Yahya Sinwar; Nembo ya Istiqama ya Palestina na Kusimama Imara Kukabiliana na Ughasibu

Natumai hujambo mpenzi msikilizaji popote pale ulipo. Nakukaribisha kutegea sikio kipindi hiki maalumu, ambacho kitasimulia maisha na ushujaa wa Yahya Sinwar, mmoja wa viongozi watajika wa Kambi ya Muqawama na miongoni mwa waasisi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina, HAMAS. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Yahya Sinwar alizaliwa mwaka 1962 katika kambi ya wakimbizi Wapalestina ya Khan Yunis iliyoko kwenye Ukanda wa Ghaza. Tokea mwanzo wake, maisha ya Sinwar yalikuwa ya tabu na shida za makazi kutokana na kuishi kwenye kambi za wakimbizi; hali na mazingira ambayo, yalimpa msukumo wa kuingia kwenye mapambano ya kukabiliana na uvamizi na ughasibu wa ardhi za Palestina unaofanywa na Wazayuni. Na ndiyo maana Sinwar, kama walivyokuwa watoto wengi wa Kipalestina, alipofikia rika la uchipukizi alijiunga na kambi ya Muqawama ya kupambana na utawala wa Kizayuni na akaja akawa mmoja wa waasisi wa tawi la kijeshi la Hamas la Brigedi za Izzuddin al-Qassam; brigedi ambazo, zikiwa ndiyo nguzo na mhimili wa kijeshi wa Hamas zimekuwa na nafasi kuu katika kupanga na kutekeleza operesheni za mashambulizi ya kijeshi dhidi ya uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na utawala haramu wa Israel.

Shahidi Sinwar alipoachiwa huru kutoka kwenye jela ya Israel

Kwa sababu ya harakati zake athirifu na za mtawalia katika vuguvugu la Muqawama, Yahya Sinwar alitiwa nguvuni mara kadhaa na askari wa utawala wa Kizayuni; na katika mwaka 1989 alihukumiwa na utawala huo dhalimu vifungo vinne vya maisha jela. Hata hivyo huo haukuwa mwisho wa mapambano ya Sinwar. Hata alipokuwa huko jela, mwanajihadi huyo aligeuka kuwa mmoja wa viongozi wanafikra wa wafungwa wa Kipalestina na akaweza kuwajenga wanamapambano wenzake kuwa watu wenye mioyo imara na thabiti ya mapambano. Huko kwenye gereza la utawala wa Kizayuni, Yahya Sinwar alijifunza lugha ya Kiibrenia; na kwa muda wa miaka mingi alipokuwa kifungoni aliandika na kuchapisha vitabu kadhaa kikiwemo cha riwaya yake maarufu ya “Mwiba na Karafuu”; kitabu ambacho, baada ya kuingia kwenye orodha ya vitabu vilivyouzwa kwa wingi zaidi kwenye tovuti ya Amazon, kilikuja kuondolewa katika tovuti zote kutokana na mashinikizo ya utawala wa Kizayuni.

Lakini mbali na kualifu riwaya ya Mwiba na Karafuu, Sinwar alitarjumu pia vitabu vingine vitano vya Kiibrenia na Kiingereza na anatambulika kama mmoja wa wafungwa wa kisiasa duniani aliyefanya kazi kubwa zaidi katika uga wa fasihi. Watu wengi waliokuwa karibu naye, wakimtambua Sinwar kama shakhsia wa kiutamaduni, aliyejidhihirisha katika sura ya mwanahamas, mwanamapambano na mpiganaji vita. Lakini pamoja na masuala hayo ya kiutamaduni, Yahya Sinwar hakulisahau piganio na lengo lake kuu, ambalo ndilo lengo la Wapalestina wote, yaani ukombozi wa ardhi ya Palestina wa kuitoa kwenye makucha ya maghasibu wa Kizayuni. Alianzisha mawasiliano imara yaliyojenga mshikamano madhubuti kati ya wanachama mbalimbali wa mavuguvugu tofauti ya Muqawama, na akaitumia jela kama uwanja wa kueneza fikra za kimuqawama.

2011, ulikuwa mwaka wa mabadiliko makubwa na muhimu zaidi katika maisha ya Sinwar. Katika makubaliano ya kubadilishana mateka kati ya Hamas na Israel, yaliyojulikana kama “Mabadilishano ya Gillad Shalit”, Yahya Sinwar aliachiwa huru baada ya kusota kwenye gereza la utawala wa Kizayuni kwa muda wa miaka 22. Kuachiwa kwake huru, sio tu kuliimarisha moyo wa Muqawama katika Ukanda wa Ghaza, lakini kulimgeuza pia Sinwar kuwa mmoja wa shakhsia muhimu zaidi wa Muqawama wa Palestina.

