa Kariakoo Derby. Hakuna Kipengele,” ameandika Ally Kamwe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *