
Dar es Salaam. Yanga na Simba ndiyo wawakilishi pekee kutoka Tanzania waliosalia kwenye michuano ya Caf ngazi ya klabu msimu huu ambapo zote zimetinga hatua ya makundi.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Tanzania inawakilishwa na Yanga wakati Simba ikishiriki Kombe la Shirikish Afrika.
Hatua ya makundi ya michuano hiyo itaanza kuchezwa kesho Jumanne Novemba 26, 2024 na tamati yake inatarajiwa kuwa Januari 19, 2025.
Rekodi zinaonyesha kwamba, hii ni mara ya pili mfululizo kwa Yanga kucheza makundi ya michuano hiyo baada ya msimu uliopita kufika robo fainali na kuondoshwa kwa mikwaju ya penalti 3-2 dhidi ya Mamelodi Sundowns kutokana na timu hizo kufungana mechi mbili za nyumbani na ugenini.
Kabla ya hapo, Yanga ilicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023 na kupoteza kwa sheria ya bao la ugenini mbele ya USM Alger baada ya mchezo wa kwanza nyumbani Yanga kufungwa 2-1, ugenini ikashinda 1-0 na matokeo ya jumla kuwa 2-2.
Kwa upande wa Simba, imekuwa na mfululizo mzuri wa kufika angalau robo fainali katika michuano ya Caf ikifanya hivyo mara tano ndani ya misimu saba mfululizo kuanzia 2018/2019 hadi 2023/2024.
Katika robo fainali hizo, nne Ligi ya Mabingwa Afrika na moja Kombe la Shirikisho Afrika.
YANGA VS AL HILAL
Ikiwa imepangwa Kundi A katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga kesho Jumanne itakuwa mwenyeji wa Al Hilal kutoka Sudan, timu hizo zikipambana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni.
Huo utakuwa ni mtihani wa kwanza wa Kocha Sead Ramovic raia wa Ujerumani tangu akabidhiwe kikosi hicho Novemba 15 mwaka huu akichukua nafasi ya Miguel Gamondi ambaye msimu uliopita aliiwezesha Yanga kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo baada ya kupita takribani miaka 25, kisha akaipeleka hadi robo fainali. Msimu huu kabla hajaondoka, ameiwezesha Yanga kutinga tena makundi kwa msimu wa pili mfululizo akiwa kocha wa kwanza kufanya hivyo kikosini hapo.
Ramovic anakwenda kukabiliana na Al Hilal inayonolewa na Kocha Florent Ibenge ambaye rekodi zinaonyesha kutokuwa nzuri kwake anapokuja kucheza Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Rekodi zinaonyesha Ibenge amekuwa na kipindi kigumu na baadhi ya timu mbalimbali alizoziongoza kwenye michuano ya CAF akiwa kwa Mkapa.
Katika mechi nne alizokuja akiwa na timu za AS Vita Club (2018-2019 na 2020-2021), kisha 2021-2022 akiiongoza RS Berkane zote alipoteza akicheza dhidi ya Simba, huku 2022-2023 akiondoka na sare ya bao 1-1 dhidi ya Yanga.
Wakati rekodi za Ibenge kwa Mkapa zikiwa hivyo dhidi ya timu za Tanzania, kwa upande wa Yanga katika michuano ya Caf kwenye misimu miwili ya mwisho 2022-2023 na 2023-2024, imepoteza mchezo mmoja tu ambao ulikuwa wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger ya Algeria.
Katika msimu huo wa 2022-2023, Yanga ilipangwa Kundi D ambapo ilivuna pointi tisa nyumbani ikizifunga TP Mazembe ya DR Congo (3-1), Real Bamako ya Mali (2-0) na US Monastir ya Tunisia (2-0).
Baada ya hapo Yanga ikatinga robo fainali, haikupoteza nyumbani zaidi ya kupata matokeo ya 0-0 dhidi ya Rivers United ya Nigeria yaliyokuwa na faida kutokana na ugenini kushinda 2-0.
Nusu fainali tena nyumbani ikashinda 2-0 dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini na kuiondosha kwa jumla ya mabao 4-1 kufuatia ushindi pia wa ugenini 2-1.
Katika fainali, ndipo Yanga ikapoteza nyumbani 2-1 dhidi ya USM Alger ya Algeria, licha ya ugenini kushinda 1-0, haikutosha kubeba ubingwa.
Msimu uliopita ambao Yanga ilikuwa Ligi ya Mabingwa Afrika haikupoteza mchezo wowote nyumbani ikivuna pointi saba zilizotokana na kuzifunga CR Belouizdad (4-0) na Medeama (3-0), huku ikitoka sare ya 1-1 na Al Ahly.
Katika robo fainali, Yanga ikakutana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, nyumbani matokeo yalikuwa 0-0 kama ilivyokuwa ugenini lakini ikapoteza kwa penalti 3-2.
Mbali na hayo, rekodi zinaonyesha kwamba, Yanga na Al Hilal mara ya mwisho zilikutana Uwanja wa Benjamin Mkapa msimu wa 2022-2023 ukiwa ni mchezo wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika kusaka tiketi ya kutinga makundi.
Mechi hiyo iliyochezwa Oktoba 8, 2022, Yanga ilitoka sare ya kufungana bao 1-1, ikaenda ugenini ikafungwa 1-0 na kuangukia Kombe la Shirikisho ilipoenda hadi fainali.
Msimu huu Yanga imetinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kushinda mechi zote nne za mtoano ikifunga jumla ya mabao 17 huku yenyewe ikiwa haijaruhusu nyavu zake kuguswa.
Yanga ilianza kwa kuiondosha Vital’O ya Burundi kwa jumla ya mabao 10-0, kisha ikaichapa CBE SA ya Ethiopia jumla ya mabao 7-0.
Al Hilal yenyewe ilianza kuifunga Al Ahly Benghazi ya Libya jumla ya mabao 2-1, baadaye ikaitupa nje San Pedro ya Ivory Coast kwa jumla ya mabao 3-2.
Mchezo huu, hautokuwa rahisi kwa Yanga kwani Al Hilal ina rekodi nzuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo imecheza fainali mbili za mwaka 1987 na 1992, huku ikifika pia nusu fainali mara tano kuanzia mwaka 1966, 2007, 2009, 2011 na 2015.
Pia imecheza robo fainali mbili, mwaka 1988 na 1990 na kushiriki hatua ya makundi mara nane ikianza mwaka 2008, 2014, 2017, 2019-2020, 2020-2021, 2021-2022, 2022-2023 na 2024-2025 wakati Yanga ikitinga makundi mara tatu 1998, 2023-2024 na 2024-2025.
Katika ligi ya ndani, Yanga iliyocheza michezo 10, imeshinda minane na kupoteza miwili na pointi 24, ikifunga mabao 14 na kuruhusu manne.
Al Hilal inashiriki Ligi Kuu ya Mauritania baada ya nchini kwao Sudan ligi kusimama kutokana na changamoto ya kiusalama ambapo huko inaongoza baada ya michezo saba ikishinda mitano na sare mbili tu. Ikikusanya pointi 17, ikifunga mabao 15 na kuruhusu mawili.
Mbali na timu hizo, Kundi A la Ligi ya Mabingwa kuna TP Mazembe ya DR Congo na MC Alger ya Algeria.
Akizungumzia mchezo wao dhidi ya Yanga, Ibenge amesema: “Yanga ya sasa na tuliyokutana nayo mara ya mwisho ni vitu viwili tofauti kwa sababu imebadilika kiuchezaji na inajua namna mashabiki na viongozi wao wanataka kutokana na malengo yao, itakuwa mechi nzuri na ya kusisimua kwa pande zote.”
SIMBA VS BRAVOS
Fadlu Davids baada ya kuvuka mtihani wa kwanza wa kuiongoza Simba kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kutokana na kuitupa nje Al Ahli Tripoli ya Libya kwa jumla ya mabao 3-1, kazi iliyobaki ni kufanya vizuri kufika mbali zaidi.
Katika kuanzia safari ya makundi, Simba itaikaribisha Bravos do Maquis ya Angola, mchezo ukipigwa keshokutwa Jumatano kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, saa 10 jioni.
