Yajue mambo yanayoharibu afya ya masikio yako

Machi 3 ya kila mwaka ni siku ya kimataifa ya usikivu duniani.

Kauli mbiu ya mwaka huu inasema: “Badilisha mawazo: jiwezeshe kufanya huduma ya masikio na kusikia kuwa kweli kwa wote.”

Kwa kuhimiza watu kutambua umuhimu wa afya ya masikio na kusikia, kampeni hii inalenga kuwatia moyo kubadili tabia na mienendo hatarishi ili kulinda usikivu wao dhidi ya sauti kubwa.

Vile vile kuchunguza usikivu wao angalau kwa mwaka mara moja, kulinda usikivu kwa kutumia vifaa inapohitajika na kusaidia wale wanaoishi na matatizo ya kusikia.

Watu waliowezeshwa wanaweza kuleta mabadiliko makubwa ndani yao wenyewe na katika jamii kwa ujumla ikiwamo shule za msingi, vyuoni, ofisini na viwandani.

Kelele mbalimbali zinaweza kuvumilika lakini zinaweza kuzidi kupita kiwango cha ustahimilivu wa masikio na hivyo kumsababishia mtu madhara mbalimbali ya kiafya ikiwamo kusikia kengele masikioni., kutosikia kwa muda au kudumu, kichwa kuuma, kukosa utulivu wa kiakili, uchovu na kukosa usingizi.

Mtu mmoja anaweza kukutana na kila aina za kelele ambazo masikio huzimudu na nyingine kutozimudu hatimaye kupata madhara.

Kutokana na kuwepo katika maeneo ambayo yana tatizo la kuzagaa kelele kiholela,  uwezo wa kusikia unaweza kuwa ni tatizo la muda au kudumu.

Eneo la ndani ya sikio ndio hujeruhiwa kutokana na shinikizo kubwa la mawimbi na kusababisha udhaifu mkubwa wa kusikia.

Mawimbi yanayozidi kiwango cha uvumilivu kwenye eneo la ndani ya sikio yanaweza kumpata mtu mara kwa mara kiasi cha kuharibu eneo hilo kadiri siku anavyokutana na kelele hizo.

Eneo hili linaweza kuharibiwa kutegemeana na aina ya mawimbi, uzito wa sauti na kipindi cha kuwepo katika eneo hilo lenye kelele.

Hivyo kwa wale ambao wako katika maeneo yenye kelele ni vigumu kukwepa hivyo vizuri watumie vifaa tiba vyenye kupunguza ukali wa mawimbi ya sauti.

Muhimu kuepuka kutumia zile spika ndogo za masikoni kila mara huku ukiwa unaweka sauti kubwa kwani ni kama vile kuongeza ukubwa wa tatizo.

Epuka kukaa muda mrefu kwenye eneo lenye kelele au sauti kali  na fika kwa madaktari wa masikio mapema pale unapoona una dalili za kuathirika kwa masikio.

Muhimu pia jamii kufahamu sababu zingine kadhaa zinazochangia watoto kupoteza usikivu hatimaye kupata ulemavu wa kudumu wa usikivu angali ni bado wadogo.

Sababu hizo ni pamoja na mama wa mtoto kuugua magonjwa kama vile kaswende au rubella wakati wa ujauzito, kutumia dawa bila ushauri wa mtoa huduma za afya wakati wa ujujauzito.

Mambo mengine ni mtoto kupata matatizo wakati wa kuzaliwa kama Vile mtoto kukosa hewa ya kutosha katika ubongo au kupata jeraha la ubongo, mtoto kuzaliwa na uzito na uzito mdogo chini ya kilo 2.5, matatizo ya kurithi na kuzaliwa dosari ya maumbile.

Vile vile ugonjwa kwa mtoto kama vile uti wa mgongo, surua, mumps, shambulizi sugu la masikio au  maambukizi ya bakteria kwenye masikio.

Ni muhimu kwa wajawazito kuhudhuria kliniki na kushikamana na ushauri wa wataalam wa afya na pia kumfikisha mtoto mapema hospital pale anapoumwa.

Vile vile wazazi wawavalishe watoto vikinga mawimbi makali ya sauti wanapowapeleka katka maeneo yenye kelele mfano katika mechi za mipira na burudani za muziki.

Ni wakati wa jamii kuanza leo na kuhakikisha inabakia na usikivu mzuri maishani mwao. Zuia mambo yote yanayohatarisha afya sikio.