Yanga Princess imetwaa ubingwa wa michuano ya Samia Women’s Super Cup 2025 baada ya kuitandika JKT Queens mabao 3-0 kwenye mchezo wa fainali uliopigwa Uwanja wa Aga Khan uliopo Ngaramtoni jijini hapa.
Dakika 45 za kwanza zilianza kwa JKT Queens kutumia mfumo wao wa kawaida wa kucheza soka la pasi nyingi huku wakiwaruhusu Yanga kumiliki mpira wakati wao wakisubiri kushambulia kwa kushtukiza.
Hata hivyo, hali hiyo iliwapa ugumu kupenya ngome la Yanga pindi walipokuwa wakijaribu kushambulia na kuifanya mechi hiyo kumalizika dakika 45 ikiwa 0-0.
Kipindi cha pili, Yanga waliingia na nguvu na kujipatia bao la kwanza kupitia kwa Aragash Tadesse katika dakika ya 50 ya mchezo kwa shuti kali.

Bao ambalo lilionekana kuwavuruga JKT na kujikuta wakiruhusu bao la pili katika dakika ya 78 kupitia kwa Jeannine Mukandayisenga ambaye aliwazidi kasi mabeki wa JKT na kuuweka mpira kimiani.
Wakati mashabiki wakiamini kuwa mchezo huo uliohudhuriwa na viongozi wengi wa soka utamalizika hivyo, Mukandayisenga alifanya tena kazi kubwa na kuifungia Yanga bao la tatu na kuipa timu hiyo ubingwa huo ambao ni mara ya kwanza unawaniwa.
Katika mchezo wa mshindi wa tatu ambao ulipigwa mapema saa 8:00 mchana, Simba Queens iliichapa Fountain Gate Princess mabao 2-1.

Zawadi kwa washindi wa michuano hiyo itatolewa siku ya Jumamosi katika kilele cha sherehe za siku ya Wanawake duniani .