MABOSI wa klabu ya Yanga, inadaiwa wameanza hesabu mapema za kutafuta mrithi wa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Stephaine Aziz KI anayetajwa huenda akaondoka mwishoni mwa msimu huu wa 2024/25 baada ya kuitumikia timu hiyo ya Wananchi kwa misimu mitatu yenye mafanikio.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotua mezani mwa Mwanaspoti, inaelezwa mwanzoni mwa msimu huu, licha ya kuwa Aziz KI kuwa na ofa nyingi mezani mwake, alikubali kusaini mkataba mpya wa kuendelea kukipiga Jangwani huku akiwa na sharti la kuondoka muda wowote ikiwa itatokea ofa nyingine nono zaidi.
Hata hivyo, Mburkina Faso huyo, alihitaji kuondoka wakati Yanga ikiwa imesimama yenyewe, ikumbuke kuwa ndani ya msimu huo 2023/24 ilikuwa mabegani mwake kuanzia katika michuano ya ndani hadi kimataifa.

Ndani ya msimu huo, Aziz KI hakushikika alifunga mabao 21 na kutoa asisti nane katika ligi ambako alikuwa mfungaji bora, akiisaidia Yanga kutwaa ubingwa wa ligi na kombe la FA huku pia ikifika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kulingana na upendo kwa mashabiki wa Yanga, nyota huyo alitia saini kwenye mkataba wa miaka miwili ambao utatamatika mwishoni mwa msimu ujao na kuzigomea timu kibao ikiwemo Mamelodi Sundowns, Kaizer Chief za Afrika Kusini, Al Ahly ya Misri na ASFAR ya Morocco.
Kwa mujibu wa taarifa inaelezwa, vigogo hao wa soka la Afrika na wamerudi kwa kasi huku safari hii vita hiyo ikiongozwa na Wydad Casablanca ambao inaelezwa wapo tayari kutoa Sh2.5 bilioni.
“Tayari mchakato wa kutafutwa mrithi wake umeanza, kuna ofa nyingi kubwa hivyo ni ngumu kwa awamu hii kukomaa na mchezaji, naweza kuwahakikishia kuwa Aziz anaasilimia kubwa za kuondoka mwishoni mwa msimu,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Haitakuwa kinyonge itakuwa ni biashara yenye faida kwa Yanga, kumekuwa na vikao mara kwa mara na mchezaji anahitaji kuondoka kwa heshima na ndiyo maana alikubali kuongeza mkataba mwanzoni mwa msimu. Aziz amefurahia wakati wake akiwa na hapa na amejisikia kama yupo nyumbani.”
Mbali na Wydad inaelezwa kuwa zipo timu kutoka Saudia, ambazo nazo zimeonyesha nia na kumhitaji nyota huyo, hivyo biashara inaweza kufanyika mwishoni mwa msimu huu ili kupata faida kwa mchezaji huyo.
MSIKIE WAKALA
Akifanya mahojiano ya moja ya chombo cha habari cha Afrika Kusini siku chache zilizopita, Mwakilishi wa mchezaji huyo, Zambro Traore alinuliwa akisema; “Nimewasiliana na Wydad Athletic Club kuhusu hamu yao ya kumchukua Aziz Ki, lakini hadi sasa sijapokea ofa rasmi kutoka kwa klabu hiyo ya Morocco.”
Wakala huyo aliongeza; “Mchezaji hana shida kuhama kwenda Morocco, na amekuwa akifuatilia ligi ya Morocco hivi karibuni. Nilipokea ofa kutoka kwa Al-Masry Club hapo awali, lakini ofa hiyo ilikataliwa na Yanga”

Mbali na Aziz KI, klabu ya Wydad imekuwa ikihusishwa pia kumpigia hesabu mshambuliaji Clement Mzize, ambaye mabosi wa Yanga wamelegeza sasa na kusema wapo tayari kumuuza, huku klabu iliyopo Ubelgiji ikitajwa kuvutia zaidi kwa kuweka dau la maana.