
YANGA Princess wiki iliyopita imetambulisha vyuma vitatu vya kimataifa lakini usajili ulioshtua zaidi ni ule wa nyota wazawa.
Dirisha hili dogo lililofungwa Januari 15, Yanga ilitambulisha nyota watatu wa kimataifa ambao ni kiungo mkabaji, Lydia Akoth kutoka Kenya Police Bullets, kiungo mshambuliaji Aregash Kalsa kutoka C.B.E ya Ethiopia, Jeaninne Mukandayisenga wa Rayon Soprts ya Rwanda.
Ukiachana na wachezaji hao, awali timu hiyo ilitambulisha nyota watatu wazawa, mabeki Diana Mnally na Protasia Mbunda na kipa Zubeda Mgunda.
Ni miongoni mwa sajili zilizotikisa kwenye ligi ya wanawake kutokana na ubora wa wachezaji hao ambao ni wazoefu kwa Mnally na Mgunda ambao wote waliwahi kucheza Simba na kubeba mataji ya ndani na lile la CECAFA 2022.
Mmoja wa kiongozi wa Yanga (hakutaka kutajwa jina) alisema sababu ya msimu huu kusajili wachezaji wazawa ni pamoja na kuingiza nyota hao kwenye kikosi cha timu ya taifa ‘Twiga Stars’.
“Muda mrefu timu yetu haijapeleka wachezaji timu ya taifa ‘Twiga Stars’ na kwa matakwa ya Kocha Edna Lema alitaka wachezaji hao tukaona pia wanaweza kusaidia timu yetu,” alisema kiongozi huyo.
Hadi sasa nyota hao wameshacheza mechi mbili za ligi wakionyesha kiwango bora hasa kwa kipa Mgunda ambaye mechi ya pili mfululizo anamuweka benchi Mnigeria, Rita Akarekor.
Msimu huu hadi sasa Yanga ilisajili wazawa Agnes Pallangyo, Wema Maile, Silvia Mwasha, Mgunda, Mbunda na Mnally.