Shahidi Yahya Sinwar (kushoto) alipokutana na Kiongozi Mkuu wa Mpinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei, Tehran baada ya kutoka jela

Baada ya kuachiwa huru, Yahya Sinwar alibadilika kwa kasi na kuwa mmoja wa shakhsia wakuu wa harakati ya Hamas na mhimili wa upitishaji maamuzi ya kisiasa na kijeshi katika Ukanda wa Ghaza. Kutokana na ushujaa na msimamo wake thabiti, alitambuliwa na watu wa Ghaza kama shujaa wa taifa; shakhsia ambaye kwa weledi na umahiri aliokuwa nao wa masuala ya kimkakati, aliweza kutoa mchango muhimu katika kuimarisha uwezo wa kujihami na wa kiulinzi wa Hamas; na uongozi wake ulikuwa na taathira kubwa katika kuongeza uwezo wa kijeshi na kiulinzi wa Wapalestina. Kwa uwezo wake mkubwa wa kuongoza vikosi vya Muqawama, Sinwar alifanikiwa kutoa changamoto kubwa na kali kwa Israel na kuifanya Ghaza ngao imara ya kukabiliana na mashambulio makali ya utawala huo ghasibu.

Moja ya sifa ya kipekee aliyokuwa nayo Sinwar ilikuwa ni uwezo mkubwa wa kuratibu operesheni na upangaji maamuzi ya kimkakati. Baada ya kuachiwa huru kutoka kwenye jela za utawala wa Kizayuni, na kwa kutumia umahiri wake, Yahya Sinwar aliweza kuimarisha kwa kiwango kikubwa sana uwezo wa kiulinzi wa Hamas. Kwa kutumia uzoefu na tajiriba alizopata katika vita vilivyopita na nyenzo haba za ndani, kiongozi huyo wa Muqawama aliweza kuyaunganisha na kuyaongoza matawi mbalimbali ya Muqawama ndani ya Palestina, kufika hadi ya kutoa changamoto mpya za kijeshi kwa utawala unaoikalia Quds tukufu kwa mabavu.

Moja ya mafanikio makubwa aliyopata Sinwar katika uongozi wake ni kuongeza uwezo wa Hamas wa kujiundia yenyewe makombora. Kwa kuandaa mipango na mikakati makini aliwezesha kuongezwa kiwango cha uundaji zana za kivita katika mazingira magumu iliyokuwa nayo Ghaza ya kuwekewa mzingiro na kuupa Muqawama ujasiri wa kutoa jibu kali kwa mashambulizi ya kila leo ya Israel. Mafanikio hayo yaliifanya Hamas itambulike kama harakati athirifu na yenye sauti katika eneo.

Katika kipindi chote cha kuwemo kwake kwenye kambi ya Muqawama, Yahya Sinwar alikuwa daima akipigania kudumishwa mshikamano na umoja kati ya vikosi vya wanamuqawama. Kwa kuendeleza mshikamano huo kati ya wanachama wa harakati ya Hamas na harakati zingine za Palestina, alifanikiwa kupunguza sana tofauti za ndani na kuweza kujenga kambi moja iliyoungana, ya kukabiliana na utawala wa Kizayuni.

Katika uga wa kimataifa pia, Sinwar alitoa mchango mkubwa katika kupatikana uungaji mkono duniani kwa Muqawama wa Wapalestina. Kwa kujenga uhusiano na nchi za kanda na kufanya juhudi za kutafuta uungaji mkono wa kisiasa na kifedha kwa Muqawama, Sinwar aliweza kuimarisha nafasi ya Wapalestina katika upeo wa ulimwengu mzima. Yahya Sinwar, alikuwa siku zote akitilia mkazo ulazima wa kushirikiana na nchi zingine na harakati nyingine za Muqawama katika eneo. Kwa hatua yake ya kuanzisha miungano kadhaa ya mavuguvugu ya Muqawama katika nchi za kanda hii, aliweza kubuni mtandao mpana wenye uratibu dhidi ya Israel na sera zake za hujuma na uvamizi. Sinwar alikuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba Muqawama wa Palestina ni Muqawama halali na wa kisheria, ambao lengo lake ni kuilinda ardhi ya Palestina na kutetea haki za wananchi wa Palestina.

Lakini mbali na uga wa kijeshi, Yahya Sinwar alikuwa akipendwa sana katika nafasi yake ya kuwa ni kiongozi wa watu. Alikuwa daima akiyashughulikia kwa uzito maalumu matatizo na mahitaji ya watu wa Ghaza na akijaribu kuboresha maisha ya Wapalestina katika mazingira magumu yaliyowakabili ya kuwekewa mzingiro wa pande zote na utawala wa Kizayuni. Kwa kusimamia kwa umakini mkubwa rasilimali zilizopo, na kuziwekea utaratibu sahihi wa ugawaji na utumiaji katika kipindi cha hali ngumu ya kiuchumi, Sinwar aliweza kwa kadiri ilivyowezekana kudhamini mahitaji ya msingi ya watu wa Ghaza na kuwapunguzia mibinyo na dhiki za kiuchumi zilizotokana na mzingiro wa miaka kadhaa wa utawala dhalimu wa Israel. Gazeti la Financial Times lilikiri katika moja ya ripoti zake lilipoandika yafuatayo: “Sinwar amegeuka kuwa shakhsia wa ngano na wa kipekee katika Ukanda wa Ghaza. Wapalestina wengi sana wanajivunia naye; na ni mtu anayependwa mno, na watu wa Palestina”.

