Yanga kileleni baada ya siku 86 ikiichapa Kagera Sugar

Dar es Salaam. Baada ya kutokaa kileleni mwa msimamo wa ligi tangu Novemba 7, 2024, Yanga imerudi katika nafasi hiyo baada ya leo kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa KMC, Complex, Dar es Salaam.

Ushindi huo umeifanya Yanga ifikishe pointi 42 na kuipiku Simba ambayo ina pointi 40.

Yanga ililazimika kusubiri hadi  dakika ya 32 kupata bao la kuongoza kupitia kwa Clement Mzize ambaye alikwamisha shuti kali nyavuni  kwa mguu wa kulia akipokea pasi kutoka kwa Stephane Aziz Ki.

Baada ya Yanga kupata bao la kuongoza, iliendeleza mashambulizi langoni mwa Kagera Sugar na dakika ya 35 ilifanya shambulizi lililozaa penalti baada ya kiungo wake Mudathir Yahya kuangushwa ndani ya eneo la hatari la Kagera Sugar na Hija Shamte lililomfanya refa Nassor Mwinchui kuamua mkwaju wa penalti.

Penalti hiyo iliyopigwa na Stephane Aziz Ki ilipanguliwa vyema na kipa wa Kagera Sugar, Ramadhan Chalamanda.

Hii ni mara ya pili kwa kiungo huyo kukosa penalti katika ligi msimu huu, mara ya kwanza akifanya hivyo Novemba 7, 2024 dhidi ya Tabora United ambapo timu yake iliambulia kichapo cha mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Mwanzoni mwa kipindi cha pili, kocha wa Yanga, Sead Ramovic alifanya mabadiliko akimtoa Israel Mwenda aliyekuwa akichezeshwa winga, nafasi yake akichukua Pacome Zouzoua.

Kuingia kwa Pacome, kuliifanya Yanga iongeze mashambulizi ambayo yalikuja kuzaa matunda katika dakika ya 60 baada ya Mudathir Yahya kufunga bao la pili akiwa eneo la hatari la Kagera Sugar akimalizia pasi ya Prince Dube, kisha Pacome akaongeza bao la tatu dakika ya 78 kwa mkwaju wa penalti ulitokana na Maxi Nzengeli kufanyiwa faulo katika eneo la hatari.

Maxi alifanikiwa kutengeneza bao la nne lililofungwa na Kennedy Musonda kwa kichwa katika dakika ya 87 baada ya kuanzishiana kona fupi kati yake na Kibwana Shomari.

Hadi filimbi ya kumaliza mchezo inapulizwa, Yanga ilitoka kifua mbele kwa ushindi huo.