
Timu mbili ambazo zimetinga fainali ya Samia Women’s Super Cup 2025 kitemi, Yanga Princess na JKT Queens, kesho zitatoa majibu ya ipi ilifanya maandalizi mazuri ya michuano hiyo wakati zitakapokutana kwenye Uwanja wa Aga Khan kuanzia saa 10:15 jioni.
Mechi hiyo itatanguliwa na mcheza wa kuwania mshindi wa tatu kati ya Simba Queens na Fountain Gate Princess utakaoanza saa 8:00 mchana.
Yanga iliingia fainali baada ya kupata ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Fountain Gate Princess katika mechi ya nusu fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, wakati JKT Queens iliichapa Simba Queens bao 1-0 katika mechi hizo zilizochezwa jana, Jumanne, Machi 4, katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Ni kama historia imejirudia kwa timu hizo kukutana kwenye mchezo wa fainali kwani mara ya mwisho kukutana katika hatua kama hiyo ilikuwa ni Oktoba 5,2024 katika mchezo wa Ngao ya Jamii ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Dar es Salaam na JKT Queens kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Lakini, mara ya mwisho kukutana timu hizo ilikuwa ni Desemba 17, 2024 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake ambapo JKT Queens iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Donisia Minja katika dakika za 30 na 85.
Mchezo huo unatazamiwa kuwa mgumu kwa sababu kila timu inalitaka kombe hilo, Yanga Princess ikitaka la pili tangu kuanzishwa kwa timu hiyo miaka 10 iliyopita.
Mara ya mwisho kutwaa ubingwa ilikuwa ni Oktoba 17,2018 ilipotwaa ubingwa wa mashindano ya Ligi Daraja la kwanza kwa kuichapa Tanzanite Queens ya Arusha mabao 2-1.
Huku JKT Queens ikihitaji kombe la pili msimu huu baada ya lile la Ngao ya Jamii walilochukua mbele ya Yanga na kuendeleza rekodi ya kuwa timu yenye makombe mengi nchini.
Mabadiliko ambayo Yanga Princess ilifanya kwenye usajili wa dirisha dogo na ubora walionao kwa sasa unamfanya kocha wa timu hiyo, Edna Lema kuweka wazi kuwa anaamini ushindi utapatikana mbele ya JKT.
Amesema mchezo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani wao, lakini tayari amewasoma na kujua udhaifu wao upo sehemu gani, hivyo atautumia kupata ushindi.
Kocha wa JKT Queens, Esther Chaburuma amesema wachezaji wake wako salama na anaamini hakuna kitakachoshindikana kuibuka na ushindi upande wao.
“Fainali siku zote inakuwa ngumu kikubwa ni maandalizi kuelekea kwenye mchezo huo, jinsi gani wachezaji wangu watapokea yale maelekezo na kwenda kufanyia kazi uwanjani,” amesema Chaburuma.
Akizungumzia mchezo wa mshindi wa tatu dhidi ya Fountain Gate Princess, kocha wa Simba Queens, Yussif Basigi amesema wamejiandaa vyema kushinda licha ya malengo ambayo walikuja nayo Arusha kutibuliwa na kipigo kutoka wa JKT Queens.
Samia Women’s Super Cup itafikia tamati kesho, Alihamisi ambapo zawadi zitatolewa Jumamosi kwenye sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambazo zitafanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Michuano hiyo kwa mwaka huu imeshirikisha timu nne za Ligi Kuu ya Wanawake ambazo zinashika nafasi tatu za juu na moja ikiingia kama mwenyeji.
Timu hizo ni Simba Queens, JKT Queens, Yanga Princess na Fountain Gate Princess ambayo imeingia kama mwenyeji