Hii ni mara ya sita Simba inacheza hatua ya makundi katika michuano ya Caf ndani ya misimu nane mfululizo tangu 2018/2019 hadi 2024/2025. Mara zote hizo ilipotinga makundi, imeishia robo fainali ambapo ilikuwa 2018/2019, 2020/2021, 2022/2023 na 2023/2024 upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika na moja Kombe la Shirikisho msimu wa 2021/2022, huku misimu miwili ya 2019/2020 na 2021/2022 ikishindwa kufika makundi. Msimu huu itakuwaje?
Kocha Mkuu wa Bravos, Mario Soares, amesema wanapaswa kujiandaa vyema na mchezo dhidi ya Simba baada ya kuishuhudia timu yake ikiwa haina mwenendo usioridhisha katika Ligi Kuu ya Angola ambapo imecheza michezo 12 ikikusanya pointi 16 nafasi ya tano baada ya kushinda mitatu, sare saba na kupoteza miwili, ikifunga mabao 11 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 10, jambo linaloonyesha wazi haipo vizuri maeneo mawili ya ushambuliaji na uzuiaji, kitu kinachoweza kuipa faida Simba itakapokutana nayo.
Hata hivyo, rekodi ya mechi tano za mwisho za ligi, Bravos imeshinda moja, sare tatu na kupoteza moja, wakati Simba ikishinda zote tena bila ya kuruhusu bao.
Simba katika Ligi Kuu Bara inaongoza ikifikisha pointi 28 zilizotokana na kufunga mabao 22 na kuruhusu matatu pekee huku ikishinda mechi tisa, sare moja na kupoteza moja.
Ushindi wa mechi tano mfululizo za mwisho katika ligi kabla ya kucheza na Bravos, umewapa jeuri mastaa wa Simba ambapo beki wa kulia wa timu hiyo, Shomari Kapombe amesema hawana presha kubwa ingawa wanatakiwa kuwa makini ili waanze vizuri mechi za makundi.
“Unajua timu ikipata matokeo mazuri inajijenga kiushindani, tofauti na tulivyopoteza mchezo dhidi ya Yanga na kuambulia sare mbele ya Coastal Union na tulikuwa tunakosa utulivu na kutengeneza maelewano mazuri.
“Matokeo mazuri ya mechi tano mfululizo yametuondolea presha kwa mashabiki, sasa tunacheza kwa utulivu na kuelekea mchezo wetu wa kwanza hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika naamini tutakuwa kwenye ubora zaidi.
“Baada ya kumaliza mchezo wetu na Pamba sasa tunaelekeza akili zetu zote kimataifa mchezo ambao ni muhimu kwetu kuhakikisha tunapata matokeo mazuri kwenye uwanja wetu wa nyumbani, tutaingia kwenye mchezo huo tukiwa imara katika kuziwania pointi tatu,” alisema Kapombe.
Kocha Mkuu wa Bravos, Mario Soares, amesema: “Tuko katika kundi gumu kutokana na aina ya wapinzani tuliokuwa nao, ni kweli tumekuwa na mwenendo usioridhisha ila haya ni mashindano tofauti na hata namna ya uchezaji na maandalizi kwa ujumla yanabadilika, tunawaheshimu kila mmoja wetu.”
Akizungumzia ubora wa Simba msimu huu, Soares alisema timu hiyo ina wachezaji bora ambao wamekuwa wakicheza kitimu zaidi bila kujali mmoja mmoja, hivyo anaiheshimu kutokana na kiwango ilichojiwekea, hasa inaposhiriki michuano ya kimataifa.
“Siwezi kusema mchezaji mmoja mmoja kwa sababu ukiangalia wanacheza kwa umoja ndio maana wanaongoza Ligi Kuu, huu utakuwa mchezo mzuri na mgumu kwa kila upande, ingawa tunapaswa kuongeza umakini kuanzia uzuiaji na ushambuliaji pia,” alisema Soares.
Bravo inarejea tena Dar es Salaam msimu huu baada ya mchezo wa awali wa marudiano wa michuano hiyo kutoka suluhu na Coastal Union uliochezwa Agosti 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, hivyo kufuzu hatua inayofuatia kwa jumla ya mabao 3-0 kutokana na ushindi huo wa nyumbani. Pia ikaenda kuiondosha Saint Eloi Lupopo kwa jumla ya mabao 3-1 na kufuzu makundi.
Simba katika kundi lake mbali na Bravos, kuna CS Sfaxien ya Tunisia na CS Constantine kutoka Algeria.