Yanga kutangaza utalii kupitia ‘Visit Zanzibar’

Katika juhudi za kuimarisha utalii wa ndani na kikanda, Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZCT) imeingia ushirikiano na klabu ya Yanga wakisaini mkataba wa kutangaza vivutio vya Zanzibar kupitia kauli mbiu ya ‘Visit Zanzibar’.

Mkataba huo ulisainiwa Machi 28, 2025 na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Arif Abbas pamoja na Rais wa Yanga, Hersi Said mbele ya Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Soraga.

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, Abbas amesema kupitia Visit Zanzibar kwenye jezi za Yanga, Zanzibar itanufaika kwa kufikia soko la kutangaza utalii wa ndani, kikanda na Bara la Afrika kutokana na umaarufu wa timu hiyo na wachezaji wake kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.

Naye Hersi amesema klabu hiyo kwa kushirikiana na Kamisheni ya Utalii Zanzibar kwa msimu mzima wa 2025/2026, nembo ya Visit Zanzibar itawekwa kwenye jezi rasmi za Yanga kwa mashindano yote.

“Pia tumejipanga kutoa elimu na hamasa kwa Watanzania kutembelea vivutio vya nyumbani. Hakuna sababu ya kwenda Ibiza au Dubai ilhali tunayo Zanzibar,” amesema.

Waziri Soraga kwa upande wake ameipongeza Yanga kwa hatua hiyo ya kizalendo kushiriki katika juhudi za kuutangaza utalii wa Zanzibar.

Amesisitiza kuwa sekta ya utalii inakabiliwa na ushindani mkali kutoka visiwa jirani, hivyo juhudi za ziada kama hizo ni muhimu katika kuhakikisha Zanzibar inaendelea kuwa kivutio cha kipekee.

Ushirikiano huu ni hatua ya kimkakati inayolenga kutumia nguvu ya michezo katika kuitangaza Zanzibar kimataifa, huku ukichochea pia utalii wa ndani kwa kuhamasisha jamii kutembelea maeneo ya kihistoria na vivutio vya asili vya visiwa hivi viwili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *