Yanga kuna kazi nzito, saba kufumua kikosi 2025/26

YANGA inafanya mambo yake ya usajili kimyakimya kwa ajili ya msimu ujao, hiyo ni baada ya kujihakikishia mapema tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na kwa sasa kuongoza msimamo wa ligi na mapema tu imeanza kuboresha kikosi chake.

Timu hiyo yenye uhakika wa kumaliza nafasi mbili za juu Ligi Kuu Bara msimu huu, katika maboresho hayo ya kikosi imeanza mazungumzo na wachezaji wanaomaliza mikataba, pia wale inaowahitaji kuwasajili.

Kama mambo yatakwenda vile ambavyo inazungumzwa kwa sasa, ni wazi kuna nyota saba wataondoka mwishoni mwa msimu huu wakiwemo watatu wanaounda kikosi cha kwanza.

Wachezaji wanaounda kikosi cha kwanza cha Yanga ambao huenda wakaondoka mwishoni mwa msimu huu ni kipa Djigui Diarra, kiungo mkabaji Khalid Aucho na kiungo mshambuliaji Stephane Aziz Ki.

Wengine ni Kennedy Musonda, Clatous Chama, Jonathan Ikangalombo na Yao Kouassi Attohoula.

Mchakato wa kujaza nafasi za wanaoondoka umeanza na Yanga kwa sasa ipo kwenye mazungumzo na kiungo mshambuliaji wa Singida Black Stars, Josaphat Arthur Bada (22) sambamba na kiungo wa Asec Mimosas, Koimizo Maiga (24).

Chanzo cha kuaminika kutoka Yanga kimeliambia Mwanaspoti uongozi wa timu hiyo tayari umeanza kufanya mchakato wa usajili wa msimu ujao huku Bada akiwa mmoja wa nyota wanaohitajika kikosini hapo.

Bada mwenye mabao matatu na asisti nane msimu huu, ameanza mazungumzo na Yanga ya kujiunga nayo msimu ujao.

Mbali na Bada, pia mshambuliaji wa Singida Black Stars, Jonathan Sowah naye yupo kwenye rada za mabingwa hao watetezi.

“Ni kweli mazungumzo ya kunasa saini ya kiungo huyo yameanza na yapo katika hatua nzuri, nafikiri kama mambo yataenda sawa atakuwa sehemu ya kikosi chetu msimu ujao kama mchezaji wa ndani baada ya kubadili uraia,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza.

“Tumezingatia mambo mengi kutamani kuwa na mchezaji huyo, ni moja ya wachezaji walioonyesha uwezo mkubwa kwenye ligi yetu, pia tunaamini anaweza kuongeza nguvu kwenye kikosi chetu kutokana na aina yake ya uchezaji,” alisema mtoa taarifa huyo.

Bada anamudu kucheza namba nane na 10, kutua kwake ndani ya kikosi hicho itakuwa sehemu ya kuwa mbadala wa Stephane Aziz Ki ambaye anatajwa kuondoka mwishoni mwa msimu.

Pia ataongeza kasi ya kuwania namba kikosini kama timu hiyo itafanikiwa kumbakiza Pacome Zouzoua ambaye anacheza eneo hilo akiwa amefunga mabao manane na asisti tisa akihusika kwenye mabao 17 kati ya 68 yaliyofungwa na timu hiyo.

Kwa upande wa Koimizo Maiga anayecheza eneo la kiungo mkabaji, anatajwa kwenda kuchukua nafasi ya Khalid Aucho.

Kwa mujibu ya mkataba wa Aucho ambao aliongeza mwaka mmoja msimu uliopita, mwisho wa msimu huu unamalizika na haijafahamika kama kuna mazungumzo yoyote kwa pande zote mbili huku taarifa zikibainisha hatakuwa na kikosi hicho msimu ujao.

“Hakuna mchezaji mbaya ambaye tumemtoa Asec Mimosas, ukiangalia ni timu yenye vipaji vikubwa, si unaona Pacome (Zouzoua), Aziz Ki (Stephane) na Yao (Kouassi Attohoula), hivyo ni suala la muda tu kumalizana naye na kila mmoja atamuimba.

“Kiungo mkabaji tangu ametua Aucho ambaye analituliza eneo hilo akicheza kwa ubora tumekuwa tukibahatisha kupata mchezaji mwingine bora wa kumpa changamoto, lakini kwa huyu wa Asec tunaamini ataleta kitu cha tofauti.”

Kiungo huyo ni zao la Saint-Etienne ya Ufaransa, kama akitua Yanga atakuwa ni mchezaji wa nne kutoka Asec baada ya Stephane Aziz Ki, Yao Kouassi Attohoula na Pacome Zouzoua.

Mabingwa hao watetezi pia wanatajwa kumrejesha aliyekuwa kiungo wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ anayecheza Azam ambaye ni kinara wa asisti Ligi Kuu Bara msimu huu akiwa nazo 13 na mabao manne.

Yanga pia inatajwa kuwa kwenye mazungumzo na beki wa zamani wa Simba ambaye sasa anakipiga AS FAR Rabat ya Morocco, Henock Inonga na kiungo mshambuliaji raia wa Kenya, Mohammed Omar Ali Bajaber.

Kigogo mmoja wa Yanga ameliambia Mwanaspoti, mazungumzo na baadhi ya wachezaji wanaohusishwa nao yanaendelea kwani wapo wenye mikataba na timu zao hivyo ni suala la makubaliano na waajiri wao huku wengine ambao wapo huru mazungumzo yapo kwenye hatua nzuri.

HALI ILIVYO

Kuna nyota saba wa kimataifa wanaotajwa kuondoka mwishoni mwa msimu huu. Wanaotajwa huenda wakaondolewa ni Yao Kouassi Attohoula, Khalid Aucho, Kennedy Musonda na Clatous Chama ambao mikataba yao inafikia ukingoni. Mwingine ni Jonathan Ikangalombo aliyetua kikosini hapo dirisha dogo la usajili msimu huu.

Mbali na wanaomaliza mikataba yao, pia inaelezwa Aziz Ki amepata dili, hivyo atauzwa mwisho wa msimu huu kama ilivyo kwa kipa Djigui Diarra raia wa Mali ambaye mbadala wake anatajwa kuwa ni Amas Obasogie anayecheza Singida Black Stars.

“Sababu kubwa ya kufikiria kuachana na Aucho ni majeraha ya mara kwa mara na uwepo wa Duke Abuya ambaye kwa sasa anafanya vizuri eneo hilo,” kilisema chanzo hicho.

Abuya mwenye uwezo wa kucheza nafasi zote za kiungo kwa sasa amekuwa akitumika zaidi chini akisaidiana na Mudathir Yahya ambaye hapo awali walikuwa wanacheza na Aucho.

Nyota wengine wenye uwezo wa kucheza kiungo mkabaji ni wazawa Salum Abubakar ‘Sureboy’, Jonas Mkude na Aziz Andambwile.

Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amezungumzia mikakati ya usajili ndani ya timu hiyo akisema: “Wachezaji bora wengi lazima uanze kuwatafuta mapema, kama mchezaji yupo huru maana yake mkataba wake unaelekea kumalizika na yule mwenye mkataba mazungumzo na klabu yake yanaanza kipindi hiki.

“Tumeanza kuboresha timu yetu kwa ajili ya msimu ujao, maboresho ya kwanza ni kubakisha nyota tulionao kwa mujibu wa ripoti ya mwalimu, wale ambao watataka kuondoka, tutaangalia kwa maslahi ya klabu nani tumuondoe, lakini malengo makubwa ni kutengeneza timu ya msimu ujao kwa sababu tayari tuna tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa,” alisema Kamwe.

Hivi karibuni, Mwanaspoti lilikuhabarisha kwamba Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi amewasilisha ripoti inayohitaji kuboresha maeneo manne ya kikosi hicho ambayo ni mshambuliaji wa mwisho, namba 10, beki wa kati na kiungo mkabaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *