Yanga na nuksi ya mechi ya kwanza makundi

Matokeo ya kufungwa mabao 2-0 nyumbani kutoka kwa Al Hilal kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, yameendeleza mkosi ambao Yanga imekuwa nao kwenye mechi za mwanzo za hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika.

Mabao ya Adama Coulibaly katika dakika ya 63 na Yasir Mozamil katika dakika ya 90 ya mechi ya leo, yameifanya  Yanga kutowahi kupata ushindi kwenye hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika, mara zote sita ambazo imewahi kushiriki.

Mara ya kwanza kwa Yanga kushiriki hatua hiyo ilikuwa ni mwaka 1998 ilipotinga katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo mechi ya kwanza, Yanga ilitoka sare ya bao 1-1 nyumbani na Manning Rangers ya Afrika Kusini.

Mwaka huo, Yanga ilimaliza ikiwa ya mwisho kwenye kundi lake ikikusanya pointi mbili.

Yanga ilisubiri tena hadi 2016 ilipoingia katika hatua ya makundi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika na mchezo wa kwanza ilipoteza kwa bao 1-0 ugenini dhidi ya MO Bejaia ya Algeria na mwaka huo ilimaliza ikiwa nafasi ya mwisho na pointi nne.

Mwaka 2018 ikatinga tena hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho na mchezo wa kwanza ikapoteza kwa mabao 4-0 ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria.

Yanga ilimaliza ikiwa na pointi nne na kuishia hatua ya makundi.

Mara ya nne ilikuwa ni msimu wa 2022/2023 ilipofanikiwa kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo mechi ya kwanza ilifungwa mabao 2-0 na Monastir ya Tunisia ingawa msimu huu ilifika hadi fainali ya mashindano hayo.

Msimu uliopita, Yanga ilianza vibaya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa mabao 3-0 na CR Belouizdad ya Algeria lakini hata hivyo ilipambana hadi kufika hatua ya robo fainali