Kuna msemo wa kiandamizi kwenye ulimwengu wa idara ya ufundi kwenye soka kwamba makocha huajiriwa ili wafukuzwe.
Huu ni msemo maarufu duniani kote kwa sababu matokeo yanapoenda vibaya tu, mtu wa kwanza kutupiwa lawama huwa ni kocha na kinachofuata baada ya lawama ni kutupiwa virago.
Lakini kwa Tanzania kufukuza makocha hakutokani tu na matokeo mabaya, bali ni fasheni.
Ijumaa ya Novemba 15, Yanga ilitangaza kumtimua kocha wake, Miguel Gamondi.
Ukiangalia rekodi za kocha huyo raia wa Argentina tangu aichukue Yanga, huwezi kuamini kwamba amefukuzwa kwa sababu ya matokeo bali fasheni.
Kwa takribani miaka mitano iliyopita, klabu ya Yanga ilikuwa na utulivu kidogo katika hii fasheni ya fukuza fukuza makocha, tofauti na wakubwa wenzake, Simba na Azam FC.
Tangu afukuzwe Zlatko Krmpotic kutoka Serbia mwaka 2021 na nafasi yake kuchukuliwa na Nasreddine Nabi, Yanga haikufukuza kocha hadi Miguel Gamondi.
Kwa watu waliozoea fukuza fukuza, hiki kilikuwa kipindi cha mateso makubwa.
Kwa hiyo ni lazima wakubwa wali’miss’ kutimua mtu, ikaangukia kwa Gamondi.
Raia huyo wa Argentina anakuwa kocha wa 13 kutimuliwa na Yanga tangu 2012 na kuifanya klabu hiyo iwe imetimua makocha wengi kuliko mataji ambayo imepata katika kipindi hicho.
Ukurasa huu unakuletea makocha wote 13 waliotimuliwa na Yanga tangu 2010.
Kostadin Papic (2010) – Serbia
Alijiunga na Yanga mwaka 2008, akichukua mikoba ya Dusan Kondic. Alijiuzulu 2011 akipinga kitendo cha uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti Imani Madega kumteua Fred Felix Minziro kuwa kocha msaidizi bila yeye kushirikishwa.
Sam Timbe (2011) – Uganda
Alijiunga na Yanga 2011 kuchukua nafasi ya Papic na akaiwezesha kushinda ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Kagame, mara zote kwa kuipiku Simba.
Kwa mataji hayo mawili, Timbe alibatizwa jina la kocha wa mataji lakini alifukuzwa miezi minane baadaye kufuatia matokeo mabaya.
Kostadin Papic (2011) – Serbia
Kuondoka kwa Timbe kukamrejesha Papic Jangwani, kuendelea kukinoa kikosi cha wananchi.
Hata hivyo, ukazuka mgogoro mkubwa wa kiuongozi ulioanza kwa kujiuzulu kwa Makamu Mwenyekiti Davies Mosha.
Kilele cha mgogoro huo ni kichapo cha 5-0 kutoka Simba na mwisho wa msimu Yanga ilishika nafasi ya 3. Papic akafukuzwa.

Tom Saintfiet
Tom Saintfiet (2012) – Ubelgiji
Kuondoka kwa Papic kukatoa nafasi kwa Tom Saintfiet aliyefahamika zaidi kama mtakatifu Tom.
Mechi ya kwanza alishuhudia kichapo cha 2-0 kutoka kwa Atletico Olympic ya Burundi kwenye Kombe la Kagame.
Timu hiyo ilikuwa ikifundishwa na Cedrick Kaze, ambaye alikaribia kutua Yanga kabla ya Krmpotic, na sasa anatajwa tena kwamba huenda akakamilisha dili.
Saintfiet akaiongoza Yanga kushinda Kombe la Kagame lakini sare ya 0-0 na Tanzania Prisons kule Mbeya na kipigo cha 3-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar, kikamgombanisha na bosi wake Yusuf Manji kiasi cha kutishiana bastola, na hatimaye akafukuzwa.
Ernie Brandts ( 2012-13) – Uholanzi
Shujaa wa Uholanzi wa Kombe la Dunia 1978, Ernie Brandts, akafuatia kubeba kikombe cha machungu cha Jangwani.
Akaanza kwa kichapo kutoka kwa Kagera Sugar lakini gari likawaka hadi akachukua ubingwa wa ligi kuu 2012/13.
Sare ya 3-3 dhidi ya Simba, timu yake ikiruhusu uongozi wa 3-0 hadi mapumziko, kupotea ilimtia doa na safari yake ikakamilika kufuatia kichapo cha 3-1 kutoka Simba kwenye mechi ya bonanza la Mtani Jembe.
Hans Van Pluijm ( 2014) – Uholanzi
Alianza kazi Januari 2014 akiipokea timu iliyokuwa ikiongoza ligi kwa alama moja juu ya Azam FC.
Lakini kibao mwisho wa msimu Yanga ikaukosa ubingwa kwa Azam FC na mwenyekiti Manji hakufurahishwa.
Japo mambo yalifichwa kisiasa, lakini Hans alitimuliwa, yeye na msaidizi wake Mkwasa, na kukimbilia Uarabuni.

Marcio Maximo
Marcio Maximo (2014) – Brazil
Kocha huyo wa zamani wa Taifa Stars alishatajwa kujiunga na Yanga tangu 2012 kabla ya kiza kinene kutanda na msala kumuangukia mtangazaji na mchambuzi mmoja nchini, kwamba alimtisha kocha huyo eti Yanga hakukuwa salama kwake.
Safari hii akaja kuchukua mikoba ha Hans na akaanza vibaya kwa kuogopa kushiriki mashindano ya Kombe la Kagame nchini Rwanda.
Maximo alitaka kupeleka kikosi cha vijana lakini CECAFA wakasema hayo ni mashindano ya wakubwa (senior teams).
Ushindi wa 3-0 dhidi ya Azam FC kwenye Ngao ya Jamii ulionekana mwanzo mzuri kwake lakini ilipoanza ligi hali ilikuwa mbaya.
Alianza kwa kichapo cha 1-0 kutoka Mtibwa Sugar na safari yake ikahitimishwa na kichapo cha 2-0 mbele ya Simba kwenye Mtani Jembe.
Hans Van Pluijm ( 2015-16) – Uholanzi
Hans van Pluijm akarejea Yanga na kuisaidia kushinda ngao ya jamii, ligi kuu na ubingwa wa kwanza wa mahindano mapya ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports.
Pia aliiwezesha Yanga kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Afrika.
Hata hivyo, mwanzo wa kusuasua kwenye ligi ya 2016/17 kukamponza na kuondolewa kwenye nafasi yake.
Akageuzwa kuwa mkurugenzi wa ufundi na nafasi yake ya ukocha kuchukuliwa na George Lwandamina.
Mbinu kama hii Yanga waliitumia 2007 kwa Jack Lloyd Chamangwana (marehemu) ili ampishe kocha mpya Milutin Micho.
Hans akawa mkurugenzi wa ufundi kwa muda mfupi, halafu akaacha kazi yeye mwenyewe na kwenda kuwa kocha mkuu wa Singida United.

George Lwandamina (2016 – 2018) – Zambia
Akitoka kuiongoza Zesco kufika nusu fainali ya ligi ya Mabingwa Afrika, Lwandamina maarufu kama Chicken, aliisaidia Yanga kushinda ubingwa wa ligi kuu 2016/17 na kufika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Afrika.
Hata hivyo, kipindi chake kilikumbwa na ukata mkubwa kufuatia mwenyekiti Manji kujiuzulu.
Lwandamina maisha yakamshinda, akabwaga manyanga 2018
Mwinyi Zahera (2018 – 2020) – DRC
Nafasi ya Lwandamina ikajazwa na Mwinyi Zahera.
Kocha huyu mwenye maneno mengi, akaisaidia Yanga nafasi ya pili kwenye ligi katika moja ya misimu mibaya zaidi kiuchumi klabuni hapo.
Kwa nafasi hiyo, Zahera alionekana shujaa lakini neema ilipokuja msimu uliofuata, matokeo hayakupatikana na uongozi wa Dkt. Mshindo Msolla ukamtimulia mbali.

Luc Eymel
Luc Eymel (2020) – Ubelgiji
Luc Eymel alianza kwa kichapo cha 3-0 nyumbani kutoka kwa Kagera Sugar.
Kichapo cha 4-1 kutoka Azam kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports na matokeo ya kusuasua kwenye mechi za mwisho mwisho za msimu, vilimtia mihemko uliomsababishia kutoa kauli zilizotafsiriwa kuwa ni za kibaguzi, akaliwa kichwa.
Zlatko Krmpotic (2020) – Serbia
Ndipo akatajwa Zlatko Krmpotic kuliongoza bench la ufundi la Yanga kuelekea kuanza kwa msimu mpya wa VPL.
Ujio wake wa kuchelewa ulisababisha timu kuanza kwa sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons kabla ya ushindi mfululizo hadi anafukuzwa.
Sababu za kufukuzwa kwake ni aina mbaya ya mpira ambao Yanga inacheza chini yake.
Miguel Gamondi (2024) – Argentina
Alijiunga na Yanga mwaka 2023 akirithi mikoba ya Nabi aliyeondoka mwenyewe baada ya kupata mafanikio makubwa Jangwani.
Gamondi tayari ana heshima kubwa sana akiwa na Yanga baada ya kutwaa makombe makubwa msimu uliopita likiwemo la Ligi Kuu Bara, pamoja na CRDB Federation.
Amefukuzwa mwaka 2024 kwa sababu mbalimbali vikiwemo vichapo viwili dhidi ya Azam FC na Tabora United.
Makala hii imeandikwa na Mzee wa Fact.