Shahidi Yahya Sinwar akiamkiana na wananchi Wapalestina wa Ghaza

Katika medani ya kijeshi, moja ya hatua za aina yake aliyochukua Sinwar ilikuwa ni kupanua wigo wa mbinu za kivita na kutumia teknolojia ya kisasa katika mapambano dhidi ya uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na utawala wa Kizayuni. Kwa kupanua mashambulizi ya utumiaji wa ndege zisizo na rubani za droni na kutumia teknolojia mbalimbali za kisasa, aliweza kulipa mashinikizo mapya ya kijeshi jeshi la utawala bandia wa Israel. Teknolojia hizo ambazo zimetumiwa katika uvamizi wa karibuni wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza zimeonyesha namna Hamas ilivyopiga hatua kijeshi chini ya uongozi wa Yahya Sinwar na kuleta mtikisiko ulioyumbisha kambi ya adui Mzayuni.

Kwa kutumia tajiriba na uzoefu wa huko nyuma sambamba na suhula na nyenzo haba za ndani, Sinwar aliweza kuufikisha Muqawama wa Wapalestina kwenye upeo mpya wa utayari wa kijeshi na kulifanya jeshi la Israel likabiliwe na changamoto mpya na za aina tofauti. Hii imemaanisha kwamba, Israel haiwezi tena kuendeleza uvamizi na hujuma zake za kijeshi kwa kutegemea mbinu za huko nyuma; na kwa hiyo ikae na kufikiria mikakati mingine mipya ya kukabiliana na Muqawama wa Wapalestina.

Hatua kadha wa kadha za kishujaa, istiqama na msimamo thabiti wa Yahya Sinwar vimemgeuza mwanamapambano huyo kuwa nembo ya Muqawama na istiqama ndani ya nyoyo za wananchi wa Palestina. Kwa moyo imara na azma thabiti aliyokuwa nayo, Yahya Sinwar alikuwa akisisitiza kila mara juu ya kupigania na kutetea haki za Wapalestina na hakukubali kwa namna yoyote ile kurudi nyuma au kulegeza msimamo katika mapiganio matukufu ya Muqawama. Yahya Sinwar aliwahi kutangaza mara kadhaa kwamba, mapambano ya Wapalestina yataendelea hadi ardhi zote zinazokaliwa kwa mabavu zitakapokombolewa na wakimbizi wote Wapalestina kuweza kurejea makwao.

Kwa ushujaa na weledi aliokuwa nao, kiongozi huyu mkubwa wa Muqawama aliweza kutoa changamoto kwa maadui wa Palestina na kusambaratisha mara nyingi malengo yao maovu dhidi ya ardhi hiyo.

Na hatimaye Yahya Sinwar, ambaye aliendeleza mapambano dhidi ya utawala vamizi wa Israel hadi tone la mwisho la damu yake, huku taswira za ushujaa wake na kujitoa mhanga kwake zikiakisiwa duniani kote, alifikia daraja ya juu na tukufu ya kufa shahidi kwenye medani ya makabiliano ya ana kwa ana na wanajeshi wa utawala dhalimu wa Kizayuni.

Shahidi Yahya Sinwar ameonyesha kwa mara nyingine tena kwamba, Muqawama wa Palestina ungali hai na imara; na hakuna shaka yoyote kuwa, kwa kuendelea kuwepo uongozi wa watu kama Yahya Sinwar, mustakabali wa Muqawama wa Palestina utazidi kung’ara na utazidi kuliletea taifa hilo heshima na fakhari. Kwa irada yake madhubuti mithili ya chuma na moyo wenye matumaini kamili, aliendeleza njia ya mapambano ili kuvionyesha vizazi vijavyo kuwa, njia ya mapambano kwa ajili ya ukombozi, haki na uadilifu haitasimama katu. Hakuna chembe yoyote ya shaka, kuwa Yahya Ibrahim Hassan Sinwar, akiwa ni nembo ya Itiqama na Muqawama, ataendelea kubaki nyoyoni mwa wananchi wa Palestina; na mapambano yake yatakipa ilhamu kizazi cha wanamapambano wa Palestina wanaoendeleza juhudi za kupigania uhuru, izza na heshima yao. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/