
Dodoma. Mkutano wa 19 wa Bunge la 12 utaanza Aprili 8, 2025, jijini Dodoma. Ni mkutano wa mwisho katika uhai wa Bunge la 12 chini ya Spika Dk Tulia Ackson na Naibu wake, Mussa Zungu, pamoja na wenyeviti watatu.
Katika mkutano huu wa mwisho wa uhai wa Bunge la Tanzania, kwa uzoefu, wabunge hupitisha miswada iliyobaki, hasa ile yenye umuhimu mkubwa kwa Serikali na wananchi, kuhakikisha inapita kabla ya Bunge kuvunjwa.
Ni katika mkutano huo inatarajiwa kuona wabunge, badala ya kuchangia mijadala, wakitumia fursa hizo kueleza wanayoyasimamia bungeni ili kushawishi wapigakura.
Hali ya kisiasa inatarajiwa kuwa ya joto zaidi kwa sababu wabunge wanajiandaa kwa uchaguzi mkuu Oktoba 2025. Wanaotaka kurejea bungeni wakihaha kutetea rekodi zao na kushambulia wapinzani wao kisiasa.
Yawezekana kwa baadhi yao kuanzisha michakato ya kujipanga kwa kufanya kampeni za chini kwa chini, wakijikita kutafuta fursa za kuchangia mijadala inayovutia wapigakura na kujenga taswira nzuri kwa umma.
Kupitia mkutano huo, yanaweza kuibuka masuala nyeti kama vile hoja za matumizi ya Serikali, miradi ya maendeleo, na changamoto zinazowakabili wananchi.
Kwa ujumla, mkutano unatarajiwa kuwa na mijadala yenye msisimko, ikichochewa na matarajio ya uchaguzi na hitimisho la kazi ya miaka mitano kwa wabunge waliopo.
Baadhi ya wabunge walianza pilikapilika kwenye Mkutano wa 18 wa Bunge uliomalizika Februari 2025, ambapo kwenye mijadala walijikita kuzungumzia majimbo yao badala ya hoja za kitaifa.
Yaliyojiri Bunge la 12
Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kulihutubia Bunge Juni 27, 2025, na kulivunja rasmi, watunga sheria hao wataondoka wakikumbuka walivyofanya mabadiliko ya uendeshaji wa mhimili huo wa dola kutokana na matukio na nyakati.
Baadhi ya mabadiliko yalikuwa ya lazima kutokana na mazingira na kauli za viongozi, akiwemo Spika wa Bunge.
Moja ya mabadiliko yalitokana na tahadhari ya ugonjwa wa Uviko-19, yaliyohusisha fedha na muda.
Wabunge walifanya mikutano kwa kutumia muda mfupi tofauti na kanuni zinavyoelekeza.Kwa kawaida, vikao huanza saa 3:00 asubuhi na kuahirishwa saa 7:00 mchana, kisha kurudi saa 11:00 jioni hadi 1:14 usiku.
Wakati wa Uviko-19, walilazimika kukutana saa 8:00 mchana na kuondoka saa 12:00 jioni. Utaratibu huo ulirejewa kutoka Bunge la 11, ulikoanza Machi 31, 2020.
Maswali ya wabunge yalitumwa moja kwa moja kwenye vishikwambi vyao ili kurahisisha namna ya kuyajibu. Maswali ya nyongeza yaliwahusu waulizaji pekee.
Matumizi ya Tehama yalichukua nafasi, ambapo kishikwambi kilitumika kwa jambo lolote lililohusu Bunge.
Tofauti na ilivyozoeleka, mawaziri na naibu mawaziri walijibu maswali wakiwa wamekaa kwenye viti vyao badala ya kwenda eneo maalumu kwa kazi hiyo. Hapakuwa na maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
Kumbi mbili zilitumika kwa wakati mmoja na zilifungwa runinga. Baadhi ya wabunge walitumia kumbi hizo kama kichaka cha kujificha, kwani walifika, wakasaini kisha kuondoka, ikihesabika wameshiriki vikao.
Mabadiliko mengine yalihusu mlango wa Spika kuingia bungeni.
Akiwa kwenye kiti cha Spika, Job Ndugai alitoa tangazo la kubadili kanuni za Spika kuingia ukumbini anapokwenda kuongoza vikao vya Bunge na anapotoka.
Badala ya kuingia kwa kutumia mlango wa mbele, ulianzishwa utaratibu wa Spika kuingia ukumbini kwa mlango wa nyuma unaotazamana na kiti cha Spika, ambao ni hatua zisizozidi 10.
Ndugai alitoa maelezo kuwa amefanya hivyo kwa kuiga mabunge mengine duniani, hivyo kuwataka wabunge wa Tanzania kuona ni kitu cha kawaida kwani ni sehemu ya maboresho.
Bunge Live
Baada ya kukwama kwa zaidi ya miaka sita, Bunge la 12 lilishuhudia mikutano yake ikirushwa mubashara.
Aprili 4, 2022, Spika, Dk Tulia alitangaza kurudishwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge (Bunge Live), akisema ni dai na hitaji la wananchi.
Kuondolewa kwa utaratibu huo kulizua malalamiko kutoka kwa wananchi wakisema uliwanyima haki ya kufahamu wawakilishi wao wanafanya nini kwenye vikao walivyowatuma, wengine wakisema Bunge lilikuwa gizani.
Hata hivyo, Bunge Live lilirejeshwa likiambatana na masharti kwamba hairuhusiwi kuchukua taarifa za moja kwa moja, zikiwamo video, hadi Kurugenzi ya Mawasiliano ya Bunge itoe kinachoitwa material—mkusanyiko wa taarifa zilizorekodiwa kwa shughuli zinazoendelea.
Wajibu maswali wabanwa
Naibu mawaziri, ambao kwa sehemu kubwa ndio wajibu maswali ya wabunge na mara chache mawaziri, hivi sasa ni marufuku kwao kutoka eneo la kujibia maswali baada ya kutoa majibu ya msingi.
Akimaliza kujibu, hulazimika kubaki eneo hilo hadi atakapohitimisha maswali ya nyongeza kwa idadi atakayoulizwa kwa maelekezo ya Spika.
Awali ilikuwa ni Waziri Mkuu pekee aliyetumia kipindi cha maswali ya papo kwa hapo Alhamisi kusimama hapo hadi ahitimishe kujibu maswali.
Ilivyo sasa, hairuhusiwi mjibu maswali kwenda kukaa kabla ya kuruhusiwa na Spika, Naibu wake au Mwenyekiti wa Bunge ambaye atakuwa amekalia kiti kwa wakati huo.
Mabadiliko ya kamati
Kulifanyika mabadiliko ya muundo wa Kamati za Kudumu za Bunge ili kuendana na muundo wa wizara zilivyo.
Kwa mabadiliko hayo, kulikuwa na nyongeza ya kamati za Bunge, huku uendeshaji wake ukitajwa kuwa tofauti ili kuendana na wakati.
Katika Bunge la 12, hapakuwa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Badala yake, kwa kutumia Kanuni za Bunge zilizorekebishwa, kulitambuliwa kuwa ipo kambi ya walio wachache.