Yalipo matumaini ya kuimarika kwa Shilingi

Dar es Saalam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeeleza kuwa Shilingi ya Tanzania inatarajia kuimarika ifikapo mwishoni mwa mwaka huu kutokana na ongezeko la mapato ya fedha za kigeni linalotarajiwa kwa siku zijazo.

Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita viwango vya kubadilisha fedha Shilingi ya Tanzania na Dola ya Marekani vimebadilika kutoka Sh2,374.7 Januari 02, 2025  hadi Sh2,652.8 Aprili 4, 2025

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Naibu Gavana wa BoT, Dk Yamungu Kayandabila anayesimamia uchumi na sera za fedha amesema chombo hicho cha juu cha usimamizi wa fedha kinaangalia kwa karibu mwenendo viashiria vyote vinavyoongeza msukumo kwenye viwango vya kubadilishia fedha za kigeni.

“Tunatarajia kuwa Shilingi kuimarika sawa na ongezeko la mapato ya fedha za kigeni. Hadi Desemba tutalala usingizi na mvi zitapungua,” amesema Dk Kayandabila wakati akitoa taarifa ya Kamati ya Sera ya fedha (MPC).

Amesema kulingana na matarajio ya kuimarika kwa urari wa malipo ya kawaida, kamati ilibaini kuwa mabadiliko ya thamani ya shilingi katika robo ya kwanza ya 2025 ni ya msimu na hivyo Shilingi inatarajiwa kuimarika sambamba na ongezeko la mapato ya fedha za kigeni nchini.

Aidha, Machi 24, mwaka huu, Gavana wa BOT, Emmanuel Tutuba alitoa taarifa juu ya mwenendo wa Shilingi dhidi ya Dola akisema katika kipindi cha miezi kumi na miwili iliyopita hadi wakati huo, Shilingi ilishuka kwa asilimia 3.6.

Hata hivyo, amesema ni vyema kufahamu kuwa, katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2024, Shilingi iliongezeka thamani kwa asilimia 9.51, na kuwa sarafu iliyofanya vizuri zaidi duniani kabla ya kubadilika tena kuanzia Januari 2025.

Amesema kushuka kwa Shilingi kunatokana na mzunguko wa msimu wa mabadiliko ya fedha za kigeni nchini na sera ya fedha za kigeni ya Benki Kuu, inayoruhusu kubadilika kwa thamani ya sarafu kulingana na nguvu za soko kwani thamani yake huamuliwa na nguvu ya soko na upatikanaji wa fedha za kigeni sokoni.

Kuhusu mwenendo wa Shilingi mtaalamu wa Uchumi, Dk Felix Nandonde alisema ni muhimu kulinda sarafu ya ndani dhidi ya zile za kigeni kwa kuangalia sera zinavyowezesha uuzaji wa bidhaa, huduma na rasilimali katika masoko ya nje.

“Kufanya hivyo kutasaidia kuondoa mfumuko wa bei kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ikiwemo bidhaa za mafuta. Sasa sera itakayotungwa itasaidia kuhakikisha kuwa nchi inauza sana kuliko kununua,” amesema Dk Nandonde.

Amesema thamani ya shilingi ikianguka inaweza kufanya baadhi ya biashara katika soko la ndani kuyumba jambo ambalo linaloweza kufanya kufungwa kwake na kutengeneza tatizo la ukosefu wa ajira.

“Tuangalie zaidi sera zilizopo zinachocheaje kupelekea kuimarisha shilingi, moja ya jambo ni kuangalia uzalishaji wa malighafi, sera zinavyochochea uwekezaji katika viwanda na kuongeza thamani bidhaa zetu na uuzaji wake nje ya nchi,” amesema Dk Nandonde.

Katika kuuza huduma nje Dk Nandonde amesema baadhi ya nchi zimefika mbali na sasa zinauza rasilimali watu katika mataifa mbalimbali jambo ambalo linasaidia kurejesha fedha za kigeni.

Yalipo matumaini

Akiwasilisha taarifa ya MPC, Dk Kayandabila alisema Sekta ya nje imeendelea kuimarika na katika mwaka unaoishia Machi 2025, nakisi ya urari wa malipo ya kawaida ilikuwa takriban asilimia 2.6 ya Pato la Taifa ukilinganishwa na asilimia 3.7 kwa kipindi kama hicho mwaka 2024, kutokana na ongezeko la mauzo nje ya nchi hususan utalii, dhahabu, korosho na tumbaku.

“Kwa upande wa Zanzibar, urari wa malipo ya kawaida ulikuwa ziada ya dola milioni 563.5 ikilinganishwa na ziada ya dola milioni 407.4 kwa mwaka ulioishia Machi 2024, kutokana na ongezeko la mapato ya utalii,” amesema Dk Kayandabila huku akisisitiza kuwa ufanisi huo ni mzuri.

Amesema katika kipindi hicho, mfumuko wa bei kwa Tanzania Bara ulikuwa wastani wa asilimia 3.2. Kwa upande wa Zanzibar, mfumuko wa bei ulipungua kufikia asilimia 5.1 mwaka 2024, kutoka asilimia 6.9 mwaka 2023.

Mfumuko huo ulipungua hadi asilimia 4.8 mwezi Februari 2025 kutoka asilimia 5.3 mwezi Januari 2025, kutokana na kupungua kwa bei za chakula. Mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kuwa tulivu, ukiwa takribani asilimia 3.2 kwa robo ya pili ya mwaka 2025.

Kwa upande wa akiba za kigeni, Dk Kayandabila amesema akiba ya fedha za kigeni iliendelea kuwa ya kutosha katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 na hali inatarajiwa kuendelea kuwa hivyo kwa siku zijazo.

“Akiba ya fedha za kigeni ilifikia zaidi ya dola bilioni 5.6, kiasi kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi kwa takribani miezi 4.5, na inatarajiwa kubaki katika viwango hivi kwa robo ya pili ya mwaka 2025,” Amesema Dk Kayandabila.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *