Yanayotokea ni kukiua, kukiimarisha Chadema?

Yanayotokea ni kukiua, kukiimarisha Chadema?

Mwanza. Swali kuu linalogonga vichwa vya wengi kuanzia ndani na nje ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ni je, yanayotokea yanakiua au yanakiimarisha?

Swali hilo linatokana na misukosuko inayoendelea kutokea ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Mwenyekiti wake, Tundu Lissu yuko mahabusu baada ya kushtakiwa kwa kesi ya uhaini inayomkabili ambayo haina dhamana, Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kutengua uteuzi wa viongozi wake wanane wa Kamati Kuu na Sekretarieti na baadhi ya viongozi na makada kutangaza kujivua uanachama ni miongoni mwa mambo yanayoibua maswali kuhusu hatima ya chama hicho.

Katika hoja zake, Ofisi ya Msajili inadai akidi ya kikao cha Baraza Kuu iliyowaidhinisha viongozi hao, akiwemo Katibu Mkuu, John Mnyika na Manaibu wake wawili wa Zanzibar na Bara haikutimia.

Katikati ya mtanziko huo, baadhi ya waliokuwa viongozi na makada wa Chadema tangu Mei 7, 2025 wanajivua uanachama wao, huku ufa uliotokana na mchakato wa uchaguzi wao wa ndani ya Januari 21, 2025 ukihusishwa.

Pazia la kujivua uanachama lilifunguliwa na baadhi ya wajumbe wa kundi la G55 ambao msimamo wao ulikuwa ni chama kushiriki uchaguzi mkuu ujao.

Msimamo huo unakinzana na ule wa chama kudai kwanza mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi kupitia kampeni yenye kaulimbiu ya ‘No reforms, No election.’

Miongoni mwa waliojivua uanachama wa Chadema ni pamoja na waliokuwa wajumbe wa Sekretarieti ya Chadema chini ya uongozi uliopita ambao ni Manaibu Katibu Mkuu, Salum Mwalimu (Zanzibar), Benson Kigaila (Bara) na aliyekuwa Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Catherine Ruge na Mwenyekiti wa Kanda ya Kati ambaye pia alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu, Devotha Minja.

Pia wamo aliyekuwa Katibu wa Sekretarieti ya Chadema, Julius Mwita, Mkurugenzi wa zamani wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema ambaye pia ndiye msemaji wa kundi la G55.

Pamoja na mambo kadhaa, wanaojivua uanachama wanataja chuki, ubaguzi na kutengwa kwa waliomuunga mkono Mwenyekiti wa zamani, Freeman Mbowe wakati wa uchaguzi mkuu wa chama Januari 21, mwaka huu kuwa miongoni mwa sababu za wao kujiondoa Chadema.

Kitendo cha kiongozi mkuu wa chama kuwa gerezani, Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kutowatambua na kuwaengua viongozi na wimbi la makada kujivua uanachama ndicho kinaibua siyo tu hofu, bali pia swali la je! huu ni mwanzo na mwisho wa Chadema?

Historia ya matukio yaliyowahi kushuhudiwa kwa vyama vya NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF) vilivyopoteza nguvu ya kisiasa na kuporomoka kutokana na sababu za ndani na nje ya vyama hivyo ni sababu nyingine inayoibua hofu miongoni mwa wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa kuhusu hatima ya Chadema.

Dk Bagonza atoa ushuhuda

“Kwa maoni yangu, Chadema itaimarika zaidi kwa kubakiwa na viongozi na wanachama waaminifu,’’ anasema Dk Benson Bagonza, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe.

Akijibu swali iwapo kitendo cha baadhi ya viongozi na wanachama kujivua uanachama kitakiathiri Chadema, Askofu Bagonza anasema; “Ni heri kuwa na watu wachache waaminifu kuliko kuwa na idadi kubwa ya watu ambao ni mamluki na wenye kuweka mbele matamanio yao binafsi kuliko malengo na matamanio ya kitaasisi.’’

Anasema Chadema imejijenga na kuwa taasisi kubwa inayokusanya watu wengi wenye nia, malengo na matamanio tofauti, ambao miongoni mwao, wamo wanaojiunga kwa ajili ya fursa za uongozi na wale wanaojiunga kwa kuvutiwa na kuamini katika sera, msimamo na malengo ya chama.

“Taasisi ikifikia hatua hiyo, ni lazima ikumbane na haya yanayotokea ndani ya Chadema. Wale waliojiunga kwa kufuata fursa wakibaini kuwa malengo yao hayawezi kutimia ni wazi watajiondoa na kujiunga kwenye vyama vingine kutimiza malengo yao,” anasema Askofu Bagonza

Anasema katika mafundisho ya kiimani kwa waumini wa dini ya Kikristo, hatua hiyo inaakisi maandiko yanayopatikana kwenye Biblia Takatifu katika kitabu cha 1. Yohana 2:19-21.

Kiongozi huyo wa kiroho anasema kupitia maandiko hayo, Mtume Yohana anasema; “Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangelikuwa wa kwetu, wangelikaa pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote walio wa kwetu.’’

Edwin Soko, mchambuzi wa masuala ya kisiasa anaunga mkono hoja ya Chadema kuimarika zaidi kutokana na yanayoendelea, ikiwemo baadhi ya viongozi na makada kujivua uanachama kwa sababu kitabakiwa na viongozi na wanachama waaminifu wanaoamini katika msimamo na malengo ya chama.

