Yaliyojiri mkutano wa Waziri Kabudi, TFF, TPLB, Yanga na Simba Kwa Mkapa

SWALI ambalo huko mtaani mashabiki wanajiuliza ni kwamba, hiyo mechi ya Kariakoo Dabi ipo au haipo? Hiyo ni baada ya kuahirishwa kwa mchezo huo namba 184 wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Simba uliopangwa kufanyika Machi 8, 2025 kabla ya kuahirishwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).

Baada ya mchezo huo kuahirishwa na Yanga kushikilia msimamo wake kwamba haichezi mechi nyingine dhidi ya Simba bali inataka kupewa pointi tatu, ndipo Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi alipoitisha kikao na viongozi wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi Kuu ya Tanzania (TPLB), Klabu ya Yanga na Simba ili kutatua mgogoro uliopo.

Kikao hicho maalumu kwa ajili ya kujadili mustakabali wa mchezo huo wa Kariakoo Dabi, kilifanyika Alhamisi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

YANGA YATOKA NA MSIMAMO WAKE

Baada ya kikao cha kwanza kilichohusisha viongozi wa Yanga, ilishuhudiwa vigogo wa timu hiyo wakitoka saa 9:21 alasiri, ambapo wengi waligoma kuwa wazungumzaji sana wakimuachia rais wao Hersi Said kusema lolote.

Mara baada ya Hersi kutoka, alisema wamekuwa na kikao kizuri na wizara hiyo chini ya Waziri Kabudi na kilikuwa maalum kwa ajenda ya mchezo namba 184 ambao Yanga ilitarajiwa kucheza dhidi ya Simba.

“Uongozi wa Yanga tukiwa kamili na kamati yake ya utendaji tumeonana na mheshimiwa waziri, naibu waziri, katibu mkuu, naibu katibu mkuu na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa.

“Klabu ya Yanga imepata nafasi ya kufikisha yale ya msingi kabisa kutokana na mchezo ule na baada ya kufanya hivyo dhamira ya wizara ilikuwa kutaka kusikia kipi kinatoka kwa uongozi wa Yanga.

“Sisi kama viongozi jukumu letu ni kusimamia maslahi ya taasisi yetu ambayo taasisi yetu inasimamia wanachama na timu kwa ujumla.

“Kwahiyo tulikwenda kufikisha ujumbe wetu kuhusiana na msimamo wetu kama taasisi, Waziri na timu yake ikatusikiliza na wakapata ya kuuliza maswali na tukawajibu.

“Waziri amekuja na mwanzo mzuri akituambia nafasi hii sio kwamba ni eneo la kufanya uamuzi isipokuwa ni nafasi ya kutafuta suluhu juu ya tatizo lililotokea na akitaka kujifunza kutoka kwa Yanga nini hasa kimetusibu.

“Tumeweza kufikisha yote ambayo tulistahili kuyafikisha kama viongozi ambayo yanabeba ujumbe kama Kamati ya Utendaji na ujumbe wa wapenzi na mashabiki wetu nchi nzima.

“Ujumbe huu umemfikia waziri na timu yake wameupokea, tumewaachia waufanyie kazi na tumekubaliana tutakuwa na vikao endelevu ili kupata suluhu ya jambo hili.

“Nichukue fursa hii kuwaaambia wanachama na mashabiki wa Yanga sisi tupo hapa kwa ajili ya kusimamia maslahi ya klabu yetu, niwatoe hofu kwa namna yoyote kwamba viongozi wao ni imara na wako hapa kwa ajili ya kusimamia maslahi ya taasisi, wakae kwa kutulia, suluhu itakayopatikana tutarudi kwao kuwajulisha,” alisema Hersi.

Wakati hayo yakiendelea, taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zinabainisha kuwa Yanga wamebaki na msimamo wao uleule wa kutocheza mechi nyingine dhidi ya Simba bali wanataka kupewa pointi tatu.

Hata hivyo, taarifa hizo zimebainisha kwamba Waziri Kabudi amewaambia viongozi wa Yanga kikao hicho si kwa ajili ya kufanya uamuzi bali ni kusikiliza pande zote kabla ya kuangalia uwezekano wa kupata suluhu.

NJE YA UWANJA

Nje ya Uwanja wa Benjamin Mkapa, kulikuwa na mashabiki wa Yanga waliokuwa wakisubiri kwa hamu kuonana na viongozi wao na kutaka kufahamu nini wameenda kujadili.

Mashabiki hao walitulia pale walipowaona Injinia Hersi na Arafat Haji wakitoka kisha kupata neno kutoka kwa viongozi wao hao.

Hersi alizungumza na mashabiki hao kwa ufupi akiwaambia: “Wananchi eeeeh, si mko sawa? Nyie mlituchagua kuisimamia Yanga. Asanteni.”

Baada ya hapo, gari alilopanda Injinia Hersi na Arafat likaondoka huku mashabiki wa Yanga wakilisukuma na kuimba ‘hatuchezi, hatuchezi, hatuchezi.’

SIMBA YAKANA KUJADILI KUHUSU DABI

Simba nao walimaliza kikao chao na Wizara ya Utamaduni, Sanaaa na Michezo huku ikikana ajenda ya mchezo dhidi ya Yanga kuzungumzwa kwenye mkutano huo.

Simba iliingia kwenye mkutano huo saa 9:23 alasiri, msafara wao ukatoka saa 11:33 jioni ambapo viongozi wake wakakutana kwa kikao kifupi wakiwa wamesimama kabla ya mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu kuzungumza na waandishi wa habari.

Wakati Mangungu anatoka, amesema kikao chao na Waziri Profesa Palamagamba Kabudi kilikuwa na ajenda ya maendeleo ya soka nchini.

Mangungu alisema kwa kuwa mkutano huo umekuwa wa makundi tofauti, inawezekana serikali imetofautisha ajenda za kikao hicho ambapo klabu yake haikujadili mchezo namba 184 wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Simba ambao uliahirishwa Machi 8, 2025.

“Tunashukuru kwamba tumezungumza yote ambayo yalikuwa ni ya umuhimu, tumeyawasilisha kwa mheshimiwa waziri na timu yake lakini vikao vitaendelea,” amesema Mangungu huku akiongeza.

“Tumejadili maendeleo ya soka Tanzania, maendeleo ya soka yako mengi, kuna maeneo ambayo kama mnavyofahamu Waziri ni mpya katika wizara hii pamoja na uzoefu mkubwa alionao nadhani kuna mambo yalitakiwa tujadiliane kwa pamoja.

“Kwanza hata sijui kama Yanga walifika hapa, leo tumeanza kikao cha awali lakini kuna vikao vitaendelea, kikao chetu sisi hakihusiani na chao (Yanga) kama kingehusiana na chao nadhani tungekaa pamoja, wao walipokutana na waziri wanajua walichozungumza naye na kama walijadili hilo ni sawa lakini sisi haya ninayoyaeleza ndio tuliyojadili.”

Akijibu kuhusu hatma ya mchezo wa Kariakoo Dabi, Mangungu amesema: “Mamlaka si ilishasema mechi itapangiwa tarehe, kuna haja gani tena ya kusema hatma yake, mechi itachezwa siku nyingine kama itakavyopangwa, wao wameshikilia kanuni lakini kanuni hiyohiyo inaipa Bodi ya Ligi kuahirisha mechi pale inapoona inafaa.”

TFF, TPLB WATOKA ‘KIBUBU’

Hatimaye viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), na wale wa Bodi ya Ligi (TPLB) walimaliza kikao chao na wizara ya Utamaduni Sanaaa na Michezo chini ya Waziri Palamaganda Kabudi.

Viongozi hao wakiongozwa na Rais Wallace Karia, makamu wake wawili Athuman Nyamlani na Steven Mnguto pamoja na Katibu Mkuu wa TFF Wilfred Kidao walitoka uwanjani hapo saa 1:31 usiku.

Mara baada ya kutoka viongozi hao walionekana kutawanyika kwa makundi mawili ambapo wa kwanza alikuwa Mnguto ambaye aligoma kuongea lolote akisema Rais Karia ndiye ataweza kuongea.

“Kikao kimemalizika kweli lakini siwezi kuongea lolote labda mfuateni rais wangu ndiye anayeweza kusema lolote kwenye hili,”amesema Mnguto.

Wakati Mnguto akisema hivyo, Karia naye hakuwa tayari kuzungumza akitamka neno Moja pekee:”Siongei na mtu.” kisha akapanda kwenye gari na kuondoka uwanjani hapo.

Hali hiyo imeendelea pia kwa Kidao ambaye alisema:”Jamani wasubirini wizara watasema, Mimi sipo tayari kuongea lolote nawahi kupata futari,”amesema Kidao huku naye akiingia kwenye gari na kuondoka eneo hilo.

SERIKALI NAO KAMA TFF, TPLB

Wakati waandishi wa habari wakimsubiri kwa hamu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amabaye aliwaita viongozi hao wa soka na klabu kujadili mustakabali wa Dabi ya Kariakoo huenda akazungumza majadiliano yalivyokuwa na upi mustakabali wa sakata hilo, haikuwa kama ilivyotarajiwa.

Waziri Kabudi alitoka kikaoni akiongozana na naibu waziri wake Hamis Mwinjuma,  Katibu wa wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa na aliyekuwa rais wa TFFambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa, Leodgar Tenga.

Licha ya kuzongwa na waandishi wa habari wakitaka azungumze chochote kusuhu kikao, Waziri Kabudi hakuweza kusema lolote zaidi ya kuwapungia mkono waandishi wa habari walikuwa eneo hilo.

Naibu Waziri Hamisi Mwinjuma alinukuliwa akisema “mimi sina cha kuwaambia kabisa”

Katibu wa wizara hiyo Gerson Msigwa naye alisikika akisema “waandishi kwenye hili subirini, kuweni wapole mtapewa mrejesho”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *