Yaliyojiri kesi anayedaiwa kujeruhi, kutishia kwa bastola Club 1245

Dar es Salaam. Kesi inayomkabili mshtakiwa Derick Derick Junior, ambaye alionekana katika kipande cha picha jongefu (video) kilichosambazwa katika mitandao ya kijamii, akimshambulia mtu mwingine kwa mateke na kitako cha bastola, imepangwa kuanza kusikilizwa ushahidi Januari 21, 2025, katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni.

Tarehe hiyo ilipangwa jana Jumatano, Novemba 20, 2024 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Is-haq Kupa, wakati ilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali huku upande wa mashtaka ukieleza unatarajiwa kuwa na mashahidi 12 na kuwasilisha vielelezo kadhaa.

Derick (36), ambaye ni Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mkazi wa Salasala jijini Dar es Salaam anakabiliwa na mashtaka mawili, kujeruhi na kutembea na silaha hadharani kwa namna ya kuleta utisho, akidaiwa kutenda makosa hayo Oktoba 27, saa 12.30 asubuhi, eneo la Maaki katika Club ya 1,245, iliyopo wilayani Kinondoni.

Katika shtaka la kwanza, Anadaiwa katika shtaka la kwanza alimjeruhi usoni sehemu ya jicho na puani Julian Bujuru kwa kumpiga kwa kitako cha bastola.

Katika shtaka la pili, anadaiwa tarehe hiyohiyo katika eneo hilo ambalo ni klabu ya usiku, alitoa silaha na kumtishia Bujuru, kitendo ambacho kinatishia amani kinyume cha kifungu cha 84 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Jana Jumatano, kesi hiyo iliendelea kwa usikilizwaji wa awali, hatua ambayo mshtakiwa husomewa muhtasari kisha hupewa nafasi ya kubainisha mambo au maelezo anayoyakubali na yale asiyoyakubali.

Katika maelezo aliyoyakubali mshtakiwa huyo kupitia wakili wake Jeremiah Mtobesya alibainisha ni pamoja na jina lake na umri wake na makazi yake ni mkazi wa Salasala Kilimahewa, Salasala jijini Dar es Salaam.

Wakili Mtobesya alieleza pia mteja wake alijisalimisha mwenyewe polisi na akakabidhi bastola aina ya Berreta na kwamba anakubali kuwa anashtakiwa mahakamani hapo.

Mambo asiyokubaliana nayo mshtakiwa huyo ni pamoja na kabila lake kwamba si Mkurya bali yeye ni Mjita, kukamatwa na Polisi, kumiliki bastola, kuzozana na mlalamikaji Julian, kumshambulia kwa kumpiga kwa mateke na kitako cha bastola usoni jichoni na kuvuja damu.

Mengine ni asiyokubaliana nayo ni kutoa bastoa hadharani, mlalamikaji kupelekwa hospitalini, kusambaa katika mitandao ya kijamii kipande cha video kinachomuonyesha akitenda makosa hayo na kuhojiwa kwa kumpiga mlalamikaji.

Mwendesha mashtaka, wakili wa Serikali Mwandamizi, Saada Mohamed aliieleza mahakama wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo wanatarajia kuwa na mashahidi 12 na vielelezo kadhaa.

Wakili wa utetezi, Mtobesya alisema kwa upande wao watataja idadi ya mashahidi wao na vielelezo watakavyoviwasilisha hapo baadaye wakati watakapoanza kujitete.

Mshtakiwa huyo alipandishwa kizimbani mahakamani hapo Oktoba 29, 2024, siku mbili baada ya kipande hicho cha video kuonekana mitandaoni, na kusomewa mashtaka hayo na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Dickson Swai.

Hata hivyo, alikana mashtaka hayo na upande wa mashtaka ulisema upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa umekamilika na uliomba kupangiwa tarehe ya usikilizwaji wa awali.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Is-haq Kupa alisema dhamana ya mshtakiwa iko wazi kwa masharti ya kuwa na mdhamini mmoja anayetambulika kisheria atakaye saini bondi ya Sh8 milioni. Mshtakiwa huyo alitekeleza sharti hilo na akaachiwa huru kwa dhamana.