“Chama cha Mapinduzi (CCM) kimewahi kukimbiwa na viongozi na makada wenye ushawishi, akiwemo Kingunge Ngombale Mwiru, Edward Lowassa, wabunge na viongozi kadhaa wa mikoa na wilaya, lakini bado kiko imara.

Vivyo hivyo Chadema imewahi kukimbiwa na makada wake maarufu, lakini kimeendelea kuwa imara. Naamini hata sasa kitabaki imara baada ya mawimbi yanayoikumba,’’ anasema Soko.

Huku akitaja baadhi ya vyama, kikiwemo ANC ya Afrika Kusini na Kanu ya Kenya, Soko anasema; “Chama cha siasa kukimbiwa na viongozi na makada siyo tatizo…jambo muhimu ni jinsi inavyoshikilia msimamo na malengo yake, huku ikijifunza kutokana na yanayotokea.”

Heche na bahari kutema uchafu

Akijibu swali kuhusu yanayotokea ndani ya Chadema, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Bara), John Heche anasema; “Bahari hujisafisha yenyewe kwa kutema na kutupa uchafu ufukweni kwa njia ya maji kujaa na kupwa. Hicho ndicho kinachotokea ndani ya Chadema; wale wasio wa kwetu wanajiondoa wenyewe ili chama kibaki salama.”

Anasema yanayotokea, kuanzia kesi dhidi ya Mwenyekiti wao, Lissu, baadhi ya viongozi na wanachama kujivua uanachama na uamuzi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa yanakiimarisha zaidi chama hicho badala kukidhoofisha.

“Tumefanya ziara Kanda ya Kusini na Nyasa tukiwa na Mwenyekiti Lissu na juzi nimemaliza ziara Kanda ya Victoria na Serengeti; Watanzania wamejitokeza kwa wingi kutuunga mkono kwa kuhudhuria mikutano yetu hadi ile iliyofanyika nyakati za asubuhi. Umma unaunga mkono msimamo wetu wa kudai mabadiliko,’’ anasema Heche.

Makamu Mwenyekiti huyo pamoja na viongozi wengine, akiwamo Katibu Mkuu, John Mnyika na wajumbe kadhaa wa Kamati Kuu wamefanya ziara ya siku 10 katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kuanzia Mei 8, 2025 hadi Mei 17, 2025 ambako walihutubia mikutano ya hadhara ikiwa ni sehemu ya kampeni yao ya kudai mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi kupitia kaulimbiu ya ‘No reforms, No election.’

Anasema ziara ya Kanda ya Victoria na Serengeti inayoundwa na mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Simiyu, Mara na Shinyanga imefanyika muda ambao baadhi ya viongozi na wanachama wameutangazia umma uamuzi wa kujivua uanachama wa Chadema, lakini bado umati mkubwa umehudhuria mikutano yote ya hadhara iliyofanyika katika mikoa hiyo.

 “Chadema ni taasisi imara. Hakiwezi kufa kwa sababu ya baadhi ya viongozi na wanachama wanaojiondoa kwa sababu ya ndoto zao za ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu ujao, kutokana na msimamo wa chama wa kutoshiriki uchaguzi bila marekebisho ya sheria na mfumo wa uchaguzi,’’ anasema Heche.

Anasema hii siyo mara ya kwanza kwa Chadema kukimbiwa na viongozi na watu wenye majina makubwa na ushawishi na wala haitakuwa ya mwisho, kwa sababu kila mwanachama anayo sababu inayomfanya ajiunge au kujiondoa kwenye chama.

“Chadema tulikimbiwa na Makamu wenyeviti watatu, Dk Amani Kabour, Said Arfi na Profesa Abdallah Safari pamoja na Makatibu wakuu wawili, Dk Wilbroad Slaa na Dk Vicent Mashinji, lakini kimezidi kuimarika na kuwa imara zaidi kwa sababu umma unakiunga mkono,’’ anasema Heche.

Anataja orodha ya viongozi na makada wenye ushawishi waliowahi kujiondoa Chadema na chama hicho kubaki imara kuwa ni pamoja na waliokuwa Manaibu Makatibu wakuu, Zitto Kabwe na Shaibu Akwilombe, wabunge, mameya na wenyeviti wa halmashauri.

“Chama hiki hakijafa Awamu ya Tano tulipokimbiwa na wabunge wa majimbo zaidi ya saba na madiwani zaidi ya 300 waliojivua uanachama kuunga mkono juhudi; hata sasa hakitakufa,’’ anasema na kusisitiza Heche.

Anasema kamwe chama hicho hakitayumba katika msimamo wa kudai mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi utakaoweka sawa uwanja wa siasa kwa wagombea na vyama vyote vya siasa.

Bila kuingia kwa undani, Makamu mwenyekiti huyo amedai baadhi ya wanaojivua uanachama wameahidiwa nafasi za uongozi, ukiwemo ubunge na udiwani, ahadi anayoamini haitatimia kutokana na historia ya nyuma wakati wa uchaguzi wa mwaka 2020.

“Wanaojivua uanachama kutafuta fursa ya ubunge na udiwani kupitia vyama vingine wajiulize watashindaje kwa sheria na mfumo huu uliowazuia kushinda chaguzi zilizopita wakiwa Chadema yenye ushawishi na uungwaji mkono wa Watanzania wengi,” anasema na kuhoji Heche.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *