Hii Dabi ya Dar ngonjeni tuone, kutokana na ukweli kwamba mashabiki wa soka wanajiuliza kwa sasa wakati wakiendelea kusubiri mchezo mkali na wa kusisimua wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga dhidi ya Azam FC, utakaopigwa leo Jumamosi kwenye Uwan-ja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Pambano hilo litakalopigwa kuanzia saa 12:00 jioni, linasubiriwa kwa hamu kutokana na kasi iliyoanza nayo Yanga msimu huu ya kugawa dozi kwa timu zote ilizokutana nazo katika Ligi Kuu na hata mechi za michuano mingine, huku Azam ikitazamwa kama timu inayoweza kupunguza kasi hiyo kama itashinda leo.
Mwanaspoti linakuletea rekodi za kushtua ambazo kama ni shabiki wa timu mojawapo kati ya hizo, hupaswi kabisa kwenda uwanjani na matokeo yako mfukoni.

Mchezo huu utakuwa ni wa kisasi kwa timu zote mbili kwani mara ya mwisho kwao kukutana ilikuwa fainali ya Ngao ya Jamii Agosti 11 mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambapo Azam FC ilikubali kichapo cha mabao 4-1.
Ushindi huo kwa Yanga ulikuwa wa kisasi kwani ma-ra ya mwisho katika Ligi Kuu Bara ilichapwa na Azam FC mabao 2-1, Machi 17 mwaka huu, yaliyo-fungwa na Gibril Sillah na Feisal Salum ‘Fei Toto’ hu-ku Clement Mzize akifunga la kufutia machozi.
Kichapo hicho ndicho kilichoipa Yanga hasira zaidi kwani tangu Machi 17, mwaka huu kikosi hicho cha Muargentina, Miguel Gamondi hakijawahi kupoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu Bara kuanzia msimu uliopita na huu, zaidi ya kushinda au kuambulia sare.
Tangu Machi 17 mwaka huu, Yanga imecheza jumla ya michezo 18 ya Ligi Kuu Bara na kati ya hiyo imeshinda 17 na kutoka sare mmoja tu wa (0-0) dhidi ya JKT Tanzania, mechi iliyopigwa Aprili 24 mwaka huu, kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.
Katika michezo hiyo 18 iliyocheza Yanga kwa kipindi hicho chote, imefunga jumla ya mabao 35, ikiwa na wastani mzuri wa kufunga mawili kwa kila mchezo, huku eneo la kujilinda likiwa limeruhusu nyavu zake kutikiswa matatu tu.

Upekee wa mchezo huu unatokana na rekodi za ti-mu hizi wakati zinakutana kwani Azam inapoifunga Yanga ni kama inaiongezea nguvu ya kufanya vizuri zaidi, kwa sababu hata mara ya mwisho ilipoifunga Machi 17, imeendeleza kiwango bora hadi sasa.
Pia, tangu mara ya mwisho Azam FC ilipoifunga Yanga kwa bao 1-0, Aprili 25, 2021, la mshambuliaji Mzimbabwe, Prince Dube dakika ya 86, kikosi hicho cha Gamondi kimecheza jumla ya michezo 50, ya Ligi Kuu Bara kikiwa nyumbani bila ya kupoteza.
Katika michezo 50 ya nyumbani, Yanga imeshinda 45 na kutoka sare mitano ambapo kikosi hicho ki-mefunga jumla ya mabao 117 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 18, huku mechi 36 kati ya hizo timu hiyo haijaruhusu bao lolote ‘Clean Sheets’.
Mashabiki wanasubiri kuona kama Azam FC itashinda kwa mabingwa hao watetezi ingawa rekodi zinaonyesha timu hiyo imekuwa pia na bahati mbaya pindi inapokutana na Yanga katika michezo ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Novemba tangu mwa-ka 2008.
Tangu miamba hii ilipoanza kukutana 2008, huu utakuwa ni mchezo wa tatu kuchezwa Novemba ambapo katika mara zote mbili Azam imechezea kichapo ikianza na (2-0) Novemba 7, 2012, kisha kuchapwa tena bao 1-0, mechi iliyopigwa Novemba 25, 2020.

Mchezo huu utakuwa ni wa 33 wa Ligi Kuu Bara kwa timu hizi kukutana tangu Azam FC ilipopanda rasmi Julai 27, 2008, baada ya kuifunga Majimaji ya Songea mabao 2-0, Uwanja wa Jamhuri Dodoma, ambapo Yanga imeshinda 13, sare tisa na kupoteza 10.
Katika michezo 32, ya Ligi Kuu Bara iliyopita baina yao tangu mwaka 2008, Yanga imefunga mabao 43, huku Azam FC ikifunga 40.
Tangu zimeanza kukutana ni michezo minne tu ili-yozalisha mabao mengi, matano (5) ambapo Azam FC imeshinda miwili ikianza na 3-2 Aprili 8, 2009 na (3-2) Septemba 23, 2013 huku Yanga ikishinda miwili pia (3-2), Desemba 25, 2022 na 3-2, Oktoba 23, 2023.
John Bocco anayeichezea JKT Tanzania kwa sasa akitokea Simba, ndiye mchezaji aliyeacha rekodi pale Azam FC kwa kuifunga Yanga mabao mengi, kwani hadi anaondoka Julai 2017, baada ya kui-chezea kwa miaka 10 alikuwa ameifunga mabao 10.
Bocco ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao mengi ya Ligi Kuu Bara akiwa amefunga 156, am-bapo ameyafunga katika timu tatu tofauti, akianza na Azam FC aliyoifungia 84, Simba akifunga 70, hu-ku JKT Tanzania anayoichezea hadi sasa akifunga mawili tu.
Tangu Azam FC imteuwe Mmorocco, Rachid Taoussi Septemba 7, mwaka huu akichukua nafasi ya Msen-egali, Yousouph Dabo, kocha huyo ameiongoza katika jumla ya michezo minane ya Ligi Kuu Bara ambapo ameshinda mitano, sare miwili na kupoteza mmoja.
Kiujumla Azam FC imecheza michezo tisa ya Ligi Kuu Bara msimu huu, ikishinda mitano, sare mitatu na kupoteza mmoja hadi sasa, huku mmoja aliouongoza Dabo kabla ya kutimuliwa Septemba 3, mwaka huu ulikuwa wa suluhu na JKT Tanzania Agosti 28, 2024.
Kwa upande wa Yanga msimu huu, imecheza michezo minane ya Ligi Kuu Bara ambapo imeshinda yote tena bila ya kuruhusu bao lolote.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imepenyezewa zinaele-za mwamuzi wa kati, Ahmed Arajiga kutoka Manyara ndiye aliyependekezwa na kamati ya waamuzi kwa ajili ya kutafsiri sheria 17 za mpira wa miguu, wakati miamba hiyo itakapokutana leo Jumamosi.