Yanga kunogesha uzinduzi uwanja mpya wa Singida BS

Dar es Salaam. Leo ni siku ya kihistoria kwa wapenda soka wa Mkoa wa Singida na Tanzania kwa ujumla, wakati klabu ya Singida Black Stars inazindua rasmi uwanja wake mpya kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Yanga.

Wachezaji wa Singida Black Stars wanaotegemewa kung’ara kwenye mchezo huu ni pamoja na mshambuliaji wao hatari, Jonathan Sowah ambaye ameonyesha kiwango bora katika michezo ya hivi karibuni kwa kufunga mabao saba na ndiye gumzo kwa mashabiki mkoani hapa.

Kwa upande wa Yanga SC, pamoja na baadhi ya nyota wao kuwa na majukumu ya timu za taifa, bado wana kikosi imara chenye uwezo wa kupata matokeo chanya, wakiwemo mastaa Pacome Zouazoa, Aziz Ki pamoja na Yao Kouassi ambao wanatarajia kunogesha uzinduzi huo leo.

Uwanja huo uliopo Mtipa mkoani Singida, umejengwa kwa viwango vya kisasa ukiwa na nyasi bandia kwa kushirikiana na wadhamini mbalimbali ukiwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 7,000.

Sherehe za uzinduzi zinatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na michezo, huku mgeni rasmi akiwa Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA.

Burudani mbalimbali zimetayarishwa kabla ya mechi kuu, ikiwa ni pamoja na muziki kutoka kwa wasanii maarufu wa Bongo Fleva, michezo ya asili, na maonesho ya utamaduni. Mashabiki watapata fursa ya kushuhudia historia ikiandikwa kwa mara ya kwanza mkoani hapa.

Kilele cha tukio hili kitakuwa ni mchezo wa kirafiki kati ya wenyeji Singida Black Stars na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC utakaochezwa kuanzia saa 10 jioni.

 Mechi hii inatajwa kuwa ya kuvutia kutokana na nafasi za timu hizi katika msimamo wa ligi, ambapo Yanga wanaongoza kwa pointi 58 huku Singida Black Stars wakiwa nafasi ya nne na pointi 44.

Licha ya kuwa mechi ya kirafiki, upinzani baina ya timu hizi mbili umeibua hamasa kubwa kwa mashabiki. Singida Black Stars wanataka kutumia uwanja wao mpya kuonyesha ubabe wao, huku Yanga wakitaka kuendeleza rekodi yao nzuri dhidi ya wapinzani wao.

Hata hivyo, mechi hii inachezwa kipindi ambacho baadhi ya wachezaji wapo katika majukumu ya timu zao za taifa kwa mujibu wa kalenda ya FIFA.

Hii inamaanisha kuwa vikosi vya pande zote viwili vitakuwa na mabadiliko, jambo linaloweza kuleta mtazamo mpya wa kiufundi kwa benchi za ufundi.

Kocha wa Singida Black Stars, David Ouma alisema licha ya kuwakosa baadhi ya nyota wake wa kikosi cha kwanza, amewaandaa wachezaji waliopo kikamilifu kwa mchezo huu.

“Huu ni uwanja wetu mpya, tunataka kuuanza kwa ushindi ili kutoa heshima kwa mashabiki wetu na wadhamini waliotuunga mkono,” alisema.

Kwa upande wa Yanga SC, Miloud Hamdi alisema huu ni mchezo wa maandalizi kuelekea hatua ya mwisho ya ligi, lakini pia ni fursa kwa wachezaji wengine kuonyesha uwezo wao.

“Hatutaki kupoteza mchezo huu hata kama ni wa kirafiki. Tutapambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” alisema.

Katika michezo miwili ambayo timu hizo zimekutana kwenye Ligi Kuu, Yanga imefanikiwa kushinda yote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *